KUFIWA NA MUME/MKE
Jambo la kwanza linalohuzunisha zaidi ambalo lina
kiwango cha asilimia 100 ni mtu kufiwa na mke au mume. Rekodi
zinaonesha kuwa, watu wanaofiwa na wapenzi wao huwa na huzuni kubwa kiasi cha
kutishia maisha yao.
Msongo wa mawazo, mauzauza ni mambo ambayo yanatajwa
kusababisha vifo vya ghafla na vya muda mfupi kwa watu waliofiwa na waume/wake
zao, huku sababu ya vifo hivyo ikibaki kuwa ni msongo wa mawazo
(stress).
Licha ya ukweli kwamba kufiwa mume/mke ni jambo zito
lakini, huzuni inapokuwa ya kudumu kiasi cha kutishia maisha ya mtu,
suala la uzembe wa kufikiri huchukua
nafasi.
Hivyo, ili mtu aweze kuepukana na matatizo
yanayotokana na kufiwa ni lazima afuate muongozo ufuatao ambao utamsaidia
kuipunguza au kuiondoa huzuni hiyo ambayo ni mbaya kuliko nyingine zote
duniani.
Kwanza, ni
kukubaliana na ukweli kwamba mwenza amefariki na hatarudi, kulia na kuhuzunika
hakusaidii. Pili ni kuziondoa taratibu kumbukumbu zote zinazokuja na kutawala
mawazo kuhusu mkeo/mumeo aliyekufa.
Usiyazamishe mawazo kwenye tukio hilo, ukiona kuwaza
kunajitokeza ni bora kupuuza mawazo hayo kwa kutoyapa nafasi ya kukutawala.
Usipende kukaa peke yako kwa muda mrefu. Usiangalie picha na kutembelea kaburi
la marehemu mara kwa mara bila kuwa na sababu za msingi.
Usivute taswira ya maisha mliyokuwa mkiishi zamani.
Kaa karibu na watu uwapendao, tembelea sehemu zenye kuvutia. Epuka kuzungumzia
mambo ya marehemu wako. Badili mazingira ya chumba mlichokuwa mkilala, kuwa bize
na majukumu yako na andaa mipango ya kumtafuta mwenza mpya.
TALAKA
Suala la kutalikiana linahuzunisha watu kwa asilimia
73, wengi kati ya wanaokumbwa na kadhia hii wanatajwa kuwa ni wanawake, ambao
kwa nchi za dunia ya tatu ndiyo wanaoondolewa kwenye himaya zao za ndoa kwa vile
wanaume ni watumwa wa mfumo dume. Hata hivyo imebainika kuwa wanaoumia zaidi ni
wale wanaoachwa bila kuwa na makosa ya msingi (haibagui wanaume au
wanawake).
Mwanamke au mwanaume aliyetendwa,
hukumbwa na msongo wa mawazo, hasa anapofikiria sababu dhaifu za kuachwa kwake
na pengine kulinganisha kuachwa na wema aliomtendea mwenzake wakati wakiishi
pamoja. Kwa mujibu wa uchunguzi, watu wanaohangaika na mawazo ya kuachwa ni wale
wanaodhani wamedhalilika (Inferiority complex) kwa kuachwa kwao. Mara nyingi
huwa ni watu wa kutojiamini juu ya kuweza kuishi maisha ya upweke na wakati
mwingine kudhani jamii inawacheka.
Ifahamike kwamba kuachana si kashfa, mtu anayeachwa
anatakiwa kujiamini na kuishi kwa wema ili kuiaminisha jamii kuhusu tabia yake
njema na kuwafanya watu waone kuwa mhusika hakustahili
kuachwa.
Aliyeachwa lazima ajitume kufanya kazi kwa
bidii na apange mipango yake mipya ya kimaisha, lengo likiwa ni
kuonesha uwezo wake wa kuishi peke yake. Asijenge chuki kwa mwenzake, asipange
kulipa kisasi aepuke kuchunguza mwenendo wa mwenziwe, kukutana au kuwasiliana
naye. Aishi karibu na rafiki, watoto au ndugu zake, awapende na
aombe ushauri kwao mahali anapoona anakwama, azuie mawazo ya
kuachwa.
