Baadhi
ya waumini wa dini ya Kiislamu wakiwa wamekusanyika nje ya Makao Makuu
ya Wizara ya Mambo ya Ndani, Dar es Salaam jana kushinikiza kuachiliwa
kwa wenzao waliokamatwa kwa kuchochea wenzao wagomee kuhesabiwa katika
Zoezi la Sensa ya Watu na Makazi.
Makao
Makuu ya Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi jijini Dar es Salaam jana
yalikumbwa na wingu zito pale kundi kubwa la waumini wa dini ya Kiislamu
kutoka Jumuiya za Kiislamu Tanzania walipovamia makao makuu hayo,
kushinikiza kuachiwa huru kwa Waislamu waliokamatwa kwa kuhujumu sensa.Kutokana na ukubwa wa shinikizo lililooneshwa na kundi hilo la Waislamu waliozuiwa nje ya lango la kuingilia na viongozi wao kuruhusiwa kuingia ndani na kuonana na viongozi wa juu wa Jeshi la Polisi na Wizara akiwemo Katibu Mkuu Mbarak Abdulwakil, Serikali ilikubaliana na matakwa ya kuachiwa mara moja kwa watu waliokamatwa kwa kukataa kushiriki sensa.
Hali ya wasiwasi ilianza kutanda katikati ya Jiji la Dar es Salaam katika maeneo ya Posta yalipo Makao Makuu hayo ya Wizara, pale Waislamu walipofika kwa maandamano huku wakiimba na kubeba mabango yenye ujumbe mbalimbali na kuzingira jengo la wizara hiyo kuanzia saa saba mchana hadi saa 10 jioni walipoondoka baada ya matakwa yao kutimizwa.
Pamoja na kuimba nyimbo mbalimbali za Kiislamu, pia walibeba mabango yenye ujumbe, Sensa imefeli kwa asilimia 95; IGP Mwema na Kova hamuoni Waislamu tunavyoonewa; Nchi hii inaongozwa na Mfumo Kristo; Miaka 51 ya Uhuru wa Tanzania Waislamu bado tunadhulumiwa; Tanzania ni nchi yetu sote Waislamu na Wakristo, Bakwata ni mawakala wa Serikali na Jeshi la Polisi; Kamatakamata na mauaji ya polisi yataendelea hadi lini na mengineyo.
Tofauti na ilivyozoeleka, katika patashika hiyo ya jana, askari polisi walionekana kuwa wapole huku wakishiriki kuzuia kundi hilo kulifikia lango kuu bila kutumia nguvu ingawa baadhi yao walikuwa na silaha kali za kivita na mabomu ya machozi ambazo hazikutumika.
Ilipofika saa 10 jioni wakati viongozi wao wakiwa bado wanajadiliana ndani na viongozi wa wizara hiyo, Waislamu hao walifanya swala ya alasiri na swala ya kunuti huku wakitumia mchanga na udongo kutawaza badala ya maji kama ilivyozoeleka, kitendo ambacho kinadaiwa kuwa hufanywa jangwani ambako hakuna maji. Swala hiyo iliendeshwa na Mzee Mwinyikai.
Wakiwa katika eneo hilo, alifika Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Suleiman Kova, akiambatana na Katibu Mkuu Abdulwakil na baada ya kuingia ndani, Kova alitoka na kutaka kujaribu kuzungumza na Waislamu hao, lakini hata hivyo walimgomea na hivyo Kova kurudi ndani.
Katika taarifa yao iliyosainiwa na Katibu wa Umoja huo wa Jumuiya za Kiislamu Tanzania, Mucadamu Swalehe, Waislamu hao walitaka pamoja na serikali kuwaachia waliokamatwa kwa kudaiwa kuhujumu sensa, lakini pia iunde Tume yenye mchanganyiko wa dini kutathmini mwenendo wa sensa, kuwepo na uwakilishi wa dini kwenye ukusanyaji wa takwimu mbalimbali na pia kipengele cha dini kurejeshwa kwenye dodoso la sensa.
Baada ya kumalizika kwa majadiliano, viongozi wa Waislamu hao walitoka nje na mmoja wa wanakamati Jafari Mneke alisoma maazimio ya kikao hicho huku viongozi wa juu wa jeshi la polisi wakishuhudia, ambapo aliwatangazia kwamba Serikali imesema itawaachia mara moja kuanzia jana Waislamu wote waliokamatwa kutokana na kukiuka masharti ya sensa.
"Mambo mengine wamesema watayatekeleza Jumatatu, lakini hili la kuachiwa kwa Waislamu wote waliokamatwa kwa kuipinga sensa ambayo ni haramu, serikali imeahidi kuwaachia mara moja kuanzia sasa. Kitendo hiki ni ushindi mkubwa kwetu maana ndicho kilichotuleta.
"Tulipokuwa tunakuja tulisema hatutaondoka hapa hadi matakwa yetu yatimizwe vinginevyo tungekuwa tayari kufa kwa kupigwa risasi. Kwa vile tumeibuka na ushindi sasa tuondoke turudi pale Magomeni Mchangani tukapange mikakati ya mapambano zaidi na pia mikakati ya kwenda pale NECTA (Baraza la Mitihani Tanzania) kumuondoa Ndalichako (Dk. Joyce Ndalichako- Katibu Mtendaji wa NECTA) na kuhakikisha kuwa NECTA inafumuliwa na kuundwa upya," alisema Mneke na kushangiliwa kwa nguvu na Waislamu hao.
Taarifa
ya maandishi iliyotolewa baadaye na Katibu Mkuu wa Mambo ya Ndani,
Mbarak Abdulwakil ilieleza kuwa, Serikali imepokea risala ya Waislamu na
kwamba itafikishwa kwa Waziri wa Mambo ya Ndani, Dk. Emmanuel Nchimbi
na Naibu wake, Pereira Ame Silima ambao walikuwa nje ya Dar es Salaam
kikazi.
Aidha,
imeagiza Makamanda wote wa polisi wa mikoa kusitisha ukamataji wa watu
kutokana na suala la sensa na kwamba watuhumiwa waliokamatwa waachiwe
kwa dhamana.
Abdulwakil,
katika taarifa hiyo amesisitiza kuwa, mambo yote yaliyotajwa katika
risala hiyo ya Waislamu yatashughulikiwa mara baada ya mawaziri wenye
dhamana kuripoti ofisini.
Post a Comment