|
MH. LUGOLA |
*Wasema imevunja haki za binadamu, mifugo
*Kamati teule ya Bunge yaundwa kuchunguza
SERIKALI
imesitisha ‘Operesheni Tokomeza’ iliyokuwa imeanzishwa kwa ajili ya
kupambana na vitendo vya ujangili katika maeneo mbalimbali nchini. Hatua
hiyo imekuja baada ya wabunge kupiga kelele wakipinga operesheni hiyo,
wakisema inakiuka haki za binadamu.
Wakizungumza bungeni jana,
wabunge mbalimbali walisema operesheni hiyo imeleta matatizo makubwa,
ambapo matukio mengi yamefanywa ikiwamo baadhi ya watu na mifugo kuuawa
kwa kisingizio cha kusaka majangili. Wabunge hao wamekwenda mbali zaidi
na kuitaka Serikali kuwashughulikia watendaji wote waliohusika katika
mauaji ya raia na mifugo na wote wachukuliwe hatua.
Serikali kupitia tamko la Waziri wa Maliasili na Utalii, Balozi
Khamis Kagasheki, imeridhia hoja za wabunge na kuamua kusitisha
operesheni hiyo.
“Wote waliokiuka utaratibu na maagizo ya operesheni, ni lazima hatua stahili zichukuliwe,” alisema Kagasheki.
Baadhi
ya wabunge walisimama na kuomba mwongozo wa spika wakitaka Bunge
lisitishe shughuli zake na badala yake wabunge wapate fursa kujadili
operesheni hiyo ambayo imeleta madhara kwa jamii.
Hatua hiyo
ilikuja baada ya Waziri wa Maliasili na Utalii na Waziri wa Mifugo na
Maendeleo ya Uvuvi, Dk. Mathayo David Mathayo kuwasilisha taarifa zao
ambazo hazikuwaridhisha wabunge.
Said Nkumba
Mbunge wa Sikonge, Said Nkumba alisema migogoro
ya wafugaji na wakulina ni ya muda mrefu, lakini Serikali imekuwa
ikishindwa kutatua migogoro hiyo.
“Naomba niweke msimamo wangu,
haiwezekani mpaka mambo yanakuwa makubwa kiasi hiki watu wanaathirika,
mali zao zinaathirika uhai unapotea ndipo Serikali inakuja hapa kutoa
maelezo.
“Kazi ya Serikali ilikuwa kuendelea na hili zoezi
walilokuwa nalo, naomba Bunge lichukue nafasi yake ya Bunge liunde
kamati itakayofanya kazi ya uchunguzi kwa kina.
“Huko vijijini
kuna matatizo makubwa wakulima na wafugaji hawaelewani, kila siku
Serikali badala ya kutatua tatizo inaenda kutatua migogoro kwa kutumia
mabomu na bunduki, hatuwezi kuendelea na utaratibu wa namna hii.
“Wanaofanya
operesheni wanatumia maneno mabaya kwamba wametumwa na Ikulu na uongozi
wa juu kwamba hawawezi kuhojiwa, je walitumwa kweli na Rais au
Serikali?
“Tunataka tupate taarifa za kina nani wamechukuliwa hatua hadi sasa na majangili wangapi wakubwa wamekamatwa,” alisema Nkumba.
Kangi Lugola
Kwa upande wake, Mbunge wa Mwibara, Alphaxad
Kangi Lugola alisema taarifa za mawaziri hao zimetokana na shinikizo la
Bunge ambazo zimejaa maneno matamu ya kudanganya Bunge na Watanzania.
“Waziri
wa mifugo katika taarifa yako unasema unawapa pole watu kwa usumbufu
uliowakuta, hivi kweli jambo hilo limekuwa usumbufu wakati watu
wamepoteza maisha?
“Waziri wa Maliasili na Utalii anasema
tokomeza ujangili, kumbe ni tokomeza ufugaji na miradi ya watu kujipatia
utajiri, mawaziri hawa wataponea wapi kama damu za watu zimepotea.
“Kama
Bunge lako litakubali maelezo ya Serikali kwamba ikatathimini hilo
haliwezekani, wakati Jeshi la Polisi limeua watu, maaskari wa wanyama
pori wameua watu.
“Serikali haiwezi kuwatathimini watu ambao
wamewashinda kwa muda mrefu, kazi hii lazima ifanywe na kamati teule ya
Bunge lako tukufu,” alisema Lugola.
Dk. Titus Kamani
Mbunge wa Busega, Dk. Titus Kamani, aliitupia lawama Serikali na kusema haina tofauti na ugonjwa wa sotoka unaoua mifugo.
Ester Bulaya
Mbunge
wa Viti Maalumu, Esther Bulaya (CCM), alisema anashangaa kusikia
Serikali inasema imepata mafanikio katika operesheni hiyo kwa kukamata
ng’ombe magari na meno ya tembo, badala ya kuwakamata majangili.