MIGOGORO YA NDOA
Watu ambao hawaishi kwa amani kwenye ndoa zao ni
wepesi wa kupatwa na msongo wa mawazo. Ndoa zenye wanaume/ wanawake
wasaliti zinahuzunisha wengi. Lakini ushauri wa kitaalamu unaotolewa
kuhusu jambo hili ni kila mwanandoa kumtambua mwenzake kitabia na anapoona
hakuna ulinganifu amchukulie mwenzie kama mgonjwa mwenye kuhitaji tiba na wala
si mtesaji.
Haifai kumfumania mwezako na kuanza kuwaza na kulia
badala ya kutafuta ufumbuzi au kwa lugha nyingine tiba. Ni vema kila tatizo
limalizwe kwa mwafaka, kasoro za mume au mke zisihifadhiwe kifuani na kupewa
muda wa kuumiza akili.
Viongozi wa dini, ndugu, wazee, rafiki,
wanaweza kusaidia kujenga nyufa za ndoa. Pale inapothibitika kwa ushahidi
kuwa mwanaume/mwanamke hawezi kujirekebisha hakuna njia salama ya muumizwaji
zaidi ya kuvunja ndoa au uhusiano wake na huyo mwanaume/mwanamke. Haipendezi
kuzidisha kiwango cha uvumilivu kwa vile madhara yake huwa ni
makubwa.
KUFUNGWA JELA
Maisha ya gerezani yanaumiza. Wafungwa
wengi hasa wa magereza yaliyopo ulimwengu wa tatu, hali za wafungwa huwa ni
mbaya. Wengi hufariki kifungoni au muda mfupi baada ya kumaliza. Hii inatokana
na magonjwa ambayo hutokea kwa sababu ya kushindwa kumudu mazingira na wakati
mwingine kutokukabiliana na matokeo ya hukumu, jambo ambalo huwafanya wafungwa
wengi kuwa na sononi zisizo isha. Hivyo ili kukabiliana na huzuni ya kufungwa
lazima mfungwa mwenyewe akubaliane kwanza na matokeo.
Jambo la pili ni kuacha kushindana na mshtaki wako
kwa kutumia akili, usikaribishe mjadala wa mawazo kwenye akili yako, chukulia
kwamba hiyo ni bahati mbaya ya maisha yako sawa na ajali. Hesabu kuwa hayo ni
mapito na ipo siku utatoka ukiwa mshindi na ukweli utajulikana.
Nelson Mandela alipofungwa alituliza mawazo na
hatimaye alitoka na kuwa rais wa nchi na leo ukweli wa kuonewa kwake kila mtu
kaufahamu. Ushauri mwingine ni kuzidisha upendo kwa wenzako, kuwa mwema, ridhika
na upatacho na wakati mwingine tumaini siku njema kwa kuiambia nafsi yako kuwa,
maisha ya gerezani yatapita au kama kifungo ni cha maisha, huna budi kukubali
kuishi kama mfungwa.
KIFO CHA
NDUGU WA KARIBU
Anapofariki baba, mama, kaka, dada, mtoto wako
huzuni hutamalaki. Lakini ni vema ukarejea sehemu ya kwanza kwa masaada zaidi.
Ila kwa nyongeza usiwe mtu wa kulinganisha matokeo ya maisha yako ya uyatima na
yale yaliyokuwepo wakati wazazi.
Kwa mfano usidhani unateseka kwa
sababu wazazi wako hawapo (wamekufa), inawezekana hata wangekuwepo ungeteseka
vile vile. Pambana na maisha wewe kama wewe hatimaye utashinda. Kumbuka kadiri
unavyolia ndivyo unavyozidi kujitesa na kujisogeza kwenye hali mbaya na pengine
kufa mapema.
