
Mkurugenzi
wa Lino International Agency (kushoto) akizungumza na Waandishi wa Habari
katika ukumbi wa Idara ya Habari (MAELEZO) asubuhi hii, kutaja tarehe ya
kufanyika shindano la Miss Tanzania 2012, ambayo ni Novemba 3, mwaka huu katika
ukumbi wa Blue Pearl Hotel, Ubungo Plazza, Dar es Salaam. Kushoto ni Miss Tanzania
2011, Salha Israel. Lunedenga amesema washiriki wote wa Miss Tanzania wataingia
kambini Oktoba 2 katika hoteli ya Girraffe, iliyopo Mbezi, Dar es Salaam ambako
watakaa kwa mwezi mmoja kuelekea shindano hilo, wakinolewa na walimu waliobobea,
akiwemo Salha.
Mratibu huyo
alisema kuwa mashindano ya mwaka huu yanaonekana kuwa na ushindani zaidi
kutokana na kanda mbalimbali kutoa warembo wenye vigezo vinavyokaribiana jambo
lililowapa majaji wakati mgumu wa kufanya maamuzi.
Mapema mwaka
huu, Kamati hiyo iliendesha shindano dogo na kumpata Lissa Jensen ambaye
aliwakilisha nchi katika fainali za Dunia kutokana na mabadiliko ya kalenda
yaliyofanywa na Kamati ya Miss World na mrembo atakayetwaa taji hilo katika
fainali hizo zitakazofanyika hivi karibuni atapata muda mrefu wa kufanya
maandalizi.
Shindano la
Miss Tanzania lilianza rasmi mwaka 1994 na Aina Maeda alikuwa mshindi wa kwanza,
akifuatiwa na Shose Senare 1995, Emily Adolf 1996, Saida Kessy 1997, Basila
Mwanukuzi 1998, Hoyce Temu 1999, Jacqueline Ntuyabaliwe 2000, Happiness Magese
2001, Angela Damas 2002, Sylvia Bahame 2003, Faraja Kotta 2004, Nancy Sumary
2005, Wema Sepetu 2006, Richa Adhia 2007, Nasreem Kareem 2008, Miriam Gerald
2009, Geneveive Mpangala 2010 na Salha Israel 2011.
Awali ya
hapo, mwaka 1967 lilifanyika shindano la kwanza kabisa la Miss Tanzania na Theresa
Shayo akashinda katika shindano lililofanyika kwenye bwawa la kuogelea la
hoteli ya Kilimanjaro, lakini serikali ya Tanzania wakati huo, chini ya rais wa
kwanza, hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere ikapiga marufuku mashindano kwa
sababu hayaendani na mila na desturi za Mtanzania.
Lakini Lino
International Agency, ikajenga hoja ambazo ziliishawishi serikali ya Tanzania,
chini ya rais wake wa pili, Alhaj Ali Hassan Mwinyi kuruhusu mashindano hayo
yafanyike tena, ingawa mwaka 2001 yaliponea chupuchupu kufutwa tena, enzi za
rais wa awamu wa tatu, Benjamin William Mkapa.
Ilitokana na
vazi la kuogelea ‘kichupi’, ambalo lilipingwa kwa sababu linamdhalilisha
mwanamke wa Tanzania, lakini Lino ikaboresha kipengele cha vazi hilo, kutoka la
kuogelea hadi la ufukweni, ambalo kidogo linamsitiri binti na serikali
ikaruhusu mashindano yaendelee.
Hata hivyo,
mabinti wanapokwenda kwenye shindano la dunia, wanavaa vazi la kuogelea kupanda
jukwaani, katika shindano ambalo linaonyeshwa moja kwa moja nchi zaidi ya 100
duniani na picha zao kuchapishwa kwenye majarida, magazeti na mitandao mbalimbali
duniani.
Post a Comment