WANANCHI wilayani Bunda, mkoani Mara wamempongeza Mbunge wa Viti Maalumu
anayewakilisha kundi la vijana Mkoa wa Mara, Ester Bulaya (CCM) kwa msimamo wake
wa kuchangia hoja mbalimbali bungeni ikiwa ni pamoja na matatizo ya wananchi wa
Bunda.
Walitoa pongezi hizo juzi kwa nyakati tofauti mara baada ya kusikia taarifa
kwenye vyombo vya habari kuwa mbunge wa Jimbo la Bunda, Steven Wasira (CCM)
alimkoromea Bulaya kwa madai ya kuikosoa bajeti na hatua yake ya kuyazungumzia
masuala ya Bunda wakati yeye si mbunge wa jimbo hilo.
Nyamhanga Maswi, mkazi wa Tairo alisema Esther ni mbunge wa Mkoa wa Mara
ambaye anawakilisha wananchi hususan kundi la vijana ambalo ndilo linaathirika
zaidi ambao Wasira ameshindwa kuwasaidia kwa muda wote akiwa madarakani licha ya
kuwadanganya waunde vikundi ili wapate mikopo lakini hakuna alichowatimizia.
“Sisi wana Bunda tunampongeza sana huyu mbunge maana tangu amechaguliwa
amekuwa akichangia hoja nyingi zinazogusa maendeleo yetu na hii inaonyesha ni
jinsi gani anavyokerwa na maisha duni waliyonayo wananchi wa Mkoa wa Mara
tumeona juhudi zake hususan katika suala la wananchi wa Tairo ambao maeneo yao
yamechukuliwa na EPZ lakini hawajalipwa…’’ alisema.
Naye Boniface Noni wa mkazi wa Bunda alisema wananchi wana imani kubwa na
mbunge huyo (Bulaya) na kwamba yeye kama mbunge anao wajibu wa kuipinga bajeti
kama ameona haifai na wala haiwalengi wananchi anaowawakilisha hivyo alichofanya
ni sahihi na wala hapangiwi na mbunge mwingine kitu cha kuongea.
Naye Abubakari Kiharata wa Kijiji cha Maliwanda alieleza kusikitishwa na
kitendo cha Wasira kumwingilia mbunge huyo katika majukumu yake ya kikazi na
kudai kuwa hapaswi kuuliza wala kuzungumzia mambo ya Bunda kwa madai kuwa hilo
ni jimbo lake, jambo ambalo wananchi hao wamelipinga na kusema kuwa jimbo
analoliongoza Wasira ni mali ya wananchi yeye ameshindwa kuwaongoza awaachie
wenzake.
chanzo: Gazeti la Tanzania Daima 24/06/2012 |
Post a Comment