Aliyekuwa
Rais wa Shirikisho la Ngumi za Ridhaa Tanzania (BFT), Alhaj Shaban
Mintanga, akiwa Mahakamani leo, wakati akisubiri hatima ya kesi yake.
***************************************
Na Mwandishi Wetu, jijini Dar
BAADA ya kusota kwa muda mrefu
hatimaye sasa Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam, imemwachia huru
aliyekuwa Rais wa Shirikisho la Ngumi za Ridhaa Tanzania (BFT), Alhaj
Shaban Mintanga, aliyekuwa akikabiliwa na kesi ya kusafirisha dawa za
kulevya nchini Mauritius baada kumuona hana kesi ya kujibu.
Alhaj Mintanga, hadi kuachiwa leo,
alikuwa akisota Gereza la Ukonga kwa takribani miaka minne, kabla ya
kesi yake kutolewa hukumu.
Uamuzi huo umetolewa jana na Jaji Dk.
Fauz Twaib na kusababisha mtuhumiwa huyo aliyekuwa akitetewa na
mawakili maarufu wa kujitegemea nchini, Jerome Msemwa na Yasin Memba,
kurejea uraiani na kuungana na familia yake.
Akitoa uamuzi huo, Jaji Dk.Twaib
alisema, ameisikiliza kesi hiyo tangu ilipohamishiwa mahakamani hapo
mwaka juzi, ikitokea Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, ambako upande wa
Jamhuri ili kuthibitisha kesi yao, waliweza kuleta mashahidi wanne na vielelezo.
Dk. Twaib alisema, baada ya kupitia
kwa kina vielelezo na ushahidi uliotolewa na mashahidi hao wa upande wa
Jamhuri, imebaini ni havifu na umeshindwa kuishawishi mahakama imuone
Mintanga ana kesi ya kujibu na hivyo inamwachilia huru.
Jaji Dk.Twaib, akiuchambua ushahidi
huo, alisema kwa mujibu wa cheti kilichotolewa na Tume ya Kudhibiti Dawa
za Kulevya Tanzania na ambacho kilikuwa kimesainiwa na Mkuu wa tume
hiyo, Christopher Shekiondo, kinaonesha dawa za kulevya alizokuwa
akituhumiwa Mintanga kuzisafirisha kwenda Mauritius, zina uzito wa kilo
4.9 na cheti kilichotolewa na Interpol, kinaonesha zilikuwa na uzito wa
kilo 6.
“Kwanza mahakama hii imejiuliza ni
Shekiondo ndiye aliyethibitisha dawa zile aina ya Heroin zina uzito huo
ambao unatofautiana na uzito wa ulitolewa na Interpol, mahakama
imejiuliza ni kwanini basi upande wa Jamhuri umeshindwa kumleta
mahakamani hapa Shekiondo ambaye anaishi Dar es Salaam, ili aweze kuja
kuthibitisha kuwa ni yeye ndiye aliyetoa cheti hicho, kinachoonyesha
uzito huo na kama kweli aliziona dawa hizo kwa zilizokamatwa kwa macho
na kisha akazipima na kutoa hati ile.
Kwani kuna baadhi ya mashahidi
waliieleza mahakama kuwa, Shekiondo licha kutoa cheti kile cha kuonyesha
thamani ya dawa zile, lakini hakuwahi kuziona kwa macho dawa hizo,”
alihoji Jaji Dk.Twaib.
Jaji huyo alisema, hata hivyo
ushahidi wa mashahidi hao, umekuwa ukipingana, kwani mshitakiwa alikuwa
anakabiliwa na kosa la kusafirisha dawa za kulevya, lakini shahidi wa
nne ambaye ni ofisa wa Jeshi la Polisi, Charles Ulaya, aliiambia
mahakama kuwa, Mintanga alipaswa kushitakiwa kwa kosa kula njama tu na
siyo kusafirisha dawa hizo.
“Hata kama hivyo ndivyo kama
alivyoeleza Ulaya, lakini mahakama hii imeona pia upande wa Jamhuri
umeshindwa kulithibitisha kosa hilo la kula njama, kwani wameshindwa
kuleta ushahidi unaoonesha Mintanga na wenzake hao walikaa wapi, lini,
saa ngapi na wakapanga njama za kusafirisha dawa hizo haramu aina ya
Heroin na kwa sababu hiyo, mahakama hii inamwachilia huru mshitakiwa,
kwa sababu imemuona hana kesi ya kujibu,” alisema Jaji Dk.Twaib.
Aidha, Jaji huyo alisema, karibu
mashahidi wote walikuwa wakilitaja jina la mtu mmoja aitwaye (Michael),
ambaye hakuwepo mahakamani na Charles Ulaya ambaye ndiye alikuwa
akipeleleza kesi hiyo, alisema jina la Michael walipewa na Interpool na
siyo jina la Mintanga katika sakata hilo la kusafirisha dawa za kulevya, ambalo mwisho wake lilisababisha Mintanga kufunguliwa kesi hiyo mahakamani hapo.
Jaji huyo akipangua hoja ya mawakili
wa Jamhuri, iliyodai kuwa, namba ya simu ya Mintanga ndiyo iliyotumika
kufanyia ‘booking’ kwenye kampuni za usafirishaji kwa njia ya ndege,
alisema, baada ya kupitia vielelezo, amebaini ile namba ya simu ni mali
ya ofisi ya BFT, na ndiyo maana namba hiyo ipo kwenye ‘headpaper’ za
shirikisho hilo na kwamba, mfanyakazi yoyote wa shirikisho hilo anaweza
kuitumia, hivyo simu ile siyo mali ya Mintanga binafsi ni mali ya
shirikisho.
Post a Comment