Featured
    KWA HABARI NA MATANGAZO EMAIL : pbuyegu2@gmail.com ... Get a superior results by advertising with us by E- Mail us pbuyegu2@gmail.com We will bring Your Business to Light

    Featured Posts

Loading...

Huyu ndiye Shaaban Robert, gwiji wa Mashairi



DUNIA inayoongea lugha ya Kiswahili haitausahau mchango mkubwa uliotolewa na Shaaban Robert katika kuikuza.
Kwa muhtasari tuangalie maisha ya gwiji huyu wa Kiswahili japo alikuwa na elimu ndogo ya darasani, lakini bado anasifika na kutukuzwa kila mahali kutokana na umahiri wake katika kukuza lugha hiyo.

Maisha yake
Shaaban Robert alizaliwa Januari mosi, 1909 Kijiji cha Vibambani, jirani na Machui, kilomita 10 kusini mwa mji wa Tanga, alipata elimu yake katika Shule ya Msimbazi, jijini Dar es Salaam kati ya mwaka 1922 na 1926, alifaulu na kupata cheti.
Alikuwa mshairi na mwandishi wa riwaya. Mchango wake katika lugha ya Kiswahili ni mkubwa, kwani kazi zake zinaheshimika katika fasihi ya Kiswahili na zinatumika mashuleni. Alifariki dunia Juni 22, 1962.
Aliajiriwa na serikali ya kikoloni akawa karani katika Idara ya Forodha huko Pangani mwaka 1926 – 1944. Bila shaka kukaa kwake miaka mingi hivi katika mji wa kihistoria uliokuwa mahali pa utamaduni wa Kiswahili tena mahali patulivu, kumesaidia maendeleo yake Shaaban kama mwandishi wa Kiswahili.
Tangu mwaka 1944 alihamia ofisi nyingine ya Hifadhi ya Wanyama, baadaye Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Tanga.
Mbali na maandiko yake, alikuwa na athari kubwa katika maendeleo ya lugha ya Kiswahili akiwa mjumbe wa kamati za East Africa Swahili Committee, East Africa Literature Bureau na Tanganyika Languages Board.
Kwa ujumla Shaaban Robert aliandika vitabu ishirini na viwili. Baadhi ya vitabu hivi ni Adili na Nduguze, Kusadikika, Kufikirika, Wasifu wa Siti Binti Saad, Baada ya Miaka Hamsini, na Maisha Yangu. Vitabu vyake vimetafsiriwa katika lugha za Kichina, Kiingereza na Kirusi. Alifariki dunia Juni 22, 1962 na kuzikwa Machui. Aliacha wake watatu na watoto kumi.

Familia na elimu
Wazazi wake wote wawili walikuwa wa ukoo wa Mganga wa kabila la Kiyao. Hatujui sana habari za wazazi wake, lakini twajua kwamba jina la baba yake halikuwa Robert.
Jina hili ama linatokana na matamshi mabaya ya jina lake hasa au yawezekana kuwa ni jina alilopewa alipokuwa Shule ya Msimbazi. Kwa muda mfupi yeye mwenyewe aliandika jina lake ‘Roberts’, lakini baadaye aliacha kuliandika hivyo.
Alizaliwa Vibambani, ambacho ni kijiji kilichopo kusini mwa Machui, umbali wa maili sita kusini mwa mji wa Tanga, Januari mosi mwaka 1909. Hakujiita Myao hasa, bali alikuwa mmoja wa wachache ambao daima walijiita Waswahili.
Alisoma jijini Dar es Salaam tangu mwaka 1922 hadi mwaka 1926, akawa mtu wa pili katika wanafunzi kumi na mmoja waliofaulu mitihani yao na kupewa cheti, yaani ‘School Leaving Certificate’.
Alioa mara tatu: mke wa kwanza alikuwa Mdigo. Alikuwa na watoto kumi. Alipofariki dunia aliacha watoto watano.

Kazi alizofanya alipokuwa karani wa serikali
Akiwa serikalini alifanya kazi forodhani Pangani na mahali pengine tangu mwaka 1926 hadi 1944;
Idara ya Wanyama tangu mwaka 1944 hadi 1946; na Ofisi ya Mkuu wa Jimbo la Tanga tangu mwaka 1946 hadi 1952.
Sehemu zingine ni Ofisi ya Kupima Nchi Tanga, tangu mwaka 1952 hadi 1960.
Alipandishwa cheo kuwa Grade III Higher Division mwaka 1929, na mwaka 1944 alipandishwa tena kuwa Grade II Local Service. Alikuwa mwanachama wa East African Swahili Committee, East African Literature Bureau, Tanganyika Languages, Tanga Township Authority.

Kifo na kumbukumbu
Marehemu Shaaban Robert alifariki Tanga Juni 22, 1962, alizikwa Machui, Tanga. Alituzwa zawadi ya waandishi inayojulikana kama ‘Margaret Wrong Memorial Prize’na nishani ya M.B.E.

Vitabu vyake
Maisha yangu, Kusadikika nchi iliyo angani, Kufikirika, Adili na nduguze, Masomo yenye adili, Utenzi wa Vita vya Uhuru, Wasifu wa Siti Binti Saad na Baada ya Miaka Hamsini.

chanzo: Gazeti Tanzania Daima
Download Our App

1 comments:

Halfani Sudy MOD

Ahsante kaka

Reply

Post a Comment

CodeNirvana

BLOG RAFIKI

© Copyright EMMANUEL SHILATU - BREAKING NEWS BLOG
Back To Top