Serikali imekubaliana na Waislamu kuanzishwa kwa
Mahakama ya Kadhi itakayokuwa nje ya Mfumo wa Serikali na itagharimiwa na
kuendeshwa na waumini wa dini hiyo wenyewe.
Kwa kuanzia mahakama hizo zitakuwepo katika maeneo
machache kwa lengo la kuufanya umma kuielewa vizuri tofauti na hisia potofu
zilizokuwepo kuwa zitahusisha makosa ya jinai kwa mujibu wa sheria za
Kiislamu.
Waziri Mkuu Mizengo Pinda alitoa msimamo huo wa
Serikali uliokubaliana na Waislamu jana wakati akijibu hoja mbalimbali za
wabunge wakati wa kuipitisha bajeti ya ofisi yake.
“Napenda kulijulisha Bunge lako Tukufu kwamba,
Kamati Kuu inayojumuisha Viongozi wa Waumini wa Dini ya Kiislamu na Serikali
chini ya Uenyekiti wangu, kimsingi imekubaliana kwa kauli moja Uanzishwaji wa
Mahakama hiyo Nchini itakayokuwa nje ya Mfumo wa
Serikali.
“Mahakama hiyo itagharamiwa na kuendeshwa na
Waumini wa Dini ya Kiislamu wenyewe. Serikali kwa upande wake hususan katika
hatua hizi za awali za kuanzishwa kwa Mahakama hii itaendelea kushirikiana kwa
karibu ili kuhakikisha kuwa azma hii inafanikiwa,” alisema
Pinda.
Pinda alikuwa akijibu hoja za wabunge waliotaka
kufahamu maendeleo ya Mahakama hiyo huku wakitaka Serikali itimize ahadi yake
hiyo ambayo ipo katika Ilani ya Uchaguzi ya CCM. Wabunge hao na majimbo yao
kwenye mabano ni Hamad Rashid Mohammed (Wawi); Rashid Ali Abdallah (Tumbe);
Ahmed Juma Ngwali (Ziwani) na Hussein Nassor Amar ( Nyang’hwale).
Pinda alisema; “Katika kikao cha mwisho cha pamoja
kati ya Serikali na ujumbe wa Wawakilishi wa Waumini wa Kiislamu kilichofanyika
Machi mwaka huu, tumekubaliana katika kuwezesha suala hilo liende kwa haraka,
kwa kuanzia, ni vyema zikaanzishwa Mahakama za Kadhi katika baadhi ya maeneo
machache nchini. Lengo ni kuwezesha umma kulielewa vizuri suala hili kinyume na
hisia potofu zilizopo sasa zikihusisha Mahakama ya Kadhi na Sharia (inayohusisha
masuala ya jinai) chini ya Dini ya Kiislamu”.
Pinda alitaja masuala yatakayoshughulikiwa katika
Mahakama hiyo kuwa ni pamoja na Ndoa na Talaka, Mirathi, Wosia,
Hiba/Zawadi/Tunu, Wakfu; Malezi ya Watoto na Usuluhishi wa Migogoro ya Kiislamu.
Mahakama hiyo haitahusika na Mashauri ya Jinai.
Alisema katika kikao cha mwisho cha Kamati Kuu
inayosimamia suala hilo iliamuliwa na pande zote kuwa baadhi ya wajumbe kutoka
upande Waislamu na Serikali wakafanye ziara ya mafunzo katika nchi za India,
Uingereza, Kenya na baadaye Zanzibar ili wakajifunze namna ya kuratibu na
kuendesha Mahakama za Kadhi katika nchi hizo ambazo zina Mahakama za Kadhi kwa
muda mrefu.
“Lengo ni kupata uzoefu na kujua njia bora ya
kutuwezesha kuanzisha Mahakama hiyo nchini. Ziara hiyo inatarajiwa kufanyika
hivi karibuni na kugharimiwa na Serikali,” alisema.
Akizungumzia chenji ya Rada, alisisitiza kuwa
itatumika kama ilivyokusudiwa kwani Tanzania na Uingereza zilikubaliana
asilimia 75 ya fedha hizo kwa ajili ya kununulia vitabu vya kiada, viongozi vya
walimu, mihtasari na miongozo ya mihtasari na asilimia 25 ya fedha hizo
kununulia madawati.
Kwa sasa kitabu kimoja kinatumiwa na wanafunzi 10,
lakini baada ya kununuliwa kwa vitabu hivyo wanafunzi kati ya wawili na watatu
wa shule za msingi watatumia kitabu kimoja.
Alisema vitabu hivyo vitanunuliwa kutoka katika
kampuni 13 na kati yake kampuni mbili ndio za nje, lakini zina matawi nchini.
Kampuni hizo ni Ben; Best Deal Publisher; E & D Vision; Education Books
Publisher; Jadida; LongHorn; Longman; Macmillan; Mkuki na Nyota; Mture; Oxford;
Tanzania Institute of Education (TIE) na Ujuzi Book.
Alisema fedha hizo za madawati Sh bilioni 18.1
zitaweza kununua madawati 400,000 kwa ajili ya wanafunzi milioni 1.2. Kwa sasa
wanafunzi wenye uhaba wa madawati ni 8,000,000.
Alisema ununuzi wa rada ulifanywa na Wizara ya
Miundombinu ambayo sio Muungano hivyo Zanzibar haitapata mgawo
huo.
Akizungumzia juu ya uvunjwaji wa Jiji la Dar es
Salaam lililoanzishwa mwaka 1999, Pinda alisema mapendekezo ya kulivunja jiji
hilo na kubakishwa manispaa zake tatu ili ziratibiwe na sekretarieti ya Mkoa wa
Dar es Salaam yalitolewa Novemba mwaka 2010, lakini baada ya kuonekana lina
kasoro tangazo hilo lilibatilishwa Februari mwaka
huu.
“Kutokana na Tangazo la Serikali la Juni 15 mwaka
huu, kwa sasa, kisheria Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam, bado ina hadhi
kamili ya Mamlaka ya Serikali za Mitaa. Aidha, halmashauri hiyo ina nguvu ya
kisheria kutekeleza majukumu yake kwa mujibu wa Sheria,”
alisema.
Kuhusu zaidi ya Sh bilioni 300 zilizowekwa na
Watanzania sita katika benki ya Uswisi zilizotokana na gesi ya nchini, alisema;
“Serikali kupitia vyombo vyake vya Takukuru, Financial Intelligency Unit (FIU)
wameanza kufanya uchunguzi wa taarifa hizo kwa kuzingatia taratibu za kisheria.
Uchunguzi huo utakapokamilika matokeo yake yatatangazwa,”
alisema.
chanzo: Ziro99 Blog
Post a Comment