MGOMBEA Urais wa Chama Cha Demokrasia na Maendele (Chadema), Edward Lowassa, amesema akiingia madarakani, Serikali yake itawalipa posho wenyeviti wa Serikali za vijiji, wenyeviti wa mitaa na wenyeviti wa vitongoji kwa kuwa wanafanya kazi kubwa.
Lowassa
ambaye jana alifanya mikutano mitano ya kampeni Magugu, Dongobesh,
Bashinet na Haidom, aliyasema hayo akiwa kwenye mkutano wa kampeni
Makondeko, Kateshi, wilayani Hanang, Mkoa wa Manyara.
“Serikali
yangu ikiingia madarakani wenyeviti wa vijiji, vitongoji, mitaa
tutawalipa posho. Lazima tugawane keki ya nchi kwa sababu hawa wanafanya
kazi kubwa, lazima walipwe,” alisema Lowassa.
Lowassa
anayeungwa mkono na Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), alimpongeza
mwanasiasa mkongwe nchini, Kingunge Ngombale Mwiru kwa kukihama Chama
Cha Mapinduzi (CCM).
“Nampongeza Kingunge kwa kukubali mabadiliko,” alisema Lowassa.
Akiwa
kwenye mji mdogo wa Magugu, Lowassa alisema Serikali yake itajenga
hospitali mpya za kisasa zenye vifaa vyote na wataalamu.
Kuhusu
elimu alisema wapo watu wanaokejeli sera ya kutoa elimu bure kuanzia
shule za watoto wadogo mpaka chuo kikuu wakihoji atapata wapi fedha.
Kama nchi ina gesi, madini na inaweza kununua mashangingi haiwezi kushindwa kutoa elimu bure, alisema.
“Nagombea
ili nipambane na umasikini, ninaamini hakuna urithi utakaoweza kumpa
mtoto wako kama siyo elimu ndiyo maana nasema kipaumbele changu cha
kwanza ni elimu, cha pili ni elimu na cha tatu ni elimu,” alisema.
Baada
ya elimu, alisema atahakikisha anaboresha kilimo ikiwa ni pamoja na
kutafuta soko la uhakika kwa bidhaa za wakulima na kuwaruhusu kuuza
mazao yao popote penye soko.
Naye
Waziri Mkuu wa zamani, Fredrick Sumaye, akiwa Magugu, alisema kuna
njama chafu zinaendeshwa za kuwaeleza wananchi siku ya kupiga kura
watakuta jina la Ukawa na siyo vyama vinavyounda umoja huo.
Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) unaundwa na vyama vya NCCR-Mageuzi, Chadema, CUF na NLD.
“Kwenye
karatasi ya kura hamtakuta jina la Ukawa, mtakuta majina ya vyama, rais
mtampigia anatoka Chadema na wagombea wengine wako kwenye vyama
husika,” alisema Sumaye.
Aliwataka
wananchi hao kuhakikisha wanawahi kwenye vituo vya kupigia kura ili
wasikose fursa hiyo kutokana na njama za wapinzani wao wa siasa.
Post a Comment