Hebu fikiria wangapi wamefiwa na wazazi wao, lakini
wanaishi leo maisha ya raha, kwa nini wewe usiweze. Au ni wangapi walifiwa na
watoto na leo wamepata wengine wazuri.. Kumbuka kupenda kilichokufa ni kukinai
kilicho hai na kutopenda kijacho. Hivyo kama unampenda zaidi mtoto aliyekufa
sina shaka utamdharau uliyenaye na upo uwezekano hata usipate mwingine kwani
mawazo yako yanaweza kuharibu afya yako na kukufanya usishike mimba maisha yako
yote.
KUUGUA AU KUJERUHIWA
Watu wengi wanapojeruhiwa hasa vibaya au kupatwa na
magonjwa sugu yanayotajwa kuwa hayana tiba hufadhaika sana. Mgonjwa kama kansa,
kisukari, ukimwi, BP yamewahuzunisha wengi, hii inatokana na hofu ya kufa,
ingawa ukweli unabaki kuwa kifo hakina ushirika na magonjwa hayo tu kwani kuna
wanaokufa bila kuugua magonjwa hayo.
Jambo kubwa la kufanya ni kuondoa hofu kwa kuchukua
mifano ya watu ambao wameishi/wanaishi kwa muda mrefu wakiwa na magonjwa hayo,
lakini hawajafa. Usijifananishe na waliokufa mapema kwani inawezekana walikuwa
na hofu ndiyo maana wakafa. Hofu ndiyo inayotajwa kuua watu wengi kuliko hata
magonjwa yenyewe. Acha kufikiria mawazo ya kufa, usikate tamaa,
endelea kufanya mambo yako kama kawaida na uwe karibu na watu wa kukufariji si
wa kukuvunja moyo.
Usijihukumu kuwa ni mkosa mbele ya jamii na usione
kama umeonewa na Mungu. Tembelea wagonjwa wengine hospitali, huko utaona wenye
shida zaidi yako, hiyo itakupa unafuu wa kubeba udhaifu wako. Kwa wale waliopata
ajali ni vema wakakubaliana na matokeo, wakatulia na kuwatembelea watu wenye
ulemavu ili kupata msaada wa kimawazo na wakati mwingine kufanya ibada ya kuomba
wapewe uvumilivu.
Ifahamike kuwa, ulimwenguni kuna
walemavu wengi ambao wana maisha mazuri kuliko hata wazima, hivyo basi kuwa
kilema haimaanishi kuwa umefikia mwisho wa maisha.
NDOA
Mazingira ya ndoa hasa yanapokuwa magumu tofauti na
mategemeo ya awali hutia huzuni. Pesa inapokosekana, mke/mume anapokuwa
haeleweki, ndugu na jamaa wanapokuwa na tabia mbaya zinazokwenda kinyume na
misingi ya ndoa ni mambo yanayotia simanzi. Lakini pamoja na hayo kukosekana kwa
mtoto ni jambo linalowafadhaisha watu wengi.
Namna ya kwanza ya kufanya ni kwa wanandoa wenyewe
kuondoa mikwaruzano baina yao, hili likifanyika litawapa uwezo wa kukabiliana na
matokeo yote mabaya na kupata ushindi, lakini pia wanandoa wanaopatana ni rahisi
kufarijiana katika shida kuliko wenye migogoro.
Ni jukumu la wanandoa kukuza uhusiano
na upendo ili kutiana moyo nyakati za shida. Kuepuka maneno ya kusikia na wakati
mwingine kutozingatia kejeli za watu wa pembeni wanaobeza maisha yao ya ndoa.
Kuwa na imani kwamba nyakati za kufanikiwa kwa kupata mtoto zipo na hakuna
kukata tamaa kwa kuangalia muda mlioishi kwenye ndoa.
Lakini hata kwa wale ambao bado
hawajaolewa nao wasihuzunike, kwani mara nyingi ndoa hutengenezwa na watu
wenyewe kupitia wapenzi ambao uchunguzi unaonyesha kuwa asilimia kubwa ya
wanaotaka ndoa wana wapenzi.
