Meneja wa Sekta Kupunguza Umaskini na Kusimamia
Maendeleo ukanda wa Afrika wa Benki ya Dunia Dkt Albert Zeufack, akongea wakati
wa mkutano na wanahabari Ikulu jijini Dar es salaam leo kuhusu sekta ya Gesi
asilia nchini, akiwa ameongozana na mabalozi wa nchi kadhaa pamoja na Timu ya
wataalam walioletwa na washirika wa maendeleo na inayowakilisha Benki ya
Maendeleo ya Afrika, Benki ya Dunia, Shirika la Fedha la Kimataifa, Jumuiya ya
Nchi za Ulaya na Nchi za China, Uingereza na Ujerumani
Katibu Mkuu Kiongozi Balozi Ombeni Sefue akongea
wakati wa mkutano na wanahabari Ikulu jijini Dar es salaam leo kuhusu sekta ya
Gesi asilia nchini. Nyuma yake mwenye laptop ni Meneja wa Sekta Kupunguza
Umaskini na Kusimamia Maendeleo ukanda wa Afrika wa Benki ya Dunia Dkt Albert
Zeufack, akiwa ameongozana na mabalozi wa nchi kadhaa pamoja na Timu ya wataalam
walioletwa na washirika wa maendeleo na inayowakilisha Benki ya Maendeleo ya
Afrika, Benki ya Dunia, Shirika la Fedha la Kimataifa, Jumuiya ya Nchi za Ulaya
na Nchi za China, Uingereza na Ujerumani
Mkutano huo ulihudhruiwa pia na mabalozi wa nchi
kadhaa pamoja na timu ya wataalam walioletwa na washirika wa maendeleo na
inayowakilisha Benki ya Maendeleo ya Afrika, Benki ya Dunia, Shirika la Fedha
la Kimataifa, Jumuiya ya Nchi za Ulaya na Nchi za China, Uingereza na
Ujerumani ilipotembelea Ikulu
jijini Dar es salaam leo. Wa pili kushoto ni Waziri wa Katiba na Sheria Bw. Mathias Chikawe,
akifuatiwa na Naibu Katibu Mkuu Ikulu Mama Suzan Mlawi na maafisa waandamizi wa Ofisi ya Rais,
kamati hiyo
Katibu Mkuu Kiongozi Balozi Ombeni Sefue akitoa
ufafanuzi kwa baadhi ya waandishi wa habari baada ya mkutano na wanahabari Ikulu
jijini Dar es salaam leo kuhusu sekta ya Gesi asilia nchini..PICHA NA
IKULU
TAARIFA KWA
VYOMBO VYA HABARI: YALIYOSEMWA NA KATIBU MKUU KIONGOZI LEO WAKATI WA PRESS
CONFERENCE
_________________________
Katika miaka ya
karibuni kumekuwepo kwa ugunduzi mkubwa wa gesi asili nchini Tanzania katika
maeneo ya mwambao na maeneo ya kina kirefu cha bahari ambapo mpaka sasa jumla ya
futi za ujazo trilioni 33 zimegunduliwa. Kazi ya utafutaji inaendelea na upo
uwezekano wa ugunduzi zaidi.
Kiasi hicho
kilichothibitika hadi sasa hakitoshi kutuingiza kwenye ligi ya wazalishaji gesi
wakubwa duniani. Hata jirani zetu Msumbiji wanayo gesi asilia iliyothibitika
nyingi zaidi kuliko sisi.
Lakini kiasi cha
gesi asilia kilichothibitika katika nchi yetu kinatosha kutuwezesha kuwa
wazalishaji muhimu wa gesi asilia, na tukijipanga vizuri na kuisimamia kwa
umakini sekta hii ndogo, inaweza kutusaidia kuharakisha
maendeleo.
Kinyume chake,
tusipojipanga na kuisimamia vizuri tunaweza, kama nchi, tusipate faida kubwa.
Mbaya zaidi ipo mifano ya kutosha ya nchi ambazo uvumbuzi wa gesi na mafuta
umevuruga uchumi wao.
Hivyo, kabla
hatujaenda mbali ni muhimu kama taifa tuwe na uhakika wa tunachokitaka na
tujijengee uwezo wa kufanya maamuzi sahihi ikiwemo kwenye kutunga sera, kuandaa
mkakati na kutunga sheria itakayosimamia uendelezaji wa sekta ndogo ya
gesi.
Katika kufanya
hivyo, hatuna sababu ya kuvumbua upya gurudumu. Duniani upo uzoefu wa kutosha wa
nchi ambazo hazikusimia vizuri sekta hii na kuharibiwa. Ipo pia mifano na uzoefu
wa kutosha wa waliosimamia vizuri na kufanikiwa.
Sisi tunaoanza leo
tuna fursa ya kuepuka makosa waliyofanya wengine na tuna fursa ya kuchukua
uzoefu wa waliofanya vizuri. Lakini lazima tuchukue hatua sasa. Tukichelewa
itakuwa vigumu kurekebisha makosa baadaye.
