Waziri
Mkuu, Mizengo Pinda akiteta jambo na Waziri wa Fedha, Saada Mkuya
kwenye mkutano wa wabunge ambapo waziri wa fedha aliwasilisha
mapendekezo na mwelekeo wa bajeti ya serikali kwa mwaka fedha 2014/15,
Dar es Salaam jana. Picha na Salim Shao
Dar es Salaam. Serikali
imetoa mwelekeo wa Bajeti ya mwaka wa fedha wa 2014/15 kuwa ni Sh19.6
trilioni, ikilinganishwa na Sh18.2 za Bajeti iliyopita.
Vipaumbele
vya Bajeti hiyo ni kuendeleza Mpango wa Maendeleo wa Miaka Mitano
ulioanza mwaka 2011 na Mpango wa Matokeo Makubwa Sasa (BRN) ambao
unajumuisha maeneo sita ya kitaifa ya kilimo, elimu, maji, utafutaji wa
rasilimali fedha, nishati, uchukuzi na uboreshaji wa mazingira ya
kufanyia biashara.
Katika
kuhakikisha inakusanya fedha za kutosha, Serikali imeahidi kuunda kikosi
kazi cha kufuatilia mapato yote yanayotoka halmashauri zote nchini ili
kuondoa visingizio vilivyojitokeza wakati wa ufuatiliaji wa mapato.
Hayo
yalielezwa jana na Waziri wa Fedha, Saada Mkuya wakati akiwasilisha
mapendekezo ya Bajeti hiyo kwa kamati zote za Bunge, Dar es Salaam.
Alisema
matumizi ya kawaida kwa mwaka ujao wa fedha yanalenga kufanikisha mambo
20 muhimu, yakiwamo Uchaguzi wa Serikali za Mitaa mwaka 2014, Uchaguzi
Mkuu 2015, kukamilisha mchakato wa Katiba na nyongeza ya mishahara na
kulipa kwa wakati.
Mkuya alisema makadirio ya matumizi ya maendeleo ni Sh7.7 trilioni sawa na asilimia 39 ya matumizi yote ya Serikali.
Kati ya
fedha hizo, miradi ya maendeleo imetengewa Sh5.4 trilioni sawa na
asilimia 27 na matumizi mengine ya maendeleo ni Sh2.2 trilioni.
Utegemezi
Mkuya
alisema katika mwaka unaomalizika, Serikali ilipanga kukopa Dola 700
milioni za Marekani sawa na Sh1.1 trilioni na kati ya kiwango hicho,
iliambulia mkopo wa Dola 259 milioni hivyo kuweka nakisi ya Dola441.
Alisema
katika mwaka wa fedha 2014/2015, Serikali imekusudia kukopa Sh4.2
trilioni kutoka vyanzo vya mapato vya ndani na nje ili kuziba pengo la
mapato.
Misaada na pato la taifa
Katika
mwaka wa 2013/2014, Serikali ilipokea misaada ya Sh1.1 trilioni kutoka
kwa washirika wa maendeleo ikiwa ni asilimia 50 ya ahadi ya Sh2.3
trilioni, hivyo kuweka nakisi ya Bajeti ya Sh1.2 trilioni.
Akiwasilisha
Rasimu ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa mwaka 2014/2015, Waziri wa Nchi,
Ofisi ya Rais (Uhusiano na Uratibu), Stephen Wassira alisema deni la
Taifa limefikia Sh27.04 trilioni kutoka Sh24 trilioni na kufafanua kuwa
ongezeko la deni hilo limetokana na mikopo mipya ya kibiashara na ya
masharti nafuu.
Ukusanyaji mbovu wa mapato
Akizungumzia
ukusanyaji wa kodi, Waziri Mkuu, Mizengo Pinda alisema kumekuwa na
matatizo katika ukusanyaji wa mapato ya ndani, hasa yasiyotokana na
kodi.
“Tumepata
changamoto na tunajiuliza kwa nini hatufikii malengo, lakini tunaamini
kwamba tukijipanga vyema kwenye halmashauri zetu kwa kuzibana vyema,
tutaweza kupiga hatua nyingine kutoka hapa tulipo,” alisema. (CHANZO:MWANANCHI)(FS)
Post a Comment