KUFUKUZWA KAZI
Watu wengi huchanganyikiwa au hushindwa kumudu
maisha muda mfupi baada ya kufukuzwa kazi. Hii inatokana na vyanzo vya mapato
kukoma na pengine heshima ndani ya jamii kupungua. Jambo kubwa la kufanya baada
ya kutimuliwa kazi ni kutulia. Kama ilivyo kwa vifungu vingine ni vema mtu
aliyefukuzwa kazi akawa karibu na marafiki sahihi ambao watamshauri na kumkutia
moyo.
Aliyefukuzwa kazi hatakiwi kujifungia ndani na
kuwaza. Jukumu la kwanza kabisa ni kupunguza matumizi, kutafuta vyanzo mbadala
vya kuingiza kipato kama kufanya kazi za ‘party time’ na
kadhalika.
Kuanza kutafua ajira mpya kwa kupitia watu wako wa
karibu uliokuwa nao kazini ni jambo la muhimu. Usikimbilie kurudi kijijini,
kwani huko unaweza usimudu mazingira ya kimaisha. Omba msaada kwa ndugu pale
unapoona mkwamo. Acha anasa na ulevi kwani utakuingiza kwenye matumizi makubwa
pesa yasiyostahili kwa wakati huo na wakati mwingine kukuharibu fikra.
Kuwa mwaminifu na usimweleze kila mtu shida zako.
Epuka ushawishi wa kimakundi. Itafute furaha kila wakati kwa kusikiliza muziki
ili kuifanya akili iwe imara katika kukupa majibu ya nini cha kufanya baada ya
kufukuzwa kazi. Maisha yanawezekana pia bila ajira kwani kuna wengi wanaishi
bila kazi za viwandani. Kama kuna mafao uliyopewa baada ya kuondolewa kazini ni
vema ukayatumia vema, ili yakusaidie wakati ukitafuta ajira
mpya.
SULUHU BAINA YA WANA NDOA
Wapenzi na hasa wanandoa wanapokosana na mmoja kati
yao akawa hataki suluhu, yule anayekataliwa huingia katika msongo mkubwa wa
mawazo. Mawazo hutawala juu ya kufikia makubaliano na yule aliyempenda, hangaiko
la moyo hutikisa mwili kiasi cha kutoweza kula wala kulala, hatimaye mtu hupata
ugonjwa wa moyo na baadaye kupoteza maisha.
Inashauri kuwa mkishahitilafiana na mpenzi wako,
mtafute umuombe radhi, akikataa washirikishe ndugu au rafiki wa karibu
anayesikilizwa na mpenzi wako ili akusaidie kutafuta suluhu. Wazazi na wazee ni
budi wakapewa nafasi pia.
Unapoomba msamaha usilazimishe sana kusamehewa,
kufanya hivyo kunaweza kumpa kiburi mpenzi wako na kukataa kukusamehe kwa kujua
huna pa kwenda na kwamba kukuacha kwake kunakuumiza. Suluhu inapokosekana
unatakiwa kutuliza mawazo kwa kuutumia muda wako wa mapenzi kufanya kazi zako za
kukuingizia kipato.Pendelea kubadilishana mawazo na watu wengine hasa wenye
mafanikio.
KUSTAAFU KAZI
Uchunguzi unaonyesha kuwa, watu wengi hufariki dunia
muda mfupi baada ya kustaafu kazi, hii inatokana na wengi wao kushindwa kumudu
mazingira mapya ya maisha nje ya ajira zao. Kasoro kubwa inayopatikana kwa watu
wa aina hii ni maandalizi mabaya ya kuelekea kustaafu.
