HATIMAYE
Panga la Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Rais Jakaya Kikwete,
limewashukia vigogo wa chama hicho na kuwatupa nje ya kinyang’anyiro cha
kuwania nafasi za uongozi wa jumuiya za chama na ujumbe wa Halmashauri
Kuu ya Taifa (NEC).
Wakati
panga hilo likiwashukia baadhi ya vigogo, Rais Kikwete ametoa kauli
nzito ya kutaka wagombea waliopata kutoa kauli za vitisho dhidi ya chama
hicho kufanya kile walichokusudia kukifanya.
Kikwete
katika kauli yake hiyo alionekana waziwazi kukerwa na kauli za
‘patachimbika’ au zile za kutishia kujitoa na kujiunga na vyama vya
upinzani.
Akizungumza
kwa ukali, Kikwete ambaye juzi alitamba akisema CCM haitakufa kama
inavyotabiriwa na baadhi ya watu, alihitimisha kauli yake kwa kusema
watu wenye kauli za namna hiyo walikuwa hawafai kuendelea kuwa wanachama
wa chama hicho.
Panga la
Rais Kikwete limewaangukia wagombea wenye nyadhifa zaidi ya moja
serikalini na ndani ya chama pamoja na baadhi ya wabunge.
Wengine
waliokatwa na vikao hivyo vya juu vya CCM vilivyomalizika jana mjini
Dodoma, ni wagombea waliokuwa wakiibua malumbano na wakati mwingine
kuikosoa CCM hadharani, makada waliojipambanua kama wapiganaji na
wapambanaji wa ufisadi na baadhi ya wabunge walioweka saini zao bungeni
kuunga mkono hoja ya Mbunge wa Kigoma Kaskazini, Zitto Kabwe ya kutaka
Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, ajiuzulu.
Habari
kutoka ndani ya NEC, ziliwataja walioenguliwa kuwa ni pamoja na Mbunge
wa Nzega, Dk. Hamisi Kigwangalla na Mjumbe wa Baraza Kuu la Vijana la
CCM Taifa (UVCCM), Hussein Bashe.
Bashe na
Kigwangalla ambao wamekuwa katika mvutano mkubwa wa kusaka madaraka
ndani ya chama, majina yao yalipendekezwa kukatwa kuwania nafasi hiyo
kuanzia kwenye sekretarieti, Kamati ya Maadili na Kamati Kuu kabla ya
kuthibitishwa na NEC.Makada hao wamekuwa kwenye mvutano wa kisiasa uliodumu
toka mwaka 2010 wakati wa uchaguzi mkuu ambapo Bashe alienguliwa kuwania
ubunge, Jimbo la Nzega na nafasi yake kuchukuliwa na Dk. Kigwangalla
aliyeshika nafasi ya tatu. Nafasi ya pili ilichukuliwa na mbunge wa
zamani wa jimbo hilo, Lucas Selelii.
Mbali ya hao, panga hilo limemkata Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Shinyanga, Khamis Mgeja na Mbunge wa Kahama, James Lembeli.
Mgeja na
Lembeli nao wamekuwa katika mvutano mkubwa ndani na nje ya chama.
Uhasama wao unachochewa na kambi mbili kubwa zenye uhasama mkubwa.
Wengine waliokatwa ni Mbunge wa Kisesa, Luhaga Mpina na Mbunge wa Ludewa, Deo Filukunjombe.
Wabunge hao
ni miongoni mwa waliotia saini kutaka Waziri Mkuu Pinda ang’oke. Duru
za siasa zinasema kuwa msimamo wa wabunge hao kuhusu Pinda, ndio
ulisababisha wakatwe kuwania NEC.
Athari za
saini za kutaka kumng’oa Pinda ambazo zilisababisha Baraza la Mawaziri
lipanguliwe na kuundwa upya, zimeonekana pia kumgusa Mbunge wa Musoma
Vijijini, Nimrod Mkono, ambaye ametupwa nje kuwania nafasi ya uenyekiti
wa wazazi CCM taifa.
