***************************************
Na
Mwandishi Wetu
KIJANA Julius Dawson ambaye kwa jina la kisanii
anajulikana kama 'Elinaja' (23), mkazi wa Tabata Segerea, ambaye mwaka
jana alikuwa gumzo baada ya kuandika
mashahiri ya muziki wa Bongo Flava "mistari ya Bongofleva" katika karatasi yake
ya kujibia mtihani wa kidato cha nne,
amefunguka na kuweka wazi kile kilichomfanya kufanya tukio hilo la kihistoria
katika tukio hilo lililoonekana kituko
cha mwaka.
Dawson, ambaye asili yake ni mzaliwa wa Moshi Marangu,
ambaye kwa sasa anaishi peke yake Tabata baada ya baba yake kufariki huku mama yake akiwa anaishi Wilaya ya
Kisarawe, alisema lengo la kufanya vile ilikuwa ni kufikisha ujumbe
kwa jamii ili kuokoa maisha ya vijana
wengi ambao hupotezwa muda kwa kulazimishwa kusoma bila kujali kile anachohitaji
kujana kutokana na mfumo uliopo sasa
ambao unamlazimisha kila kijana kuufuata bila ya kuwepo na mfumo
mbadala.
Akizungumza kwa kujiamini wakati akiwa katika
mahojiano na mtangazaji wa kipindi cha "Power Breakfast" cha Radio
Clouds FM, Gerald Hando, Dawson, alisema
kuwa mfumo mmoja wa maisha unawaharibia maisha vijana wengi ambao hawawezi
kufiti katika mfumo huo, ambao pengine
wangeweza kufanikiwa kama kungekuwa na mifumo mbadala kwa kuchagua wakipendacho
kusomea.
"Waulize watu hawa wanaotamba katika muziki au umiss,
utakuta wazazi wao walikuwa wanawakimbiza sana "huyu hataki shule", lakini akishafanikiwa utamsikia mzazi huyo huyo
akisema "Mungu kamjaalia mwanangu kafanikiwa katika muziki". Sasa
kama mzazi angemsapoti kwa kutambua
kipaji chake tangu mapema si angefanikiwa zaidi kuliko kumpotezea muda wake?"
Alisema na kuhoji
Dawson.
"Tatizo la nchi yetu ni kwamba kuna 'system' moja
iliyowekwa, kwamba usipoifuata huna 'option' nyingine. Wakati
naandika vile nilikuwa na lengo la kutuma
na kufikkisha ujumbe kwa wahusika wanaosimamia elimu kwamba kuna umuhimu wa
kuwekwa 'system' tofauti za maisha kwa
sababu mtu anaweza akawa si mzuri katika 'system' yao lakini akawa mzuri katika
'system' nyingine. Hivyo ziwepo ili
wazazi waokoe pesa na muda wa kulazimisha kumpeleka mtu katika kitu
asichokipenda na ambacho anakimudu.
"Ujumbe wangu ni kwamba wazazi na jamii itambue vipaji
vya vijana wao. Inapotokea mtoto tangu akiwa mdogo na akaonekana kuwa na kipaji cha kuimba ama kuigiza ama fani yeyote
basi ni vyema akasomea kitu ambacho kipo ndani yake ya damu yake kuliko kupoteza muda na pesa
bure.
Mimi ni mmoja kati ya watu walioathirika na maisha
magumu nikiwa mitaani kwa sababu tu tumeshindwa kwenda na 'system' niliyokuwa nikiihitaji. Unakuta vijana wana vipaji
vingine ambavyo vingeweza kuwafanya wakaishi maisha bora kabisa,
lakini mzazi analazimisha kufuata
anachokihitaji yeye.
"Nilipoandika jambo sikuamini kama lingekuwa kama
lilivyokuwa na kuteka hisia za kila mtu ila nilikuwa na maana yangu
kubwa ya kufikisha ujumbe. Lakini
lilivyopokewa ilikuwa tofauti. Watu walikuwa wakiangalia upande mmoja tu. Na
ilikuwa inaniumiza sana. Kuna wakati
nilikuwa nikipanda katika daladala, na kukuta watu wakiongelea jambo lile bila
kujua mlengwa wanayemzungumzia wapo naye
katika gari hilo, huku wengine wakiponda sana. Bila wao kujua na mimi nilikuwa
nikijumuika nao katika kuchangia mawazo
huku mimi nikishikilia na kusimamia msimamo wangu kwa kuwaeleza kama ambavyo
nimeeleza hapa leo, nilikuwa nawaeleza
kama haya ninayosasema hapa."