Angalia mada kuhusu maisha ya uzeeni iliyopo ndani
ya kitabu hiki ili kufahamu namna ya kustaafu kazi bila madhara. Lakini ni vema
mtu aliyestaafu akatafuta shughuli mbadala itakayomfanya awe ‘bize’, asijiingize
kwenye starehe na matumizi makubwa ya pesa, asikurupuke kufanya biashara na
kuanzisha miradi mpaka ashauriwe, apunguze matumizi ya familia ili asome upya
mfumo wa maisha bila kutegemea mshahara.
KUUGUZA NDUGU
Ni wazi kuwa watu wanapouguza ndugu zao huwa na
huzuni hasa wanapowaona jinsi wanavyohangaika na maumivu. Ni kweli, inatia
simanzi pale unapomuona mjomba, shangazi, mama mkubwa au shemeji yako akiugua,
lakini njia ya kukabiliana na huzuni hiyo ni kutopima kwa kina
namna anavyojisikia mgonjwa wako.
Elekeza nguvu katika kumsaidia, kumpenda kila
anapoonekana kuumia, kuwa naye karibu na kumfariji, usioneshe huzuni mbele ya
mgonjwa kwani kufanya hivyo ni sawa na kumvunja moyo na kumfanya mgonjwa wako
ajisikie vibaya zaidi. Mara nyingi njia sahihi ya kumuuguza mgonjwa si kumuonea
huruma bali ni kumpa faraja na kuamini kuwa atapona.
UJAUZITO
Ujauzito nao unatajwa kuwatia huzuni baadhi ya
wanawake wajawazito. Wanawake wengi huwa na hofu ya kujifungua salama. Njia
sahihi ya kuepuka tatizo hili ni kwa mjamzito mwenyewe kukwepa upweke na afanye
mazoezi. Asikaribishe hofu kwa mambo ya kusikia juu ya mwanamke fulani aliyekufa
wakati akijifungua au kutumia muda mwingi kuwaza namna atakavyoukabili uchungu
wa kuzaa na hata kuhofu kupatwa na kifafa cha mimba na kupoteza maisha.
Wanaume na ndugu hawatakiwi kuwaudhi wajawazito.
Kusikiliza muziki, kuangalia sinema za kufurahisha ni muhimu kwa mjamzito ili
kumuondolea hofu ya kujifungua. Mjamzito hatakiwi kupewa taarifa za mtu
aliyekufa akijifungua au kuogopeshwa kwa maneno kupitia hali aliyonayo. Kwa
mfano “hee, miguu inavimba hii ni hatari sana inawezekana ukapata presha wakati
unajifungua” Maneno haya hayafai kumwambia mjamzito na kama ana dalili mbaya ni
vema apelekwe kwenye tiba kuliko kutishwa.
MATATIZO YA KUJAMIIANA
Hitilafu katika mambo ya kujamiiana
hutia huzuni pia. Wanaume wenye kasoro za kimaumbile na upungufu wa nguvu za
kiume, wanawake wasiohisi tendo hukabiliwa na msogo wa mawazo. Njia pekee ya
kukabiliana na matatizo haya ni kuwaona wataalamu.Haifai kuumia kwa kuwaza namna
ya kuondokana na tatizo la kasoro za kufanya mapenzi wakati tiba
ipo.
Jambo jingine ni kwa wapenzi kuwa
wawazi pale hisia zinapokosekana. Ni lazima kusaidiana kwa kushauriana,
haipendezi kuyafanya mapenzi kuwa kitu cha siri. Kama mwenzio hakutoshelezi, ni
vema kuwekana wazi na kutafuta suluhu ya tatizo kwa kuwashirikisha wataalamu na
baadhi ya wazee ambao kimsingi wanafahamu mambo mengi.
KUISHI NA FAMILIA MPYA
Inashauri kwamba mtu anapoingia kwenye familia mpya
(akiolewa, akiishi na ndugu katika ukoo, baada ya wazazi wake kufariki dunia),
hatakiwi kujihukumu, akwepe kutafsiri atendewayo kama mtu ambaye si ndugu, bali
kwa kila jambo aone anafundishwa na afanye kila awezalo kufuata kanuni na
mazingira mapya.
