MKAZI wa Kijitonyama jijini Dar es Salaam, Robinson Mwakyusa (30),
amepandishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, kujibu mashitaka ya
kujifanya askari wa Kikosi cha Usalama barabarani na kukutwa na vifaa
vya Jeshi la Polisi.
Mwendesha mashtaka wa Serikali, Mwanaamina Kombakono, alimsomea
mshitakiwa mashtaka matatu mbele ya Hakimu, Devotha Kisoka na kusema
kuwa kabla Mwakyusa kuachishwa kazi alikuwa ni askari mwenye namba F
2460,
Katika kosa la Kwanza, Kambakono alidai kuwa Agosti 2, mwaka huu,
katika maeneo ya Chamazi Muhimbili, Wilaya ya Temeke, mshitakiwa
alijitambulisha isivyo halali kwamba ni mwajiriwa wa sekta ya
umma kitengo cha jeshi la polisi Tanzania na kwamba ni ofisa wa Kikosi
cha Usalama barabarani akiwa na cheo cha Stafu Sajini.
Alisema katika shitaka la pili, siku hiyo hiyo ya Agosti 2, katika
Kituo cha Polisi cha Mbagala, wilaya ya Temeke, mshtakiwa alikutwa na
sare za polisi wa kikosi cha usalama barabarani, simu ya upepo aina ya
Motorola GP 380 pamoja na beji iliyoandikwa ER Mwakyusa kinyume cha
sheria.
Ilidaiwa kuwa mshitakiwa alikutwa na vitu hivyo ambavyo ni mali ya
jeshi la polisi, vinavyosadikiwa kuibwa au kupatikana isivyo halali.
Katika shitaka la tatu, mshitakiwa anadaiwa kukutwa maeneo ya
Kijitonyama Mpakani B, wilaya ya Kinondoni, akiwa na nguo nne za kazi ya
polisi, ambazo ni suruali tatu na mashati ya trafiki, koti moja la mvua
la polisi, vikoti vinane vya trafiki vyenye mwanga, kofia ya trafiki ya
Uhuru, bareti na mikanda minne mali ya jeshi hilo, ambavyo vinasadikiwa
vimeibwa au kupatikana kwa njia isiyo halali.
Mshitakiwa alikana mashitaka hayo na mwendesha mashtaka alidai
upelelezi haujakamilika hali iliyomfanya hakimu Devotha kutoa masharti
ya dhamana ambapo ni mshitakiwa kutia saini saini bondi ya sh. milioni
50 na awe na wadhamini wawili ambao nao watatia saini bondi hiyo kila
mmoja.
Mshitakiwa alitimiza masharti ya dhamana na kuachiwa hadi Septemba mosi, mwaka huu, kesi itakapotajwa.
Post a Comment