Waziri
Mkuu mstaafu Frederick Sumaye (pichani), amevishauri vyombo vya dola,
hasa Polisi kutumia busara zaidi katika kutatua migogoro inayojitokeza
badala ya kutumia nguvu nyingi na silaha, kwa vile jambo hilo linaweza
kuchochea machafuko na kuvuruga amani na utulivu uliojengeka nchini.
Sumaye
aliyasema hayo alipokuwa akijibu maswali ya waandishi wa habari wa
vyombo mbalimbali, wakiwemo pia na Wahariri wa Habari na Mameneja wa
Vyumba vya Habari, nje ya ukumbi wa Hoteli ya Nashera ya mjini hapa
juzi, baada ya kufunga mafunzo ya kuwajengea uwezo wa uongozi na
utendaji wahariri hao.
Akijibu
swali kuhusu kifo cha Mwandishi wa Habari, Daudi Mwangosi, mwakilishi
wa Kituo cha Televisheni cha Channel Ten aliyeuawa kwa kupigwa na bomu
la machozi na polisi katika kijiji cha Nyololo, Mufindi mkoani Iringa
hivi karibuni.
"Watu
wote wanaliangalia tukio hili kwa masikitiko makubwa, lakini kuna kitu
cha kujifunza kama Vyombo vya Serikali kwa ujumla wake," alisema.
Kwa
mujibu wa Waziri Mkuu mstaafu huyo wa Serikali ya Awamu ya Tatu, Polisi
watumie busara katika kutatua matatizo bila kutumia nguvu za ziada ama
silaha kwani mapambano hayawezi kuleta amani, bali yanaendeleza
machafuko na kulitia doa taifa.
Waziri
Mkuu mstaafu Sumaye alisema risasi haiwezi kutatua kila kitu, bali
inaharibu na kuchochea vurugu na kusisitiza kuwa hatua ya aina hiyo
itumike pale tu ambapo juhudi zote zimeshindwa na kwamba bado watanzania
si watu wenye hulka ya kufanya fujo.
"Si
lazima kila tukio ni la kutumia silaha, bali kuwepo na njia nyingine za
kumaliza matatizo na silaha itumike pale tu hali inabidi iwe hivyo,"
alisema Waziri Mkuu mstaafu.
Hata
hivyo, alipingana na dhana iliyojengwa kuwa mauaji hayo yametokana na
kuhusishwa na siasa kwa kusema kuwa, yapo mambo mengi yamefanyika ya
kuwepo matumizi ya nguvu kubwa ikiwemo wakati wa ubomoaji wa nyumba.
Alisema,
mazingira ya siasa yameonekana kuchangamka zaidi tofauti na huko nyuma,
hivyo wanasiasa huenda wakachangia kuchokoza Polisi, lakini pia ni
wajibu wa jeshi hilo kutumia busara wakati wa kukabiliana na mambo hayo,
kuliko kutumia nguvu na silaha hasa ikizingatiwa risasi haiwezi kutatua
jambo, bali ni kuharibu.
Hata
hivyo, alisema si kwamba waandishi wa habari wanawindwa na Polisi, bali
ni pamoja na kukimbizana na raia waliopo vijijini na jambo hilo bado
halitoi taswira ya kujenga uhusiano mzuri.
"Sijui
siku hizi watu hawatii amri, kwani hata wananchi vijijini Polisi
wanapambana nao, sijui Polisi wetu wamekuwa wakali sana au ni kukosa
weledi wa kimafunzo," alibainisha Waziri Mkuu mstaafu.
Wakati
huo huo, Sumaye amewataka waandishi wa habari kuacha tabia ya kuandika
habari za kuyapendelea makundi fulani ya watu, wakiwemo wanasiasa kwa
msingi wa kuahidiwa vitu ama kupewa fedha pamoja na kutumiwa kuwachafua
watu wengine katika jamii, hasa wakati wa uchaguzi.
Alionya
kuwa, mazingira ya aina hiyo yanachangia kuporomosha maadili ya taaluma
hiyo nyeti, huku akisisitiza hali hiyo isiendelee kupewa nafasi.
"Baadhi
ya watu wanadiriki kutumia kila liwezekanalo katika kuhakikisha
wanawachafua wenzao kwa kutumia kalamu kwa kujua kalamu ina nguvu kubwa
sawa na silaha.
"Wanatumia
nguvu ya kalamu, lakini tatizo si kutumia kalamu, bali ni kwa matakwa
binafsi yanayosukumwa na matumizi ya fedha inayotoa msukumo kwa baadhi
ya waandishi wa habari kuamua kuandika habari inayomchagua mtu, kikundi
pasipo kufuata maadili ya uandishi wa habari," alisema na kuonya kuwa,
uandishi wa habari usiozingatia maadili, unaweza kusababisha madhara
makubwa mtu mmoja mmoja, taaluma ya uandishi na kwa jamii kubwa.
Post a Comment