Mara nyingi kinachowahuzunisha watu wengi wanaoishi
ndani ya familia mpya ni mawazo yao, ambayo huwashawishi kufikiri kila baya
wanalofanyiwa basi linatokana na sababu ya ujane au uyatiwa wao, wasifahamu kuwa
kukoseana ni sehemu ya maisha tu na kinacholeta maana mbaya ni mawazo ya mtu si
tendo lenyewe.
Jambo la msingi zaidi kwa mtu
anayeishi na familia mpya ni kuwa na nidhamu ya hali ya juu, ajitume katika
kufanya majukumu yake ya kimaisha na awe tayari kubadili tabia sawa na walezi
wanavyotaka.
MABADILIKO YA KIBIASHARA
Kushuka kwa biashara, kubadili maeneo na hofu za
kufilisika ni mambo ambayo huwatia simanzi watu katika kufikiri. Inashauriwa
kuwa mtu anayeendesha biashara akiona dalili za biashara yake kushuka anatakiwa
atafute mshauri wa biashara ili apate muongozo mpya.
Hifai kubabaika na kuwaza bila kutafuta kasoro
zinazoporomosha biashara yako. Ni vema kupitia mapato na kubuni mikakati mipya
ya kujenga panapobomoka. Ushauri wa rafiki mzoefu wa kibiashara ni mzuri pia.
Lakini kujifunza mbinu mpya na kukabiliana na changamoto za kibiashara kwa
kusoma masoko upya ni jambo linalotakiwa kufanyiwa kazi na mfanyabiasha yeyote.
Haifai kuishi na wasiwasi wa kufilisika, kwani kufanya hivyo kuna madhara
makubwa kisaikolojia.
KUHAMA NCHI
Unapohama nchi ambayo imeendelea kiuchumi na kuhamia
nchi maskini utafadhaika au unapoambiwa kuwa unakwenda kuishi nje ya nchi
unaweza kuwa na huzuni kwa upande mmoja, kwa mfano kufikiria maisha mapya mbali
na jamii uliyoizoea na mambo kama hayo. Unachotakiwa kufanya ni kutobabaika na
badala yake unachotakiwa kufanya ni kujifunza tamaduni za huko na kuwa tayari
kubadilika na wakati mwingine kuyakubali mabadiliko hayo kama hatua za maisha
yako. Mwisho ni kuwatumia wenyeji wako kama dira na kujitahidi kuwazoea na
kuwafanya rafiki na ndugu zako.
RAFIKI KUFARIKI
Fuata muongozo wa kipengele cha kwanza na cha tano
katika kupata ufumbuzi wa tatizo hili la kufiwa na rafiki yako. Haifai
kusononeka kupita kiasi kwa suala ambalo huwezi kubadili matokeo
yake.
MABADILIKO KAZINI
Ukibadilishwa kazi kutoka kitengo kimoja kwenda
kingine kunaweza kukuhuzunisha, lakini unachotakiwa kufanya ni kuonyesha uwezo
wako kwa kufanya kazi kwa furaha bila kupunguza nguvu, maana inawezekana
ulipopangiwa, bosi wako kaona wewe unafaa au pengine unajaribiwa katika safari
ya kupandishwa cheo.
KUPINGWA NA MKEO/MUMEO
Unapopingwa katika maamuzi yako na mumeo au mkeo
ambaye awali alikuwa hafanyi hivyo unatakiwa kujiangalia mwenyewe mahali
ulipokosea na kuangalia hoja za mwezako kuliko kuumia moyoni kwa kudhani
unadharauliwa. Fanya uchunguzi, kuwa na mazungumzo ya kina na mwenzi wako ujue
sababu ili marekebisho yafanyike haraka.
