Rais wa Zanzibar
na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein
amewatahadharisha watendaji wakuu wa Wizara na Idara za Serikali
kujiepusha na upendeleo wakati wakiendesha zoezi la kupitia Miundo ya
Utumishi ya wafanyakazi wa Umma(scheme of service).Tahadhari
hiyo ameitoa leo wakati alipokuwa akizungumza na wafanyakazi nchini
katika kilele cha maadhimisho ya siku ya wafanyakazi huko katika hoteli
ya Bwawani mjini Unguja.Amewataka
watendaji wanaohusika na zoezi hilo kulifanya kwa uadilifu na kwa
umakini mkubwa kwa kuwapanga watumishi kulingana na kiwango cha elimu,
taaluma na uzoefu walionao huku wakiainisha na kubainisha majukumu ya
kila mtumishi.Aliwaeleza
mamia ya watumishi wa umma waliohudhuria mkutano huo kuwa hivi sasa
Serikali imo katika mchakato wa kupitia Miundo ya Utumishi wa wafanyakzi
wa umma lengo likiwa ni kuhakikisha watumishi wanapata mishahara
stahiki kulingana na elimu, taaluma na uzoefu wa utumishi wao.Hata
hivyo alisisitiza kuwa asingependa kuona zoezi hilo linatawaliwa na
upendeleo ambapo mbali ya kuitia Serikali lawamani bali pia kuwavunja
moyo baadhi ya watumishi na hata kusababisha wengine kuondoka nchini.
Dk.
Shein aliwahakikishia watumishi wa umma kuwa Serikali ingependa kila
mara kuongeza maslahi yao kwa lengo la kuwapunguzia makali ya maisha
lakini dhamira hiyo inakwenda sambamba na kukua kwa uchumi ambako msingi
wake ni kwa watumishi hao kufanyakazi kwa kujituma na kuongeza tija
sehemu zao za kazi.
Alifafanua
kuwa tangu Serikali ya Awamu ya Saba iingie madarakani imekuwa
ikichukua hatua mbalimbali kuimarisha maslahi ya watumishi pamoja na
mazingira ya kazi ikiwemo kuongeza mishahara na marurupu mara mbili
mwaka 2010/2011 na mwaka 2013/2014.
Aliwataka
watumishi wa umma kujivunia mafanikio waliyoyapata na kufafanua kuwa
watumishi hivi ni tofauti na wakati wa ukoloni ambapo hivi sasa wanaweza
kumiliki nyumba za kisasa za kuishi na kwa wasiomiliki angalau wana
uwezo wa kupanga nyumba badala ya chumba kama ilivyokuwa wakati wa
ukoloni.
Hata
hivyo aliwataka wafanyakazi nchini kufanya kazi kwa bidii, ubunifu na
kuacha ubabaishaji kwani tafiti zinaonesha kuwa bado watumishi wengi
wakiwa kazini wanatumia muda mdogo kufanyakazi walizoajiriwa
Dk.
Shein alisisitiza ushirikiano wa UTATU kuwa ni suala muhimu
lisilokwepeka kwani ni lazima masula ya watumishi yajadiliwe na pande
zote husika kwa maslahi ya watumishi, waajiri na jamii kwa ujumla.
Kwa
hiyo alitoa wito kwa wizara na Idara za Serikali ambazo bado suala hilo
halijapewa kipaumbele kufanya hivyo na kueleza kuwa hakuna sababu kwa
kamati za uongozi za wizara kutoundwa au kwa zile zilizopo kutotimiza
wajibu wake.
Mhe
Rais aliueleza uongozi wa Shirikisho la Vyama Huru vya Wafanyakazi
–ZATUC kuwasiliana na Serikali mara kwa mara ikiwemo Ofisi yake kujadili
masuala mbalimbali pasi na kusubiri maadhimisho kama hayo kueleza
matatizo yao.
Kuhusu
suala la ajira Dk. Shein alisema lengo la serikali ni kupunguza ukosefu
wa ajira kutoka asilimia 17 hivi sasa hadi asilimia 11 ifikapo mwaka
2015 na kwamba hatua mbalimbali zinaendelea kuchukuliwa kufikia lengo
hilo.
Kwa
upande wake Kaimu Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Kazi na Utumishi wa Umma
ambaye pia ni Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Idara
Maalum Haji Omar Heri alitoa wito kwa uongozi wa ZATUC kushajiisha
watumishi kuanzisha matawi katika Wizara na Idara za Serikali ili
kuimarisha UTATU kwa faida ya pande zote.
Alisema
kuwa Wizara yake imekuwa na mahusiano mazuri na ZATUC hivyo ni wajibu
wa pande zote kuona kuwa mahusiano hayo yanaimarishwa kwa maslahi ya
Taifa.
Katika
risala yao iliyosomwa na Kaimu Katibu Mkuu wa ZATUC Maalim Mussa Omar
Tafurwa wafanyakazi hao waliiomba Serikali kuongeza kiwango cha chini
cha mshahara hadi shilingi 300,000.00 na kutaka kutekelezwa kwa Sheria
ya kuwepo kwa mkataba wa huduma kazini.
Risala
hiyo ilitaka pia kuangaliwa upya mabadiliko ya mishahara yaliyofanywa
hivi karibuni na Serikali kwa watumishi wenye uzoefu mkubwa kazini na
Serikali kuangalia suala la kuvunjwa sheria ya Kamati za Uongozi katika
Wizara na Taasisi za Serikali ambazo hutoa fursa kwa watumishi
kushiriki katika vikao hivyo na kutoa maoni yao.
Kwa
upande wake Mwenyekiti wa Taifa ZATUC Dk. Zahran Mohamed Nassor
aliitaka Serikali kutekeleza baadhi ya vipengele vya Sheria ya Mfuko wa
Hifadhi ya Jamii ambavyo Waziri husika kwa miaka 16 tangu kuundwa sheria
hiyo amezuia vipengele hivyo kutumika.
Post a Comment