MWENYEKITI wa Tume ya Taifa Uchaguzi nchini Jaji Mstaafu Damian Lubuva, ameeleza kushangazwa na kauli zinazotolewa na baadhi ya vyama vya siasa wakiwahamasisha wafuasi wao hasa kundi la vijana kubaki vituoni ili kulinda kura.
Kauli
hiyo ya Lubuva ambayo aliitoa Dar es Salaam jana wakati akizungumza na
waandishi wa habari inaonekana kumjibu Mwenyekiti wa Chama cha
Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Freeman Mbowe.
Akihutubia
mkutano wa kampeni jijini Dar es Salaam juzi katika viwanja wa Kawe,
Mbowe aliwataka wanachama na wafuasi wao kubaki vituoni siku ambayo
watapiga kura ili kuzilinda zisiibiwe.
Hata hivyo, Jaji Lubuva alisema kauli hiyo inajenga mazingira ya kuleta fujo nchini.
“Nashangazwa
na kauli hizo kwa sababu Tume tulishasema kwamba mfumo tulioandaa ni
mzuri na umeboreshwa kwa kuzingatia maoni yao… inakuwaje tena
wanaendelea kuwahamasisha wafuasi wao hasa vijana wabaki vituoni kulinda
kura kwanini… mawakala wapo kwa ajili gani,” alihoji.
Jaji
Lubuva alisema NEC inasisitiza watu watakaokuwa wamekwisha kupiga kura
kuondoka vituoni kwani endapo vijana watabaki kuna uwezekano wengine
wakapata hofu ya kwenda kupiga kura.
“Ndio
maana tunawataka waondoke lakini hawa wanasiasa wanaosema wabaki
kulinda kura huenda wana ajenda yao maana wasiwasi wa nini,” alihoji Jaji Lubuva.
Aliwataka
watazamaji wa uchaguzi wa ndani na nje ya nchi kuzingatia sheria,
kanuni na taratibu katika kipindi chote cha usimamizi bila kufungamana
na upande wa chama chochote cha siasa.
Aliwataka
wanawake nchini kuhimiza amani kipindi hiki cha uchaguzi kwani wana
nguvu kubwa ya ushawishi ambayo inaweza kuzuia vurugu zisitokee.
Awali
akizungumza wakati wa ufunguzi wa mada katika semina iliyowakutanisha
NEC na wawakilishi wa makundi mbalimbali ya wanawake nchini Kaimu
Mkurugenzi wa Sheria NEC, Emmanuel Kawishe, alisema NEC imejipanga
kusimamia vizuri Uchaguzi Mkuu kwa kuhakikisha unakuwa huru na haki.
“Tumeandaa
mfumo mbadala ujulikanao kama ‘Spreadsheet Excel RMS’ ambao utatumika
kuondoa makosa mbalimbali ya kibinadamu yatakayojitokeza katika zoezi la
ujumlishaji wa matokeo ya uchaguzi,” alisema.
Kawishe alisema mfumo huo utatumika iwapo kutakuwa na changamoto katika kutumia mfumo ulioandaliwa.
“Tume
imeandaa mfumo wa menejimenti ya matokeo (Result Management System)
ambao utatumika kuondoa makosa mbalimbali ya kibinadamu yanayoweza
kutokea kwa bahati mbaya katika ujumlishaji wa matokeo.
“Kasoro
au makosa hayo ni kama ujumlishaji wa kituo kimoja mara mbili, kukosea
uandikaji wa 7 badala ya 1, usahihi wa ujumlishaji na mengineyo, mfumo
huu si mgeni kwani ulitumika katika uchaguzi wa 2005 na 2010.
“Kwa
uchaguzi wa mwaka huu, tumefanya uboreshaji na kuondoa mapungufu katika
maeneo yote yaliyokuwa na changamoto 2010 na tumeandaa mfumo huu
mbadala ambao utatumika kama huu uliopo utakuwa na changamoto,” alisema.
Alisema
katika usimamizi wa zoezi la uchaguzi tume imepata changamoto ikiwamo
ya kufariki kwa baadhi ya wagombea pamoja na kuongezwa kwa mipaka ya
kiutawala ambayo imeanzishwa baada ya kutangazwa kwa majimbo mapya.
“Kuna
baadhi ya kata mpya zimeanzishwa ambazo ni Ifakara, Bariadi, Kishapu na
Bulyanhulu wakati Tume ikiwa tayari imetangaza majimbo, hivyo zipo
katika tishio la kutopiga kura lakini suala hilo linashughulikiwa,” alisema.
Post a Comment