Young
Africans imerejea jana jijini Dar es salaam na kuendelea na maandalizi
ya mchezo wa mwisho wa Ligi Kuu ya Vodacom dhidi ya timu ya Simba SC
mchezo utakaopigwa kwenye dimba la Uwanja wa Taifa siku ya jumamosi
majira ya saa 10:00 kamili jioni kwa saa za Afrika Mashariki.
Kikosi
cha Young Africans kimeweka kambi eneo la Bahari Beach kujiandaa na
mchezo huo ambao ni muhimu kwa watoto wa Jangwani kuhakikisha wanafanya
vizuri na kupata ushindi mzuri wa kumalizia ligi.
Kocha
Mkuu wa Young Africans amesema vijana wake wapo katika hali nzuri
kuelekea mchezo wa jumamosi, kwani hakuna majeruhi hata mmoja katika
kikosi chake cha wachezaji 20 walioingia kambini kujiandaa na mchezo
huo.
Hans
amesema Vijana wake wanazidi kuonyesha mabadiliko makubwa kiuchezaji,
mafunzo yake wanaonekana kuyaelewa vizuri hivyo kikubwa anaomba
waendelee kuwa katika hali nzuri kuelekea mchezo na ana imani kikosi
chake kitaibuka na ushindi.
"Nina
uzoefu na michezo wa watani wa jadi, huwa inakua migumu kwa kila timu
kutokana na kila timu kutaka kuonyesha wapenzi, washabiki na wanachama
wake kuwa wako vizuri, Simba ni timu nzuri lakini bado sioni kikwazo cha
kutuzuia tusiibuke na ushindi katika mchezo huo" alisema Hans.
Leo
jioni kikosi kitafanya mazoezi katika Uwanja wa Bko Beach Veterani
ikiwa ni sehemu ya maandalizi ya mchezo huo wa jumamosi ambapo kikosi
cha Young Africans mpaka sasa kinashika nafasi ya pili kikiwa na pointi
55 huku kikiwa kimecheza michezo 25, Simba wakiwa nafasi ya nne na
pointi 37 huku wakiwa wamecheza michezo 25.
Kikosi cha Young Africans kilichoingia kambini kujiandaa na mchezo huo ni:
Walinda milango: Deogratias Munish "Dida" na Ally Mustafa "Barthez"
Walinzi: Juma Abdul, Mbuyu Twite, Oscar Joshua, Ibrahim Job, Rajab Zahir, Kelvin Yondani na Nadir Haroub "Cannavaro"
Viungo: Frank Domayo, Hassan Dilunga, Salum Telela, Hamis Thabit, na Nizar Khalfani
Washambuliaji: Didier Kavumbagu, Mrisho Ngasa, Jerson Tegete, Hamisi Kizza, Hussein Javu na Saimon Msuva.
Post a Comment