Mkono
ambaye ni wakili maarufu nchini, jina lake pia ni miongoni mwa majina
yaliyokatwa katika vikao vya ngazi za chini na hivi karibuni
alitahadharisha kuwa endapo hatarejeshwa na NEC, patachimbika.
Mbunge wa
zamani wa Nyamagana, Antony Diallo na Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Mwanza
aliyekuwa akitetea nafasi yake, Clement Mabina nao wamekatwa.
Akizungumza
baada ya kufanya maamuzi hayo magumu, Rais Kikwete alisema anashangaa
kuona baadhi ya wagombea wa nafasi mbalimbali ndani ya chama hicho
wakitaka kuuana kuingia NEC na kugeuza uchaguzi huo kuwa uwanja wa
mapambano na kuwa na ndimi mbili.
Rais Kikwete alitoa kauli hiyo mjini hapa jana wakati akifunga kikao cha NEC.
Alisema
hivi sasa wagombea wengi wamekuwa wakijitokeza kuwania nafasi mbalimbali
za uongozi ndani ya CCM na kung’ang’ania kupata ushindi kiasi cha
wengine kufikia hatua ya kutoa kauli za vitisho kwa kusema wasipopata
nafasi ‘patachimbika’.
“Inashangaza kuona kugombea NEC tu watu wanataka kuuana, wanakimbilia nini huko ndani?” alihoji Rais Kikwete.
“Ina maana
watu hawa wanaonyesha dhahiri kuwa hawana nia njema na chama, bali
wanaingia kwa maslahi yao binafsi, hivyo tuna kila sababu ya kuwakataa
ili tujenge timu ya ushindi ambayo ndiyo nia yetu,” aliongeza mwenyekiti
huyo.
Alitumia
nafasi hiyo kuwataka wanachama kutogeuza uchaguzi huo kuwa uwanja wa
fujo kwa kutumia silaha, majembe, ngumi na mikuki kwani hiyo ni fedheha
kubwa kwa chama hicho.
Rais
Kikwete alisema kama kuna wagombea ambao watajitoa ndani ya CCM na
kuhamia chama kingine kutokana na majina yao kutopendekezwa, wajitoe.
“Hatuchagui
wagombea wenye ndimi mbili ambao wanasema kama hatutapitishwa tutahamia
chama kingine, hao tunawatakia kila la heri waende tu, kwani hawana nia
njema na chama hiki,” alisema.
Mwenyekiti
huyo ambaye alikuwa akizungumza kwa ukali, alisema anajua suala la
kuwaengua baadhi ya wagombea litazua mjadala, lakini nia ya chama ni
njema katika kuleta sura mpya na uhai.
“Kufanya
hivyo ni pamoja na kupata viongozi watakaokiletea chama ushindi katika
chaguzi za Serikali za Mitaa 2014 pamoja na Uchaguzi Mkuu mwaka 2015,
hivyo lazima watu hao watambue kuwa kazi wanayoifanya ni kuunda timu ya
ushindi wa chama na si wa watu.
“Najua kuna
ndugu na marafiki ambao hawatateuliwa kutokana na kujaa kwa nafasi na
mapungufu na madhaifu ambayo yalionekana baada ya Kamati ya Maadili
kupitia majina yao, hivyo wasione kama wameonewa bali wajue kama ndio
utaratibu wa chama wa kuhitaji viongozi shupavu, hodari na mwenye uwezo
wa kukitetea na kukipigania chama na kukipa ushindi,” alisema Rais
Kikwete.
Aliwatahadharisha
wagombea watakaotumia rushwa kwenye kampeni zao watambue kuwa Taasisi
ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) wanafanya kazi yao muda
wote, hivyo atakayekamatwa asije akamlaumu mtu.
SOURCE TANZANIA DAIMA
Post a Comment