Zambia, wakiwa ugenini Kampala, waliweza kuwafunga wenyeji wao Uganda magoli 9-8 kupitia mikwaju ya penalti, na kujiweka katika nafasi nzuri ya kuutetea ubingwa wao, katika fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika mwaka 2013, kufanyika nchini Afrika Kusini, mwezi Januari. Mikwaju 20 ya penalti ilihitajika kubainisha ni nani mshindi na aliyeshindwa, kufuatia Uganda kutangulia bao 1-0 katika mechi ya mjini Kampala.
Patrick Ochan alikosa kuusindikiza mpira wavuni kupitia mikwaju hiyo ya penalti, na wachezaji wa Uganda walikosa kuitumia nafasi yao vizuri ya kuongoza katika mchezo, na hata pia katika mikwaju hiyo ya penalti, kufuatia Zambia kushindwa kutumbukiza wavuni mkwaju wa mapema wa penalti.
Uganda walikuwa wamejiweka katika nafasi nzuri, hasa baada ya kukumbuka kwamba mjini Ndola walishindwa bao 1-0, na katika mchezo wa Jumamosi, Geoffrey Massa aliwawezesha The Cranes kuongoza kwa kufunga bao katika dakika ya 27.
Lakini licha ya juhudi kubwa, bao la pili katika muda wa dakika 90 halikuwezekana kwa Uganda, wakiongozwa na kocha kutoka Uskochi, Bobby Willimason, na kushangiliwa mno na mashabiki wengi wa nyumbani. Kipa wa Zambia Kennedy Mweene alionyesha uhodari wake na kuiokoa timu yake kutoka kwa mikwaju hatari.
Mara tu baada ya dakika 90 kumalizika na mchezo kuingia katika mikwaju ya penalti, nahodha Chris Katongo, na ambaye aliiwezesha timu yake kuwa mabingwa wa Kombe la Mataifa ya Afrika, alishindwa kupata bao, baada ya kipa wa Uganda, Denis Onyango, kuzuia mkwaju huo kutoka kwa nahodha wa Zambia.
Zambia iliibuka mshindi wa mashindano ya mwaka huu ya Kombe la Mataifa ya Afrika, baada ya kuishinda Ivory Coast kupitia mikwaju ya penalti, katika fainali ya Libreville, nchini Gabon.
Uganda ilikuwa nusra ishiriki katika fainali zilizopita, lakini walishindwa kupata ushindi katika mechi yao ya mwisho ya kufuzu, licha ya kwamba walikuwa uwanja wa nyumbani. Mara ya mwisho kwa Uganda kushiriki katika mashindano hayo ilikuwa ni mwaka 1978, walipomaliza katika nafasi ya pili.
Katika matokeo mengine ya Jumamosi, Ghana na Mali, na ambayo ni mataifa mawili yaliyofika nusu fainali katika mashindano yaliyopita, yalijihakikishia nafasi ya kufika Afrika Kusini mwaka ujao.
Chanzo: BBC
Post a Comment