Pamela Chilongola
WATU
wanne zaidi wamekamatwa na polisi wakiwa na kompyuta na meza zilizoporwa
katika Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Usharika wa
Mbagala, Dar es Salaam.Kukamatwa kwa watu hao kunafanya idadi ya
waliokamatwa kutokana na vurugu zilizotokea Ijumaa wiki iliyopita
kufikia 126.
Vurugu
hizo zilisababishwa na watu wanaodaiwa kuwa waumini wa dini ya Kiislamu
kuvamia Kituo cha Polisi Maturubai wakitaka wapewe mtoto aliyedaiwa
kudhalilisha kitabu kitakatifu cha Quran kwa kukojolea.
Mtoto
huyo wa miaka 14, anadaiwa kukojolea Msahafu alipokuwa akibishana na
mwenzake kuwa endapo angefanya kitendo hicho, angegeuka nyoka.
Vurugu hizo zilisambaa kwa baadhi ya watu kuharibu mali, kupora na kuchoma moto baadhi ya makanisa na kuharibu magari.
Kamanda
wa Polisi wa Mkoa wa Temeke, David Misime alisema jana kwamba watu hao
wanne wamekamatwa wakiwa na seti ya kompyuta na meza za kanisani
zilizoibwa katika Kanisa hilo la KKKT... “Wamefikishwa katika Kituo
kidogo cha Polisi Maturubai.”
Kamanda
Misime alisema watu hao wameunganishwa na wengine 122 waliokamatwa awali
wakihusishwa na vurugu hizo kati yao, 36 wakituhumiwa kuchoma makanisa
wakati 86 walikamatwa kwa kosa la kufanya fujo.
Alipotembelea
makanisa yaliyoharibiwa na juzi akizungumza katika kilele cha
kumbukumbu ya miaka 13 ya kifo cha Baba wa Taifa, Mwalimu Julius
Nyerere, Rais Jakaya Kikwete aliagiza hatua kali zichukuliwe kwa wote
waliohusika na uharibifu huo.
Rais pia alionya tabia ya wananchi kuchukua hatua kwa jazba na kwamba hali hiyo ikiachwa amani inaweza kutoweka.
Aliwataka Watanzania kutafakari kabla ya kuchukua uamuzi wa kufanya ghasia au uharibifu.
Viongozi wa Taasisi za kidini, wanasiasa na watu wa kada mbalimbali walilaani vurugu hizo wakisema hazikuwa na tija.
Katika
vurugu hizo, makanisa yaliyoharibiwa ni la Katoliki la Kristo Mfalme la
Mbagala Rangi Tatu, Anglikana ambalo lipo Mbagala Kizuiani, Agape
lililopo Kibonde Maji, Wasabato la Kizuiani, KKKT Ushirika wa Mbagala na
TAG Shimo la Mchanga.
Kamanda
Misime alisema kuwa ofisi yake ilikuwa ikiandaa hati za mashtaka na
kuanzia leo wahusika wanatarajiwa kufikishwa mahakamani.
“Tulikuwa
katika mkutano wa kuwaandalia kila mmoja hati yake ya mashtaka na
wakati wowote kuanzia kesho (leo) tutawafikisha mahakamani kujibu
mashtaka yao,” alisema Kamanda Misime.
Post a Comment