![]() |
Sanga kushoto, kulia ni Mjumbe wa Kamati ya Utendaji Yanga, Tito Osoro |
Na Mahmoud Zubeiry
MAKAMU
Mwenyekiti wa Yanga, Clement Sanga amesema kwamba atayafanyia kazi
masuala mawili ya madai dhidi ya klabu hiyo, la aliyekuwa kocha wa klabu
hiyo, Mserbia Kostadin Bozidar Papic na beki wao wa zamani, Mkenya John
Njoroge, ili kueipushia klabu hiyo hatari ya kuadhibiwa.
“Mambo
haya kwa kweli hatukuwa tukiyajua, ila baada ya taarifa hizi
tutayafanyia kazi, ili tuyamalize, tumeingia madarakani tumeyakuta, ila
kwa kuwa tumerithi klabu, basi tumerithi yote na hatuna budi kuyafanyia
kazi,”alisema Sanga.
Papic
amefungua mashitaka Shirikisho la Soka la Kimataifa (FIFA), dhidi ya
klabu hiyo, akidai malimbikizo yake ya mishahara, dola za Kimarekani
12,300, zaidi ya Sh. Milioni 15 za Tanzania.
Katibu Mkuu wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Angetile Osiah Malabeja aliiambia BIN ZUBEIRY jana
mchana kwamba, wamepokea barua kutoka Kitengo cha Sheria cha FIFA,
kikiwataka kuitaarifu Yanga kuhusu mashtaka yaliyowasilishwa na kocha
wao huyo zamani.
Angetile
alisema katika malalamiko yake, Papic anadai kuwa hajalipwa malimbikizo
ya mshahara wake yanayofikia kiasi cha dola 12,300 za Kimarekani na
alikuwa akiwasiliana na maofisa na viongozi waYanga, lakini hakupata
ushirikiano na hivyo kuamua kwenda FIFA.
Angetile
alisema TFF ilifanya juhudi za kuwasiliana na Yanga kuhusu malalamiko
hayo ili kujaribu kumzuia kocha huyo asishtaki FIFA, lakini juhudi hizo
hazikuzaa matunda.
“Na
kama chombo kinachosimamia uendeshaji wa soka nchini, TFF imesikitishwa
na habari hizo na inaiomba klabu ya Yanga kufanya kila jitihada
kuhakikisha kuwa inawasilisha taarifa zote muhimu na nyaraka
zinazohusiana na stahiki za kocha huyo ili kama ilishamalizana naye,
sifa ya klabu ya Yanga isafishwe,”alisema Angetile.
Alisema tayari wamekwishaiandikia barua Yanga kuitaka itekeleze utashi huo mapema iwezekanavyo.
“Tukio
hilo, si tu linachafua sifa ya klabu ya Yanga, bali soka ya Tanzania
kwa ujumla kutokana na ukweli kwamba ikishadhihirika kuwa kuna tatizo la
malipo ya makocha nchini, ni dhahiri kuwa itakuwa ni vigumu kwa klabu
zetu na hata timu za taifa kupata makocha wazuri kutoka nje kwa kuwa
watakuwa wamejengeka hofu ya kufanya kazi nchini,”alisema.
Hili
ni tukio la pili kwa Yanga baada ya mchezaji wake mwingine, John
Njoroge kuishtaki klabu hiyo FIFA na kushinda kesi yake iliyoamuliwa
mwezi Januari na Kitengo cha Usuluhishi wa Migogoro cha FIFA (DRC).
Alisema
ushindi wa Njoroge unamaanisha kuwa iwapo Yanga itashindwa kutekeleza
kumlipa mchezaji huyo kasi cha Sh milioni 17, inaweza kujikuta katika
adhabu ambayo itailazimisha TFF kuishusha daraja; kuinyang’anya pointi
kwa kiwango kitakachotajwa na FIFA; kuipiga faini au adhabu zote kwenda
kwa pamoja.
“Tunaiomba
Yanga itekeleze hukumu hiyo kwa wakati uliotajwa kwenye barua ya FIFA
ili kuepuka hatua hizo, suala la Njoroge ni moja kati ya matukio mengi
yanayohusu ukiukwaji wa taratibu za kuvunja mikataba yanayofanywa na
klabu zetu.
Post a Comment