Makongoro Oging’ na Haruni Sanchawa
CHACHA Makenge
38, (pichani), mgonjwa aliyetoa siri na malalamiko yake kwa Rais Dk.
John Magufuli ‘JPM’ kuhusu ukosefu wa mashine ya kutambua magonjwa
mbalimbali ya binadamu kwenye Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH)
yamemkuta makubwa baada ya watu wasiojulikana kuingia kwenye makazi yake
maeneo ya Chuo Kikuu cha Mlimani jijini Dar na kumwibia kila kitu.
Rais Dk. John Magufuli alipotembelea Hospitali ya Taifa, Muhimbili.
JIRANI AMJULISHA
Akizungumza na gazeti hili mwishoni mwa
wiki iliyopita akiwa bado wodini na ni siku moja baada ya Rais Magufuli
kutembelea Muhimbili, Makenge alisema siku hiyo kuna jirani yake
alikwenda kumjulia hali, akamwambia nguo zake, vyombo na nyaraka
mbalimbali vimeibwa na watu wasiojulikana.
Makenge aliongeza kuwa, taarifa za
kuibwa kwa vitu hivyo zilimsononesha sana hasa akizingatia kuwa, maisha
yake hayana adui na mtu na hajui aliyeiba ana lengo gani.
“Kule kwenye makazi yangu naishi peke
yangu, sina uadui na mtu. Nilipopatwa na matatizo ya kupigwa hadi
kuvunjwa mgongo na wanajeshi, nilipelekwa Hospitali ya Palestina, Sinza
(Dar) na hali yangu ilikuwa mbaya, nikakimbizwa hapa Muhimbili kwa
matibabu zaidi huku nikiambiwa kwenye makazi yangu kutakuwa salama,”
alisema Makenge.
ANA WASIWASI NA NANI?
Gazeti hili lilimuuliza Makenge kama ana wasiwasi na mtu yeyote ambapo alisema:
“Kama wasiwasi kibinadamu lazima uwepo.
Lakini simtaji mtu yeyote. Ila wasiwasi wangu mwingine ni usalama wa
maisha yangu. Nahofia sana nikirudi. Maana najiuliza je hao watu
wangenikuta wangeniacha kweli?
NYARAKA ZA NINI?
Alipoulizwa kuhusu nyaraka zilizoibwa
kama kuna kitu cha siri, alijibu: “Ni mambo yangu mwenyewe. Kila mtu ana
mambo yake ya siri ambayo hapendi mwingine ajue. Ila kwa mtu mwingine
hawezi kuambulia kitu kwenye nyaraka kwani, najua mwenyewe nilivyokuwa
naandika.”
ALIOMBA DAKIKA TANO KWA MAGUFULI
Makenge amekaa Muhimbili kwa miezi
miwili bila matibabu kutokana na mashine ya CT Scan na MRI kwenye
hospitali hiyo kuharibika na fedha kwa ajili ya vipimo katika hospitali
binafsi hana lakini Rais Magufuli alipotembelea hospitali hiyo kwa
kushtukiza Novemba 9, mwaka huu, mgonjwa huyo alimwomba dakika tano tu
ili atoe yake ya moyoni.
ALICHOMWAMBIA RAIS
Mgonjwa huyo alipopewa muda huo,
alimweleza rais kuhusu tatizo la kuharibika kwa mashine hizo na kumfanya
yeye kulazwa hapo kwa muda wa zaidi ya mwezi mmoja bila matumaini na
hakuwa na pesa za kwenda kupimwa na mashine za hospitali binafsi.
Ndipo Rais Magufuli alipouagiza uongozi
wa Muhimbili kuhakikisha kuwa Makenge anapata vipimo hata nje ya
hospitali hiyo na kutibiwa haraka, ikibidi atatoa mshahara wake utumike
kumtibu.
Pia Magufuli aliagiza ndani ya wiki
moja, na si zaidi ya wiki mbili, mashine za T Scan na MRI ziwe
zimetengenezwa. Hadi tunakwenda mitamboni mashine ya MRI ilikuwa
imeshaanza kufanya kazi baada ya matengenezo.
Kufuatia amri hiyo ya rais, Makenge
alisema siku iliyofuata alipelekwa Hospitali ya Besta iliyopo jijini
Dar na kupimwa na kipimo cha MRI.
“Nilifanyiwa vipimo Novemba 10, mwaka
huu, saa 4.13 asubuhi, alinipeleka muuguzi aitwaye Dora kwa kutumia gari
la kubebea wagonjwa. Novemba 11, mwaka huu nilirudishwa hapa Muhimbili.
“Nilichukuliwa vipimo vya damu saa 5.18,
baadaye akaja Dk. Antony, bingwa wa uti wa mgongo, kisha baadaye Dk.
Frank na wenzake wakaja wakasoma majibu ya kipimo cha damu na MRI.
“Waliniambia kipimo cha MRI kitarudiwa
na nitafanyiwa hapahapa Muhimbili, Jumanne ijayo (leo) kwani mashine
imeshatengenezwa,” alisema mgonjwa huyo ambaye hawezi kutembea.
TUJIKUMBUSHE KWA RAIS MAGUFUILI
Baada ya maelezo ya Makenge, Rais
Magufuli alizungumza na kiongozi mmoja wa hospitali hiyo ambapo naye
alikiri kuharibika kwa mashine hizo. Rais alionekana kushtuka na
kuumizwa na hali hiyo, akasema:
“Tatizo la hospitali za serikali
mnaharibu vifaa ili vikafanye kazi kwa watu binafsi, vifaa vya hospitali
za private (binafsi) zinafanya kazi lakini za hapa Muhimbili hazifanyi
kazi…! Na watu wanasafiri kwenda Ulaya… Mungu atawalipa.”
KUHUSU MAKENGE
“Mpelekeni huyu mgonjwa (Makenge)
akafanyiwe matibabu na mimi nitatoa hata mshahara wangu kumlipia,
haiwezekani akakaa mwezi mzima..! Na nitalifuatilia.”
GPL
Post a Comment