…………………………………………………
Na Mwandishi Wetu
Mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba Jaji
Joseph Warioba amesisitiza umumihu wa wananchi kutoa maoni maoni yao kuhusu
Katiba Mpya badala ya kukimbilia kuwasilisha maoni waliyolishwa na viongozi wa
vyama vya siasa, asasi za kiraia na kidini.
Jaji Warioba ameyasema hayo leo (Jumanne,
Oktoba 16, 2012) katika mkutano kati ya Kamati ya Bunge ya Katiba, Sheria na
Utawala na uongozi wa Tume hiyo uliofanyika katika ofisi za Tume jijini Dar es
Salaam.
Kwa mujibu wa Waziri Mkuu Mstaafu huyo baadhi
ya viongozi hao na wadau wengine wanadhani maamuzi ya kazi ya kukusanya maoni
inayofanywa kwa sasa na Tume yatamuliwa kwa kura na hivyo kuwalisha wananchi
maoni ili wayatoa kwa Tume kwa wingi.
“Wengine wanafikiri huu ni wakati wa kupiga
kura…hapana, sisi tunatafuta hoja,” alisema Mwenyekiti huyo na kuwataka wadau
mbalimbali kuwaacha wananchi watoe maoni yao binafsi.
Awali akiongea katika mkutano huo, Mjumbe wa
kamati hiyo ambaye pia ni Mbunge wa Muhambwe, Bw. Felix Mkosamali alipendekeza
Tume iwe inagawa kwa wananchi fomu maalum za kujaza maoni yao siku kadhaa kabla
ya Tume kufika ili kuwapa wananchi fursa ya kuandika maoni kwa kina tofauti na
sasa ambapo Tume hutoa karatasi hizo kabla ya kuanza
mkutano.
Akifafanua kuhusu hilo, Jaji Warioba amesema
uamuzi wa Tume kugawa fomu hizo mkutanoni unalenga kupata maoni binafsi ya
wananchi na kuongeza kuwa fomu hizo zikigawiwa mapema kuna uwezekano mkubwa kwa
wananchi kujaziwa maoni na watu wengine.
“Uzoefu wetu umeonyesha hili la watu kuelekezwa
nini cha kusema ambacho kwa kwli hawavijui kwa kina,” alisema katika mkutano huo
uliohudhuriwa pia na Naibu Waziri wa Katiba na Sheria Angellah Kairuki, Katibu
wa Tume hiyo Bw. Assaa Rashid na Naibu Katibu Bw. Casmir
Kyuki.
Pamoja na ufafanuzi kuhusu utoaji maoni binafsi
ya wananchi, Mwenyekiti huyo pia aliwaeleza Wajumbe wa Kamati hiyo kuwa lengo
la Tume ni kuhakikisha kuwa mchakato wote wa uandikaji wa katiba unakuwa wazi na
wananchi wanashiriki kikamilifu.
“Tukimaliza kukusanya maoni, tutaingia hatua ya
pili ya Mabaraza ya Katiba katika kila wilaya na baadhi ya taasisi ambapo
tunataka wananchi wenyewe katika maeneo husika wachague nani awawakilishe katika
mabaraza hayo,” alisema Mwenyekiti huyo.
Ufafanuzi huu ulifuatia swali la Mjumbe wa
Kamati hiyo ambaye pia ni Mbunge wa Kawe, Bi. Halima Mdee aliyeomba ufafanuzi
kuhusu upatikanaji wa wajumbe wa Mabaraza ya Katiba ambayo yanapitia rasimu ya
Katiba itakayowasilishwa na Tume.
Akifafanua zaidi, Jaji Warioba alisema Tume
imepanga kufanya mikutano miwili katika kila wilaya ambapo wawakilishi wa
wananchi watajadili rasimu ya Katiba itakayowasilishwa na Tume baada ya
kukusanya maoni yao katika awamu ya kwanza.
“Ni hatua ambayo tunadhani itahitaji fedha
nyingi hasa katika kuwasafirisha hao wawakilishi wa wananchi kuja katika
mikutano…hatutaki kuona wananchi wanapata sababu ya kutoshiriki hatua hii
muhimu,” alisema na kuwaomba Wajumbe wa Kamati kuzingatia hoja hizo pale Tume
itakapoomba fedha zaidi.
Pamoja na maoni hayo, Wajumbe hao pia
waliieleza Tume umuhimu wa kuongeza utoaji elimu kwa umma kuhusu masuala
mbalimbali yanayohusu Tume na Katiba.
Kwa upande wake, Naibu Waziri Kairuki alisema
Serikali itaendelea kuipa Tume hiyo kila aina ya ushirikiano ili itekeleze
majukumu yake kwa ufanisi na kuwaomba Wabunge hao kuendeleza ushirikiano
wanaoipa Tume hiyo.


Post a Comment