THE UNITED REPUBLIC OF TANZANIA
DIRECTORATE OF PRESIDENTIAL COMMUNICATIONS

Rais Jakaya Mrisho Kikwete amewaonya wananchi wa
Wilaya ya Ludewa wasiwe hodari ya kuuza ardhi na mashamba yao ambayo yatakuwa
mali sana katika miaka michache ijayo kufuatia matunda makubwa ya uwekezaji wa
Serikali katika miradi ya chuma, makaa ya mawe na madini mengi yanayopatikana
kwenye Wilaya hiyo.
Badala yake, Rais Kikwete amewataka wananchi wa
Wilaya hiyo kuchangamka mapema kuwekeza katika raslimali hizo kubwa
zinazopatikana katika Wilaya hiyo ya Mkoa wa Njombe.
Rais Kikwete alikuwa anazungumza leo, Jumatatu,
Oktoba 21, 2013, wakati alipoitembelea Wilaya huyo ikiwa ni sehemu ya ziara
yake ya siku saba katika Mkoa wa Njombe ambako tayari ametembelea Wilaya za
Njombe, Makete na Wanging’gombe.
Rais Kikwete amewaambia wananchi wa Ludewa
katika mkutano wa hadhara uliofanyika mjini Ludewa: “Msiwe hodari wa kuuza mashamba
na ardhi yetu na nyie mkabakia kama vibarua kwenye maeneo yenu,”
amesema Rais Kikwete na kuongeza:
“Msipochangamka mapema na kuanza kuangalia namna
ya kunufaika na raslimali za hapa, mtageuka manokoa wa watu wengine kwenye
ardhi yenu wenyewe. Baada ya muda mfupi raslimali hizi zikianza kuonekana
vizuri zaidi wajanja watakuwa wengi hapa na wanaojua pesa watafurika hapa
kwenu. Hivyo, jiandaeni mapema.”
Mbali na madini mengi na ya kila aina ambayo
yamethibitika kuwemo katika Wilaya ya Ludewa, Wilaya hiyo pia ina raslimali
mbili kubwa za makaa ya mawe katika eneo la Mchuchuma na miamba ya chuma katika
eneo la Liganga, maeneo yanayotenganishwa na umbali wa kilomita 45 tu.
Inakadiriwa kuwa miradi yote mikubwa na yenye
thamani ya mabilioni ya dola za Marekani itaweza kuajiri maelfu ya watu moja
kwa moja ama ama wategemezi wa waajiriwa wa moja kwa moja.
Rais Kikwete amesema kuwa kulingana na takwimu
za kitaalamu, eneo la makaa ya mawe la Mchuchuma lina kiasi cha tani milioni
370 na eneo la milima ya chuma ya Liganga lina kiasi cha tani milioni 200,
madini ambayo yatachimbwa kwa miaka inayokadiriwa kufikia 70 tokea siku
uchimbaji ukianza.
Ili kuweza kuanza uchimbaji wa madini hayo,
kiasi cha dola za Marekani bilioni 1.3 zitawekezwa katika mradi wa Mchuchuma na
kiasi cha dola bilioni 1.7 zitawekezwa katika mradi wa Liganga.
Rais Kikwete amesema kuwa ili kujiandaa na
Watanzania kunufaika na miradi hiyo mikubwa, Serikali yake imeamua kujenga Chuo
cha Ufundi Stadi (VETA) kikubwa katika eneo la Shauri Moyo, Kata ya Lugarawa,
kitakachotoa mafunzo maalum yanayohusiana na utaalam wa makaa ya mawe, chuma na
madini.
Tayari
Serikali imetoa Sh. bilioni nne kwa ajili ya ujenzi huo kwenye eneo la ekari
78.2 ambalo limetolewa na Serikali tayari kwa ujenzi kuanza Machi, mwakani,
2013.
Rais Kikwete pia ameutaka uongozi wa Wilaya ya
Ludewa na Mkoa wa Njombe kuanza maandalizi ya kuyapanga vizuri maeneo ya
Liganga na Mchuchuma kwa ajili ya uwekezaji huo mkubwa. “Anzeni kupanga namna maeneo hayo
yatakavyokuwa ili tuwe na miji mizuri na ya kuvutia katika maeneo hayo.”
Imetolewa na:
Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais,
Ikulu,
DAR ES SALAAM.
21 Oktoba, 2013


Post a Comment