Serikali imepania tusifanye
makosa na inaandaa utaratibu bora wa kusimamia uendelezaji wa sekta ndogo ya
gesi asili. Tunataka kuhakikisha kunakuwepo uwajibikaji, uwazi na uongozi bora
ili Taifa letu lipate mapato stahiki yatokanayo na uvunaji wa rasilimali hii, na
mapato hayo yatumike vizuri kama msingi wa kujenga uchumi endelevu wa kisasa,
utakaonufaisha wananchi wengi zaidi.
Mchakato wa kupata maoni ya
wadau wote ndani ya nchi unaendelea, lakini pia tunahitaji uzoefu na ushauri
kutoka kwingine duniani. Na ndio maana kwa karibu wiki moja sasa tumekuwa na
ugeni wa Timu ya wataalam walioletwa na washirika wa maendeleo kutokana na
maombi yetu. Timu hiyo inawakilisha Benki ya Maendeleo ya Afrika, Benki ya
Dunia, Shirika la Fedha la Kimataifa, Jumuiya ya Nchi za Ulaya na Nchi za China,
Uingereza na Ujerumani.
Tumekuwa na
majadiliano kadhaa na Timu hii ambayo imekutana na wadau mbalimbali ikiwemo
Serikali, taasisi za umma, makampuni ya utafutaji wa mafuta na gesi, sekta
binafsi, asasi zisizo za kiserikali, wanazuoni, baadhi ya viongozi wa vyama vya
upinzani na wenyeviti wa Kamati za Bunge. Mikutano hii ililenga kuipa Timu hii
mawazo na maoni wa wadau muhimu ndani ya Tanzania ili wayazingatie katika
ushauri wao kwetu. Mazungumzo yote yalikwenda vizuri na yana manufaa
makubwa.
Napenda kusisitiza
mambo yafuatayo:-
(i) Timu hii tumeiomba sisi. Kama
mnavyoona ina uwakilishi mpana wa Washirika wa Maendeleo. Hivyo, badala ya
kujadiliana na mmoja mmoja tumepata fursa ya kuzungumza nao wote kwa
pamoja.
(ii) Uamuzi wa mwisho kuhusu sera,
mkakati na sheria zitakazotawala sekta hii, ni wetu kwa asilimia mia moja.
Lakini katika kuamua tunataka tupate uzoefu wa wengine, ushauri wa kitaalam na
taarifa zote muhimu za kutuwezesha kufanya maamuzi sahihi. Kwa mfano,
tunachohitaji kutoka kwa Timu hii ni:-
(a) Uzoefu wa nchi ambazo zimefanya vibaya
katika kusimamia sekta zao za mafuta na gesi asilia. Lengo ni kuhakikisha
hatufanyi makosa waliyofanya wengine.
(b) Uzoefu wa nchi ambazo zimefanya vizuri
katika kusimamia sekta hii. Lengo ni kuzingatia yale yote yaliyothibitika kwa
wengine kuwa ni ya manufaa.
Mambo ya msingi kwa upande wa
Serikali ni kuhakikisha:-
(a) Tunakuwa na mikataba bora inayolinda
maslahi ya taifa lakini bila kukosa mvuto kwa wawekezaji. Hivyo tunahitaji
kujenga uwezo mkubwa kwenye eneo hili.
(b) Tunahimiza wajasiriamali wetu wajiandae
kutoa huduma kwa makampuni makubwa ya gesi ili kupata manufaa zaidi kutokana na
gesi.
(c) Tunaandaa watalaam na mafundi wanaoweza
kuajiriwa na makampuni ya gesi.
(d) Tuna mfumo thabiti wa kusimamia matumizi
ya mapato yakatakayotokana na gesi ili yasiyumbishe uchumi mkuu wa nchi bali
yawe msingi wa uwekezaji katika kubadili mfumo wa uchumi wetu na maendeleo
endelevu.
(e) Tuna mfumo thabiti na uwezo wa
usimamizi na udhibiti.
Pamoja na hayo ni muhimu
wananchi waelewe kuwa hatutakuwa matajiri mara moja. Hatutarajii mapato katika
miaka michache ijayo. Isitoshe lazima tufikirie vizazi vijavyo. Sisi tulio hai
leo ni wadhamini wa kile ambacho vizazi vijavyo vitarithi kutoka kwetu. Hivyo
itabidi tufikiri vya kutosha na kuamua kiasi gani cha mapato tutakayopata
kitumike leo na kiasi gani kitumike kujenga msingi wa maisha bora ya vizazi
vijavyo hasa ikizingatiwa kuwa kuna siku gesi hiyo
itakwisha.
Nawashukuru
washirika wa maendeleo waliotoa wajumbe kushiriki kwenye timu hii. Pia
nawashukuru wajumbe wenyewe kwa ushirikiano mzuri waliouonyesha wakati wa zoezi
hili.
Aidha nawashukuru watanzania walioshiriki na kutoa maoni yao hata kufanikisha zoezi hili.
Kwa pamoja tuhakikishe Tanzania inakuwa mfano bora wa matumizi sahihi ya rasilimali hii kwa faida na maendeleo yetu na vizazi vijavyo.
Post a Comment