Alipoulizwa na Gerald Hando, kuwa anajisikiaje kupata
fursa ya kutoa ufafanuzi wa jambo hilo hewani, Dawson alisema: "Katika siku ninayojisikia furaha maishani mwangu, ni
leo. Najiona kama mtu ambaye nimeutua mzigo mzito uliokuwa ukimuelemea. Baada ya hapa hata nikiambiwa kufa, ni
sawa tu kwa sababu nimeshautua mzigo."
Dawson pia alitumia fursa hiyo kuomba radhi kwa Jamii
kama kuna aliyekwazika ama kumkatisha tamaa yeyote kutokana na kitendo chake kile hicho.
"Maoni yangu ni kwamba jamii iwasapoti watu kufanya
kitu wanachokiweza. Mwisho kama kuna mtu ama mzazi nilimkwaza ama nilimkatisha tamaa, namuomba radhi. Mimi si 'bad boy',
mimi ni kijana mwema kabisa. kwani hata ningejaza majibu ambayo nahisi nisingeyapatia kwa usahihi bado kwangu
yasingekuwa na faida" alisema
Akielezea historia yake na kilichosababisha kuchelewa
kumaliza kidato cha nne akiwa na umri mkubwa, Dawson alisema masomo yalikuwa yakimuwia magumu na hivyo kumfanya arudie
kidato cha pili kila alipofeli kwa miaka miwili mfululizo na
hatimaye kukaa benchi kwa miaka
minne.
"Nilianza shule ya msingi Umoja Mabibo mwaka 1996,
lakini maisha yalikuwa magumu hapa mjini hivyo tukiwa na wazazi tukahamia Kisarawe.
"Mwaka 2002 nikachaguliwa kujiunga na Sekondari
Manerumango. Wakati nikiwa kidato cha pili nikafeli mara mbili. Mara
ya kwanza nilirudia, lakini mara ya pili
nikaacha shule.
"Baadaye mama yangu mdogo akanichukua nikaja huku Dar
kusoma. Nikarudia tena shule baada ya kukaa nje ya masomo kwa miaka minne.
"Shule nilikuwa naipenda, lakini yenyewe haikuwa
ikinipenda kwani aina ya elimu niliyokuwa naipata naona ilikuwa
ngumu kwangu. Nilikuwa nachukua masomo ya
biashara. Nadhani ugumu niliuona kutokana na jinsi nilivyoumbwa tu. Nilikuwa
nasukumwa pia na mama yangu mkubwa. Maksi
zangu zilikuwa za chini sana. Mwisho ndio nikamaliza kidato cha nne mwaka jana
nikiwa na umri mkubwa kama
hivi."
Alisema baada ya kufikisha ujumbe, sasa anajisikia
huru licha ya kwamba hana kazi ya kufanya ya kumuingizia kipato,
zaidi ya kujishughulisha na usanii wa
kutunga na kuimba muziki wa Bongo Flava.
"Nimefanikiwa kurekodi wimbo wangu mmoja unaitwa "Mr
President" ambao unaongelea upande wa rais anayetolea majibu
maswali ya wananchi na huku pia akielezea
ugumu wa kazi yake.
"Nimeurekodi katika studio ya prodyuza mzungu Fundi
Samweli wa Kibaha na kisanii natumia jina la "Elinaja". Katika sehemu ya mistari yake, Dawson anaimba:
"Mnasema Mr President kila mahala kajaza rafiki zake, ni nani kati
yetu anashirikiana na maadui
zake."
Na kiitikio kinasema: "Wanagomba wanasumbua kila
tatizo nasemwa mimi, mara "Mjomba" mara "Mshua" oooh Mr President."
Jina la Mjomba lilitumika katika nyimbo
za Mrisho Mpoto wakati neno "Mshua" lilitajwa katika wimbo 'Rizi-One' wa rapa
Izzo Bizness.
Dawson a.k.a Elinaja, alisema amerekodi wimbo huo kwa
fedha za kuunga-unga kutoka kwa ndugu, jamaa na marafiki."Nina nyimbo za kutosha albam nzima. Tatizo ni pesa.
Naomba jamii inisaidie kufanikisha ndoto yangu," alisema kijana
huyo ambaye aliwafanya waandishi wa
habari waangue vicheko mwaka jana wakati Mkurugenzi Mtendaji wa Baraza la
Mitihani, Joyce Ndalichako, alipoisoma
"mistari" yake ya Bongofleva, wakati akitangaza matokeo ya kidato cha nne mwaka
jana.
Baada ya mahojiano ya Dawson na Hando, watu mbalimbali
walituma ujumbe radioni Clouds FM kuonyesha sapoti yao kwa kijana huyo akiwamo Salum Mwalimu wa Vodacom na Jackson Mbado
wa Airtel, huku Salum Mwalimu akimuita kuwa ni shujaa wake.
chanzo: Sufiani Mafoto
Post a Comment