KUKOPA MKOPO MKUBWA
Watu wengi hushawishika kirahisi kukopa pesa nyingi,
lakini wanapopewa na kuanza kutafakari namna ya kulipa huingiwa na
huzuni, hivyo inashauriwa kuwa kabla ya kukopa mkopaji lazima ashauriwe na
watalaamu namna ya kuutumia mkopo huo, ili aweze kujiamini na kuwa makini na
urejeshaji ambao ndiyo huwatia hofu wakopaji wengi.
UREJESHAJI MKOPO
Unapokuwa umekopa au kuweka reheni kitu chako na
hatimaye tarehe za mwisho za kurejesha zikawa usoni pako wakati ukiwa huna
kitu/pesa, unaweza kubabaika na kuhuzunika. Unachotakiwa kufanya ni kutazama
namna ya kupata pesa za kurejesha hata kwa kuuza vitu vingine visivyokuwa na
umuhimu mkubwa ili kukomboa ulichoweka reheni. Kuwashirikisha ndugu,rafiki na
watalaamu wa masuala ya pesa wakiwemo wakopeshaji ni suala
muhimu.
KUBADILISHWA MAJUKUMU YA KAZI
Watu wengi
hupatwa na huzuni pale wanapobadilishiwa majukumu kazini ikiwemo kuhamishwa
vitengo, huku hofu yao ikiwa katika mapato na kumudu majukumu mapya
waliyopangiwa. Jambo kubwa linalotakiwa kwa mfanyakazi anayehamishwa kitengo ni
kujiamini na kuendelea kufanya kazi kwa nguvu. Kitendo chochote
cha kuvunjika moyo baada ya mabadiliko huweza kumfanya apoteze uwezo wa kufanya
kazi na kujikuta anafanya kazi kwa kiwango cha chini na kuonekana hafai na
hatimaye kufukuzwa kazi.
MTOTO KUONDOKA NYUMBANI
Wazazi wengi huhuzunika pale mtoto ambaye walikuwa wanaishi naye anapofikia uamuzi wa kuondoka kwa sababu za kikazi, kimasomo, kuolewa na hata kujitegemea. Kimsingi huzuni hii ni ya bure kwa vile kukua kwa mtoto ni pamoja na kufikia hatua hizo za kuachana na wazazi na kuishi kama mtu mzima.
Hivyo, wazazi wanachotakiwa kufanya si kuhuzunika
bali ni kuhakikisha kuwa wanampatia mtoto wao silaha za kuwa salama huko aendako
ili aweze kuwasaidia. Ikiwa mtoto anakwenda shule basi ni lazima wazazi
wamuwezeshe kusoma kwa furaha na ikiwa anaanza maisha mapya msaada wa mawazo na
elimu ya maisha mapya ni vema kumpatia.
MATATIZO YA KISHERIA
Watu wengi hukumbwa na huzuni pale wanapokabiliwa na
maatizo ya kisheria, kwa mfano kesi na tuhuma mbalimbali. Hata hivyo uchunguzi
unaonyesha kuwa, huzuni za kupita kiasi zimekuwa chanzo kikuu kinachowafanya
watu washindwe kukabiliana na tatizo lililopo mbele yao, hii inatokana na nguvu
za mwili na ufahamu kuharibiwa na msongo wa mawazo.
Kwa maana hiyo tunapokuwa na tatizo lolote la
kisheria, jambo la kwanza kabisa ni kutulia na kutafakari njia za kumaliza
tatizo hilo kwa ushindi. Tafakari hizo lazima ziambatane na namna ya kupatana na
walalamikaji, kupata watetezi wa kesi na ushauri wa namna ya kuendesha kesi
iliyojitokeza. Si busara kupaniki na kuamua mambo kwa jazba, kufanya hivyo
kumewaponza wengi ambao walikuwa na nafasi ya kushinda matatizo, lakini
walikwama kwa sababu walipoteza umakini kwa jazba.
KUKWAMA KWA MALENGO
Tunaposhindwa kufikia malengo yetu tuliyojiwekea,
kwa mfano kufeli mitihani, kushindwa kuendelea na ujenzi au kufanya hiki na kile
tulichokusudia, mara nyingi hutuingiza kwenye huzuni, lakini kanuni za mafanikio
yoyote duniani zinaanzia katika mkwamo.
