WABUNGE wa Chama cha Mapinduzi (CCM), wamedaiwa kulivuruga Bunge kwa kuibua
masuala yasiyo ya msingi wakati wa mijadala, kutokana na chama chao kukosa
mwelekeo.
Hatua hiyo imelalamikiwa kuwa inawanyima wananchi fursa ya kusikiliza hoja za
msingi zinazotolewa na wabunge makini wakati wa mijadala mbalimbali.
Maoni hayo yanakuja kufuatia mijadala ya Bunge hivi sasa kutawaliwa na
malumbano makali, vijembe, kejeli na matusi baina ya wabunge na hivyo kutumia
muda mwingi kuvutana pasipo kujadili matatizo ya wananchi.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti na Tanzania Daima jijini Dar es Salaam jana,
wananchi hao wa kada mbalimbali wakiwamo wasomi, wanasiasa na viongozi wa dini
walisema kuwa mfumo wa sasa wa Bunge haukidhi mahitaji ya wapiga kura badala
yake unaegemea kwenye maslahi binafsi ya vyama.
Mhadhiri mwandamizi mstaafu wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Dk. Azaveli
Lwaitama, alisema hiyo ni dalili ya CCM kukosa mwelekeo na kutaka kuwazuia
wananchi wasisikilize hoja za msingi kwa masilahi ya nchi.
“Wale wabunge wa CCM ndio nature (asili) yao, kwa sababu wanataka kupoteza
lengo ili watu wasi-pay attention (wasijikite) kwenye mambo serious (makini).
Huyu kijana Nchemba (Mwigulu) namfahamu alikuwa pale chuo kikuu.
“Najua anafanya hivyo kwa sababu hakutegemea amejikuta ghafla amekuwa mtu
mkubwa katika nchini, sasa hivi ni Mweka Hazina wa chama tawala, ana uwezo wa
kuongea na mkuu wa nchi wakati wowote ndiyo maana amelewa madaraka,” alisema
Lwaitama.
Alisema kuwa zamani ili mtu awe kiongozi alikuwa anafundwa kimaadili ya
chama, kwamba hata Rais Jakaya Kikwete mwenyewe alitengenezwa ndani ya CCM.
“Mbaya zaidi, wanakuwa viongozi kwenye chama alichokiasisi Julius Nyerere
lakini wao hawana uhusiano naye, wanaongea upuuzi ndani ya Bunge halafu serikali
yao inasema CHADEMA inaongoza mgomo wakati hali halisi inaonyesha wazi kwamba
lazima mtu agome.
“Hahihitaji akili kubwa kujua vyanzo vya migomo, nenda hospitali utaona
sababu za migomo, hali ni mbaya huko… badala ya kutengeneza mazingira bora
wanakimbilia kuanzisha mikoa, huu ni upuuzi,” alisema Dk. Lwaitama na kumtaka
Rais Kikwete kuacha kuwakurupua watu na kuwapa madaraka.
Mhadhiri Msaidizi mwingine wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Bashiru Alli,
alisema kuwa anashangazwa na vikao vya Bunge kutawaliwa na mizaha isiyo na
utekelezaji wa mambo ya msingi.
“Mambo mengi yanayohitaji ufumbuzi kupitia mijadala ya wabunge hayazungumzwi
kutokana na vitendo vyao vya mzaha vinavyoendelea bungeni na hivyo kero za
wananchi hazipatiwi ufumbuzi,” alisema.
Kwa upande wake Katibu Mkuu wa Chama cha NCCR Mageuzi, Sam Ruhuza, alisema
kutokana na wabunge hao kushindwa kabisa kujielekeza kwenye kujadili changamoto
zilizopo na kuishia kwenye ushabiki wa vyama, iko haja ya kufanyiwa upya semina
ya kukumbushwa wajibu wao.
Ruhusa alisema kuwa inashangaza kuona majimbo yao yanakabiliwa na kero
mbalimbali lakini wabunge wanapoteza muda mwingi kujadili masuala binafsi
yanayohitimishwa na kauli za kuudhi na hata wabunge wengine kutolewa nje.
Naye Mchungaji wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri (KKKT) Usharika wa Matumbi,
Christophile Kalata, alieleza kuwa Watanzania walipofika sasa wanahitaji
viongozi shupavu wanaoweza kusimamia rasilimali na maendeleo ya nchi kwa
masilahi yao.
“Nchi zilizoendelea zinapenda kuona au kushuhudia Tanzania ikikumbwa na
misukosuko, hivyo zinaweza kutumia mwanya huo kwa kuwatumia viongozi waliopo
kulumbana ili kazi za maendeleo ya nchi zisimame,” alisema Kalata.
chanzo: Tanzania Daima
|
Post a Comment