“Kama
Bunge lazima tufanye kazi yetu, naunga mkono hoja ya kuanzishwa kamati
teule, mtandao wa ujangili ni mkubwa, mawaziri wa wizara wanahusika
hakuna mkakati wa kupambana na ujangili,” alisema Bulaya.
John Shibuda
Mbunge wa Maswa Magharibi, John Shibuda
(CHADEMA), alisema Waziri Mkuu Mizengo Pinda, anapaswa kulaumiwa kwa
kuwa amekaa kimya wakati taarifa zote za kiintelijensia zinamfikia.
“Wizara
ya mifugo ni hasi kwa maslahi ya wafugaji, TAMISEMI ni jiko la dhuluma
na jiko la mkakati hasi dhidi ya wafugaji, sheria zilizozaa dhuluma zote
zifutwe.
“Tamisemi ipo chini ya Waziri Mkuu, wabunge wa CCM
acheni kulalamika, waanze kumuuliza Waziri Mkuu aeleze sababu ya kukaa
kimya na kumuachia rais kila kitu akifanye yeye, ningekuwa waziri mkuu
ningejiuzulu,” alisema Shubuda.
Kamati Teule
Baada ya Serikali kusitisha operesheni hiyo,
Bunge limeunda kamati teule kwa ajili ya kuchunguza mauaji ya watu na
mifugo yaliyofanywa na watumishi wakati wa utekelezaji wa operesheni
hiyo.
Mbunge wa Kilolo, Peter Msolla (CCM), ndiye alitoa hoja ya
kuundwa kwa kamati hiyo, ambayo iliungwa mkono na wabunge mbalimbali
waliochangia mjadala huo.
Mbunge wa Kasulu Mjini, Moses Machali
(NCCR- Mageuzi) alitaka kamati teule inayoundwa na Bunge ichunguze
mauaji ya mifugo yaliyofanywa na iende mbali zaidi kwa kuwapima akili
waliofanya mauaji hayo.
“Kitendo kilichofanywa na maafisa wa
operesheni dhidi ya majangili, walichofanya ni zaidi ya ugaidi, twende
mbali zaidi katika kamati kuangalia hata kuwapima akili zao, jambo hili
haliwezi kufanywa na mtu mwenye akili timamu,” alisema.
Akichangia
mjadala huo, Mbunge wa Mkanyageni, Habibu Mnyaa (CUF) alisema mtu
anatakiwa alindwe pamoja na mali zake, lakini katika operesheni hiyo
watu walinyang’anywa mali zao, wengine walisingiziwa ugaidi.
Alisema hadidu za rejea ziende mbali kuthibitisha ugaidi wao, kwani hilo litasaidia kuona haki inatendeka.
Mbunge
wa Longido, Michael Laizer (CCM), alisema katika hadidu za rejea
yaongezwe majukumu katika kamati ikiwemo kutafuta ni kwanini operesheni
hiyo badala ya kutafuta majangili wakauawa mifugo na wafugaji.
“Lazima
tukubali hoja ya kuunda kamati ili kuondoa migogoro ya wakulima na
wafugaji, mifugo imepigwa risasi imekufa na mashamba yameteketea,”
alisema.
Hadidu za rejea
Spika wa Bunge, Anne Makinda alimtaka
Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Kilimo, Mifugo na Ardhi, Profesa Peter
Msolla kuhitimisha hoja yake aliyotoa.
Msolla alilitaka Bunge kuunda kamati hiyo ambayo pamoja na mambo mengine itashughulikia migogoro ya wafugaji na wakulima.
Msola
alizitaja hadidu za rejea sita. Hadidu hizo ni pamoja na kuangalia na
kuchambua masuala ya ardhi na kuangalia mikakati mbalimbali ya Serikali
na kuchunguza utekelezaji wake.
Nyingine ni kuchambua mikakati na
kusuluhisha migogoro kati ya wafugaji na wakulima, kuangalia mikakati
ya kulinda vyanzo vya maji na uhatibifu mazingira na kutoa mapendekezo
na kuangalia mambo mengine yoyote ambayo kamati itaona inafaa.
Baada
ya Msolla kuhitimisha hoja hiyo aliwaruhusu wabunge kuziboresha hadidu
hizo, ambapo Mbunge wa Ubungo, John Mnyika (Chadema) alitaka kabla ya
kamati hiyo kuanza kazi ipitie taarifa za tume na kamati mbalimbali
zilizowahi kuundwa kuchunguza masuala ya ardhi.
Mnyika pia
alitaka Kamati hiyo iangalie suala la uwajibikaji kwa viongozi wote
watakaobainika walifanya uzembe wa kiutendaji katika suala hilo.
Kwa upande wake, Spika Makinda alisema majina ya wajumbe watakaounda kamati hiyo yatatangazwa Jumatatu.
on Saturday, November 2, 2013
Post a Comment