Loading...
UTORO WA WABUNGE WAKWAMISHA AZIMIO
************************
ulius Magodi na Hebel Chidawali, Dodoma
UTORO wa baadhi ya wabunge jana ulikwamisha kupitishwa kwa azimio la Marekebisho ya ya Pili ya Mkataba wa Ushirikiano Kati ya Jumuiya ya Nchi za Ulaya na Nchi za Afrika, Caribean na Pacific (ACP).
Hii ni mara ya pili kwa wabunge kukwamisha shughuli za Bunge katika kipindi cha miezi minne kutokana na utoro. Awali, utoro huo ulikwamisha kupitishwa kwa Bajeti ya Wizara ya Kilimo, Chakula na Ushirika.
Kukwama kwa bajeti hiyo kulikuja wiki moja tu tangu Spika wa Bunge, Anna kukemea tabia ya utoro akisema tabia hiyo ilikuwa imekithiri.
Jana, hali hiyo ilitokea baada ya Waziri wa Fedha, Dk William Mgimwa kuhitimisha kujibu hoja mbalimbali za wabunge waliochangia azimio la mkataba huo aliloliwasilisha baada ya kipindi cha maswali na majibu.
Mara baada ya Waziri Mgimwa kumaliza kujibu hoja ili kutoa nafasi kwa Bunge kupitisha azimio hilo, ndipo Mbunge wa Mkanyangeni (CUF), Mohammed Mnyaa aliposimama na kuomba mwongozo wa Spika kwa kutumia Kanuni ya Bunge, Kifungu cha 68 akitaka Bunge lisipitishe azimio hilo kutokana na idadi ndogo ya wabunge waliokuwa ndani ya ukumbi.
Aliomba Bunge lipange muda mwingine wa kupitisha azimio hilo ili marekebisho yaliyopo katika mkataba huo yapitishwe kwa mujibu wa kanuni.
Spika wa Bunge, Anne Makinda alikubaliana na ombi hilo na kuahirisha kulipitisha azimio hilo hadi leo asubuhi.
Kwa mujibu wa Kanuni za Bunge, Kifungu cha 77 (1), akidi kwa kila kikao cha Bunge wakati wa kufanya uamuzi itakuwa ni nusu ya wabunge wote, kama ilivyofafanuliwa katika Ibara ya 94 ya Katiba, isipokuwa kwamba, idadi hiyo haitahusu hoja kuhusu uamuzi wa kubadilisha masharti yoyote ya Katiba kwa mujibu wa Ibara ya 98 ya Katiba.
Wakati Spika akiahirisha Bunge, baadhi ya wabunge walionekana wakiwa nje ya ukumbi wa Bunge huku wengine wakiwa katika mghahawa uliopo katika viwanja hivyo.
Bunge la Tanzania kikatiba, linapaswa kuwa na wabunge 357.
Akichangia azimio hilo Mbunge wa Ubungo (Chadema), John Mnyika aliishauri Serikali kuwa makini na mikataba ya kimataifa huku akitaka mkataba huo wa ACP usaidie kurejeshwa kwa Sh360 bilioni zilizofichwa nchini Uswisi na baadhi ya Watanzania.
Mnyika alisema kifungu cha 29 cha mkataba huo kinataja ushirikiano katika nyanja mbalimbali ikiwamo kuzuia biashara haramu na rushwa.
Alitaka Serikali itumie kifungu hicho kuomba mabilioni ya fedha yaliyofichwa na baadhi ya Watanzania katika benki mbalimbali huko Uswisi.
Suala hili limeibuka bungeni wakati, Mbunge wa Kigoma Kaskazini (Chadema), Zitto Kabwe mwishoni mwa wiki iliyopita alikaririwa akimtuhumu , Mkurugenzi wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), Dk Edward Hosea kuwa ameiandikia barua Serikali ya Uswisi akieleza kuwa Serikali ya Tanzania haina maslahi na fedha hizo madai ambayo Dk Hoseah aliyakanusha. Zitto alidai kuwa fedha hizo zimefichwa na vigogo 10.
Mbunge wa Kisarawe (CCM), Seleman Jaffo akichangia azimio hilo, aliitahadharisha Serikali kuwa makini wakati wa kuingia mikataba ya kimataifa akisema mingine inaweza kuwa na matatizo kwa taifa.
Alisema Watanzania wasipokuwa makini katika kuingia mikataba ya kimataifa, wanaweza kujikuta wanaridhia mambo yasiyofaa kwa taifa kama vile kukubali ndoa za jinsia moja.
Awali, akiwasilisha azimio hilo, Dk Mgimwa alisema madhumuni ya mkataba huo ni kujenga ushirikiano imara utakaowezesha kujenga uchumi endelevu ili kupunguza umasikini katika nchi wanachama.
chanzo: Mwananchi
Post a Comment