Wabunge wa Chadema, Said Arfi na John Shibuda wamesema hawana hofu yoyote juu ya uamuzi utakaochukuliwa dhidi yao na uongozi wa chama hicho kwa kitendo chao cha kuhudhuria vikao vya Bunge Maalumu la Katiba.
Wakati Shibuda na Arfi wakieleza hayo, Mbunge wa
Viti Maalumu wa chama hicho, Leticia Nyerere ameibuka na kudai kuwa
hakuwahi kushiriki katika vikao vya Bunge hilo, ila alipita tu Dodoma
akielekea Kwimba, Mwanza.
Kwa nyakati tofauti wabunge hao ambao kurejea kwao
bungeni ni tofauti na msimamo wa Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) wa
kutoshiriki vikao vya Bunge la Katiba, wamesema Chadema hakina
demokrasia ya kweli kama kinavyojipambanua kwa wananchi.
Mwanasheria mkuu wa Chadema, Tundu Lissu kwa
nyakati tofauti amekaririwa akisema kuwa wabunge wote wa chama hicho
wanaokiuka msimamo wa Ukawa kwa kuingia katika Bunge la Katiba,
wajiandae kuongeza idadi ya ‘wabunge wa mahakama’.
Shibuda (Maswa Mashariki) alisema hana wasiwasi
wowote juu ya uamuzi utakaochukuliwa na chama chake, kusisitiza kuwa
iwapo atatimuliwa ndiyo atajua nini cha kufanya.
“Huwezi kuzungumzia kutibu kidonda wakati hujapata
jeraha. Ukishapata jeraha ndiyo utajua ulitibu vipi, ushonwe nyuzi au
uweke bandeji,” alisema Shibuda.
Shibuda ambaye ameshikilia msimamo wake wa
kuhudhuria vikao vya Bunge la Katiba kwa ajili ya kutetea masilahi ya
wakulima wa pamba na wafugaji, alisema uamuzi wa yeye kutafuta chama
kingine umetoka kwa wananchi wa jimbo lake.
“Wabunge wa Chadema walisusia vikao vya Bunge la
Katiba kukwepa matusi, sasa iweje leo wao wageuke vinara wa kuwatusi
wenzao. Kwa muda mrefu nimeitwa msaliti na pandikizi la CCM. Nimetukanwa
sana sasa nimechoka,” alisema Shibuda na kuongeza:
“Ukawa lazima wajidhihirishe kuwa wao ni kimbilio
la wananchi na si kutaka madaraka tu. Siwezi kuacha kuwawakilisha
wananchi wa Maswa kwa sababu ya Ukawa, hivi hao Ukawa wataleta mbegu
bora ya pamba kwa wananchi?”
Alisema mbunge akiwa bungeni hata kama itapatikana
Katiba ambayo haijatokana na maoni ya wananchi, sauti yake juu ya jambo
alilokuwa analitetea itasikika na hatahukumiwa kwa jambo lolote.
Akizungumza katika kipindi cha Jambo Tanzania
kinachorushwa na Televisheni ya Taifa (TBC1), Arfi (Mpanda Mjini)
alisema: “Sihofii kabisa ila nina hofu ya Mungu tu.
“Nashangaa wakati tunaanza harakati za kukijenga chama, tulikuwa tunawabeza CCM kwa kuendeshwa kibabe na kauli za ‘zidumu fikra za mwenyekiti’, lakini nashangaa sisi (Chadema) ndiyo tumeanza kuonyesha dalili za kutumikia kauli hizi.”
“Nashangaa wakati tunaanza harakati za kukijenga chama, tulikuwa tunawabeza CCM kwa kuendeshwa kibabe na kauli za ‘zidumu fikra za mwenyekiti’, lakini nashangaa sisi (Chadema) ndiyo tumeanza kuonyesha dalili za kutumikia kauli hizi.”
Akifafanua sababu za kurejea katika Bunge hilo,
Arfi alisema yeye ni mbunge wa wananchi na wamemtuma kuwakilisha kero na
changamoto zinazowatesa kwa miaka mingi.
“Kuna migogoro ya ardhi, maji hakuna, umeme shida pamoja na
mambo mengine mengi. Ni lazima turejee bungeni kuwasemea Watanzania,”
alisema.
Akizungumzia mgogoro wa Bunge hilo alisema mvutano
uliopo katika Sheria ya Mabadiliko ya Katiba, Kifungu cha(25), hakizuii
rasimu hiyo isibadilishwe.
Arfi alisema anashangazwa na wajumbe wa Ukawa
kulalamikia kifungu hicho wakati wao walikuwa ni sehemu ya kutunga
sheria hiyo katika Bunge la Jamhuri ya Muungano na kusisitiza kuwa
rasimu si msahafu inaweza kubadilishwa.
Hata hivyo, Arfi alibainisha wazi kuwapo kwa
makosa yaliyojitokeza katika maandalizi ya mchakato huo wa Katiba, huku
akitolea mfano kitendo cha wananchi kutoulizwa kwanza juu ya muundo wa
Serikali wanaoutaka kabla ya kuanza kwa mchakato wa kuandika Katiba.
Kwa upande wake, Leticia alisema: “Ni kweli
nilikwenda bungeni lakini sikushiriki kikao. Kwa sasa nipo wilayani
Kwimba. Nawashangaa wanaosema kuwa nimeshiriki vikao.”
Akizungumzia suala hilo, Katibu Mkuu wa Chadema Dk
Willbrod Slaa alisema chama hicho kitatoa ufafanuzi tamko juu ya
wabunge hao baadaye na kwamba hawezi kuzungumzia hoja ya mbunge
mmojammoja.
“Chadema sasa tunajikita kuzungumzia Katiba ya
nchi na kamwe siwezi kutoa kauli za kuwajibu wabunge wanaozungumza kwa
ajili ya kujifurahisha. Wao siyo muhimu kama Katiba ya nchi,” alisema.
Credit: Mwananchi
Credit: Mwananchi
Post a Comment