Matokeo ya chaguzi za ndani ya Chama Cha Mapinduzi
(CCM), yameibua taswira isiyotarajiwa kutokana na kundi linalomuunga mkono
Waziri Mkuu aliyejiuzulu, Edward Lowassa, kupata ushindi mnono.
Tayari CCM inaaminika kuwa katika wakati mgumu kuelekea
Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015, ambapo ‘safu’ iliyoshinda maeneo tofauti ya uongozi
na vikao vikubwa vya chama hicho, wapo upande wa Lowassa.
Lowassa ambaye mwaka 2005 alikuwa mmoja wa wasaidizi wa
karibu wa Rais Kikwete, alipowania urais kwa mara ya kwanza, anasadikiwa
kukigawa chama hicho hasa baada ya kuibuka kwa kashfa mbalimbali za rushwa na
matumizi mabaya ya madaraka.
Lakini kashfa kubwa zaidi ni ile iliyohusu mkataba
wenye utata wa kuzalisha umeme, uliosainiwa kati ya serikali ya kampuni ya
Richmond, ambao hata hivyo ulikuwa chanzo cha kujiuzulu kwake
(Lowassa).
Chanzo cha habari cha kuaminika kutoka ndani ya mtandao
unaoegemea upande wa Lowassa, kimeliambia NIPASHE Jumapili kuwa, hadi kufikia
mwishoni mwa wa wiki, walikuwa wamemiliki asilimia 65 ya wajumbe wa Halmashauri
Kuu ya Taifa (Nec).
Takwimu hizo zinajumuisha matokeo ya uchaguzi wa
jumuiya ya Umoja wa Vijana wa CCM (UV-CCM) ambapo kwa mujibu wa chanzo hicho cha
kuaminika, ni watu watatu pekee walioshinda, ambao hawamuungi mkono
Lowassa.
“Huyu jamaa (Lowassa) anaenda vizuri na inavyoonekana
hakuna namna ya kumzuia katika urais 2015,” kilieleza chanzo hicho ambacho hata
hivyo, kinasisitiza kuhifadhiwa kwa jina lake.
Matokeo ya chaguzi hizo yamelalamikiwa sehemu kubwa ya
nchi, kwamba ulitawaliwa na vitendo vya rushwa, lakini Katibu wa Itikadi na
Uenezi wa CCM, Nape Nnauye, alikana na kusema hali ni shwari na kwamba kashfa
hizo zinakuzwa na vyombo vya habari.
LOWASSA AZIDI KUTETEWA
Wakati shutuma na tuhuma zinazomhusisha Lowassa
zikitolewa sehemu tofauti, wapo wana-CCM wanaoamini kwamba kiongozi huyo ni
jasiri na kwamba ana uwezo wa kuongoza.
Mjumbe wa Baraza Kuu la UVCCM, Hussein Bashe, amekaririwa akisema Lowassa ni kiongozi mwenye uvumilivu na anayedhihirisha kuwa tayari kukabiliana na kuvishinda vikwazo, hivyo kustahili uongozi wa nchi.
Bashe ambaye jina lake lilitajwa katika tuhuma za rushwa wakati wa uchaguzi wa UVCCM mjini Dodoma hivi karibuni, alisema anajisikia fahari kuzifuata na kuzitekeleza siasa za Lowassa.
Kauli hiyo ni tofauti na zile zilizowahi kutolewa na wanaojulikana kama ‘makamanda wa ufisadi’ akiwemo Waziri wa Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Samuel Sitta na Waziri wa Ujenzi, Dk Harrison Mwakyembe.
Makamanda wa ufisadi wamekuwa wakiwataja matuhumiwa wa ufisadi ambao jina la Lowassa limekuwa miongoni mwao, kuwa wanastahili kufukuzwa uanachama na kunyimwa nafasi ya uongozi wa nchi.
Chanzo: Nipashe
Post a Comment