WANANCHI wa
kada mbalimbali nchini, wamempa ‘big up’ na kumuunga mkono Mbunge wa
Kisesa kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Luhanga Mpina (pichani) kwa
kitendo chake cha kuomba Bunge la Jamhuri ya Muungano kusitisha mikutano
yake, ili fedha zinazolipwa kwa wabunge ziiwezeshe serikali kulipa deni
la shilingi bilioni 90 inazodaiwa na Bohari Kuu ya Madawa (MSD)
iliyogoma kutoa dawa kwa hospitali za umma.
Wakizungumza
kwa nyakati tofauti mara tu baada ya Mpina kutoa kauli hiyo Jumanne
wiki hii bungeni Dodoma, wananchi hao wamesema kitendo hicho ni cha
kishujaa na kimeonyesha uzalendo wa hali ya juu bila kujali itikadi za
kisiasa.
“Hii
ni aibu kwa serikali, inashindwa kulipa deni kwa muda mrefu hadi MSD
inashindwa kujiendesha, sasa wanapokataa kutoa dawa, maana yake ni
maumivu kwa wananchi wa hali ya chini, hasa wa vijijini. Bora wao wa
mijini wanaweza kwenda kununua kwenye maduka ya dawa. Serikali haijali
kwa sababu vigogo wake wanatibiwa nje kwa hiyo hawaoni umuhimu wa kulipa
deni hilo kwa sababu haliwagusi,” alisema Felix Duni aliyejitambulisha
kama mjasiriamali, mkazi wa Mbagala, Dar.
John
John, mwenyeji wa Nzega mkoani Tabora, alisema hakutegemea kama hoja
hiyo ingeweza kutolewa na mbunge wa CCM, kwani kufanya hivyo ni kama
kuivua nguo serikali yake, hivyo ujasiri wake unapaswa kuigwa, kwani
vikao vya bunge havina umuhimu kuliko afya za wananchi wanaowawakilisha.
“Wao
wamechaguliwa na wananchi, katika hali kama hii, lazima waungane kutetea
afya zao, serikali lazima itilie maanani suala hili, Bohari Kuu ya
Madawa inabebeshwa mzigo wa bure, kwa nini deni linakuwa kubwa kiasi
hiki wakati kila mwaka wizara ya afya inapewa pesa? Tunataka wabunge
kama hawa wenye kujali wananchi wao,” alisema John alipozungumza kwa
njia ya simu.
Gazeti
hili lilipokea simu pia kutoka kwa wananchi wa Mikoa ya Singida,
Mwanza, Morogoro na Dar es Salaam, ambao walitoa pongezi nyingi kwa
mbunge huyo na kumtaka Spika wa Bunge, Anne Makinda kulipa uzito jambo
hilo, vinginevyo, waishinikize serikali kulipa deni hilo.
Baada
ya mbunge huyo kutoa ombi hilo, Naibu Spika, Job Ndugai alimjibu kuwa
suala hilo litapelekwa kwa Kamati ya Uongozi wa Bunge ili kujadiliwa na
kwamba jibu lake litatolewa. Hadi gazeti hili linakwenda mtamboni, bado
jibu lilikuwa halijatolewa.
Bohari
Kuu ya Madawa ilisitisha kutoa huduma kwa baadhi ya hospitali za
serikali kutokana na deni kubwa ambalo halijalipwa kwa muda mrefu.
Hospitali ya Taifa ya Muhimbili peke yake, inadaiwa kiasi cha shilingi
bilioni tisa, kitendo kilichosababisha hospitali hiyo kubwa ya umma
kupandisha ada kwa wagonjwa wanaolala na vitanda, jambo ambalo
limelalamikiwa sana na wananchi.


Post a Comment