Ndugu zangu,
Leo ni siku ya Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere. Asubuhi hii hapa Iringa najiandaa kwenda kwenye mjadala ulioandaliwa na Kigoda Cha Mwalimu pale Chuo Kikuu cha Mkwawa. Hapo kuna mada yenye kuhusisha suala la Muungano kwenye uandikaji wa Katiba Mpya. Nimeambiwa, kuwa kutakuwa na wazungumzaji mahiri, akina Zitto Kabwe, January Makamba na wengine.
Hawa ni vijana pia. Nitapenda sana kwenda kuwasikiliza na kujifunza. Lakini, tunapozungumzia Muungano kwenye kuandika Katiba mpya inahusu pia mradi mkubwa wa Ujenzi wa Umoja wa Kitaifa ambao Mwalimu Nyerere aliuanzisha, aliusimamia, hata hivyo, tunaona sasa unavyoporomoka na kuliacha taifa letu mashakani. Inahusu Mradi wa Ujenzi wa Umoja wa Kitaifa. Mwalimu alijenga misingi imara ya Ujenzi wa Umoja Wa Kitaifa ( Nation Building).
Kuijenga jamii ya Watanzania yenye kuamini kwenye ukweli kuwa sisi sote ni ndugu. Kwamba Nchi yetu haina dini. Yenye kupiga vita ubaguzi wa aina zote, iwe wa rangi, kabila au dini. Ilimchukua Mwalimu na taifa letu miaka mingi sana kuijenga misingi hiyo iliyowawezesha pia Watanzania kuwa na mioyo ya uzalendo kwa Taifa lao.
Tunaona sasa, kazi hiyo iliyochukua miaka mingi, kutokana na ubinafsi na uroho wa madaraka ya baadhi ya wanasiasa wetu, wanapelekea kubomoka kwa misingi hiyo na kuliacha taifa letu kwenye hatari ya kuangamia. Ndio, msingi wake ni ubaguzi wa kisiasa unaotokana na ubinafsi na tamaa ya mali kwa baadhi ya tuliowapa dhamana za kufanya maamuzi makubwa kwa niaba yetu.
Ni hali ya baadhi ya tuliowapa dhamana za uongozi kuishiwa chembe chembe za uzalendo; mapenzi kwa nchi yao.Ni watu wenye kulinda maslahi yao na ya wanaowazunguka. Wako tayari hata kutumia mbinu za Umafia kutimiza malengo yao. Watanzania wengi sasa wanaopoteza moyo wa uzalendo kwa nchi yao.
Kuna hata wenye kufikia kutamka; 'Nchi hii ina wenyewe'. Kuna anayetamka hilo kwa lengo la kumtishia mwenzake au kulazimisha kitu fulani kifanyike. Lakini, kuna wenye kutamka hivyo kuashiria kukata tamaa. Kuwa hata wafanye nini, hakuna anayewasikiliza ama kuwajali.
Hizi si dalili njema kwa taifa. Kuna wanaoiba mali ya umma mchana wa jua kali. Hakuna anayewagusa. Ukiuliza utajibiwa; “Ah! Nchi ina wenyewe!”. Kwamba kuna baadhi yetu hawajisikii kuguswa na nchi hii, hawajisikii kuwa na nguvu ya kupiga vita maovu yanayotusumbua. Baadhi yetu wameanza kupungukiwa na mapenzi na nchi yao.
Ni hatari. Tuna lazima ya kuwa na ujasiri wa kupigania maslahi ya nchi yetu. Ni heri kufa kwa kupigwa risasi kuliko fedheha ya kufa kwa kuumwa na mbu wa Malaria katika nchi ambayo ina rasilimali za kutuwezesha kujenga uwezo wa kuangamiza malaria.
Lakini, tunakubali wachache miongoni mwetu wahujumu rasilimali zetu. Juni 16, 2004 nilipata kuandika hili kwenye gazeti la Majira; kuwa Tanzania ina vyote, kasoro Watanzania. Niliandika; kuwa Tanzania ni nchi nzuri sana. Ni nchi ya kujivunia. Kwamba Tanzania ni nchi kubwa sana kwa eneo.
Ni nchi yenye rasilimali nyingi; ardhi yenye rutuba, mito, maziwa, milima, mabonde, bahari na vivutio vingi vya asili. Hata hivyo, Tanzania ni moja ya nchi masikini sana duniani. Kwa nini? Ndio, kikubwa kinachokosekana Tanzania ni Watanzania.
Tanzania tunayoijenga sasa ni mkusanyiko tu wa watu wa makundi mbali mbali wenye kwenda kwa staili ya 'kila mtu na lwake'. idadi ya Watanzania wenye uzalendo na mapenzi kwa nchi yao inazidi kupungua. Ubinafsi umekithiri, na ubinafsi mbaya zaidi ni ule wenye kufanywa na viongozi.
Na hilo ni Neno la Leo.
Maggid Mjengwa,
Iringa,
0788 111 765
chanzo: Maggid Blog
Post a Comment