Na Mahmoud
Zubeiry
KOCHA mpya wa Yanga, Thom
Saintfiet amesema kwamba sera yake ni ushindi na mataji na hahofii mpinzani
yeyote katika soka ya Tanzania, ikiwemo watani wao wa jadi, Simba
SC.
Akizungumza katika Mkutano na
Waandishi wa Habari jioni ya leo, makao makuu ya klabu makutano ya Mitaa ya
Twiga na Jangwani, Dar es Salaam, Saintfiet alisema kwamba yeye ni muumini wa
ushindi na mataji, hivyo anachotaka ni ushindi tu.
“Nikishinda 5-0 ni vizuri,
lakini hata nikishinda 1-0 si mbaya, mimi ni mshindi na ndio maana nimekuja hapa
kushinda,”alisema.
Thom alisema kwamba akili yake
hapo kwa Simba tu, bali wapinzani wote katika Ligi Kuu na akasema anataka
kurejesha ubingwa wa Ligi Kuu, ambao msimu uliopita klabu hiyo ilipokonywa na
watani wao hao wa jadi.
“Upinzani ni mkubwa,
nasikitika mwaka jana timu imepoteza ubingwa wa Ligi Kuu, lakini si mbaya, si
lazima timu bora kila mwaka iwe na taji. Hata Barcelona ni timu nzuri, lakini
haikuchukua ubingwa wa Ligi ya Mabingwa wala La Liga.
Timu (Yanga) ilibeba nafasi ya
tatu msimu uliopita, siyo nzuri sana. Nataka nishirikiane na wenzangu kurejesha
heshima,”alisema.
Saintfiet alisema kwamba
ameona wachezaji ni wazuri na anamuamini kocha anayemkuta Freddy Felix Minziro
ni mzuri na amefanya kazi nzuri. “Timu ilicheza mechi na Express wiki iliyopita,
nimeambiwa ilicheza soka nzuri na kushinda, naamini naikuta timu ikiwa
vizuri,”alisema.
Mbelgiji huyo alisema kwamba
ana wiki moja kabla ya kuanza kwa Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati, Kombe
la Kagame na hana wasiwasi atafanya vizuri kwa sababu timu ina wachezaji wazuri
na Minziro alianza kuwaandaa mapema.
Saintfiet alikataa kuzungumzia
falsafa yake akisema hataki wapinzani wake wajue siri zake, ila akasistiza sera
yake ni ushindi na kubeba mataji.
Tom
Saintfiet alizaliwa Machi 29, mwaka 1973 mjini Mol, Ubelgiji na kabla ya kuwa
kocha alicheza soka katika nafasi ya kiungo kuanzia mwaka 1983 hadi 1997
alipostaafu na kuwa kocha akiwa ana umri wa miaka 24, akiweka rekodi ya kocha
kijana zaidi kuwahi kutokea katika soka ya Ubelgiji.
Saintfiet amefundisha nchi
kadhaa kuanzia kwao Ubelgiji, Qatar, Ujerumani, Visiwa vya Faroe, Finland na
Uholanzi.
Pia
ana uzoefu wa kutosha wa kufundisha soka Afrika akiwa amefundisha Namibia na
Zimbabwe kama kocha Mkuu wa timu za taifa za nchi hizo.
Anasema kabla hajakwenda
Namibia, Saintfiet alikuwa kocha wa klabu ya Ligi Kuu Finland, iitwayo RoPS
Rovaniemi na mwaka 2002, alikwenda kuifundisha B71 Visiwa vya Faroe ambayo
aliiwezesha kushika nafasi ya pili katika Ligi Daraja la kwanza. Anasema kutoka
hapo, akaenda kuwa kocha wa Al-Ittihad Sports Club ya Qatar (sasa inaitwa
Al-Gharafa SC) ambako alidumu hadi mwaka 2004 alipochukuliwa kuwa kocha wa timu
ya taifa ya vijana chini ya umri wa miaka 17 ya Qatar.
Saintfiet ana leseni
Shirikisho la Soka Ulaya (UEFA) ya kufundisha soka ya kulipwa popote barani
humo, ambayo aliipata mwaka 2000.
Kati ya mwaka 2006 na 2007
alikuwa Mkurugenzi wa Ufundi wa FC Emmen ya Daraja la Kwanza Uholanzi na pia
amewahi kufanya kazi kama Mshauri wa Ufundi wa Shirikisho la Soka la
Kazakhstan.
Amewahi kuwa Mchambuzi wa
soka katika Televisheni katika nchi za Ubelgiji, Afrika Kusini na Namibia na
alifanya kazi kama mkalimani DFB. Amesomea Saikolojia ya Michezo na
Uchumi.
Anazungumza lugha kibao na kwa
ufasaha zaidi ni Kiholanzi, Kiingereza, Kifaransa, Kijerumani, Kifaroe na ‘ana
jua jua’ Kiarabu, Kiafrikana na Kispanyola na sasa tayari ameanza kujifunza
Kiswahili.
Baada ya kumaliza kusaini
mkataba majira ya 9:47 jioni, Saintfiet aliyewasili jana mchana nchini,
aliteremka Uwanja wa Kaunda kuanza kufundisha timu. Kwanza alianza kuzungumza na
wachezaji kuwaelezea falsafa zake na kisha akaanza kazi.
Post a Comment