Hivyo basi tunapoona tumeshindwa kufikia lengo la
kile tulichotaka kukifanya haimaanishi kuwa hatuwezi, bali tumepungukiwa nguvu
ambazo lazima tuzitafute kutoka katika miili yetu kwa kutumia uwezo na uelewa
wetu ambao ni mkubwa mara 1000 ya tunaotumia kila siku katika maisha
yetu.
Unapokuwa umekwama katika kitu chochote, jiulize
sababu kwanini umeshindwa. Baada ya kupata sababu hizo tafakari
njia na mbinu mpya za kuelekea kwenye ushindi huku ukiamini kuwa mafanikio
yanatokana na juhudi pamoja na kutorudia makosa yaliyoleta mkwamo. Haifai kukata
tamaa, hata kama umekwama mara elfu moja.
Tunapokwama mara kwa mara ni vema tukawashirikisha
watu katika kila jambo tunaloona kuwa linasumbua akili, ushirikishaji huo
unaweza kutusaidia kupata uzoefu kutoka kwa wenzetu ambao pengine wamevuka
vikwazo vikubwa tofauti na hivyo tunavyokabiliana navyo.
Jambo la mwisho la kuzingatia tunapoanza hatua mpya
za kuelekea katika ushindi tusikubali kurudia kosa, kama kufeli kwako mtihani
kulitokana na kutosoma kwa bidii, usirudie kosa hilo ongeza bidii za kusoma au
kama umeshindwa kujenga nyumba kwa sababu ya kuwa na matumizi makubwa ya pesa
usikubali kuendelea na matumizi hayo, badala yake jibane na utimize nia
yako.
MKE KUANZA/KUACHISHWA KAZI
Inaelezwa katika uchunguzi wa kitaalamu kuwa wanaume
wengi huhofia wake zao kuanza kazi, hii inatokana na wivu wa kimapenzi . Wanaume
hudhani kuwa mke anapokwenda kuajiriwa atakuwa na nafasi kubwa ya kushawishiwa
kuanzisha uhusiano mpya na wanaume wengine.
Lakini ukweli ni kwamba huzuni hii mara nyingi huwa
ni ya bure na matokeo yake huzaa wivu ambao husambaratisha ndoa na uhusiano.
Kitu cha msingi kinachotakiwa kufanywa na mwanaume ni kuwa karibu na mkewe
kumjengea hali ya kujiamini na kumtimizia yote anayostahili kama mke, likiwemo
tendo la ndoa na ukaribu ambao mara nyingi unatajwa kuwa tiba kubwa ya
usaliti.
Aidha kwa wale ambao wake zao wanafukuzwa kazi,
jambo la muhimu ni kutiana moyo na kushirikiana kwa ukaribu kutumia muda wa
dhahabu kupata kazi. Hili linatakiwa kwenda sambamba na kujaliana wakati wote wa
tatizo. Hali yoyote ya kumtenga na kumwacha mkiwa ni hatari kwa uhusiano.
Pamoja na hilo endapo kipato cha mwanamke kilikuwa
ni sehemu ya matumizi ya nyumbani basi mume na mke wanawajibu wa kukaa pamoja na
kupanga upya matumizi yao ili kuondoa pato ambalo lilikuwa linatumika kutoka
katika mshahara wa mwanamke ambaye kafutwa kazi.
KUANZA/KUMALIZA SHULE
Wanafunzi wengi wanapopata nafasi ya kuanza shule
kwa hatua yoyote ile hujawa na hofu ya kuweza kukabili mazingira mapya.
Inashauriwa kuwa mwanafunzi anapokwenda kuanza shule lazima awe
tayari kubadilika kufuatana na mazingira na asiwe mtu wa kuogopa changamoto
atakazokutana nazo shule, suala hili limeelezewa kwa kina katika kipengele cha
mwanafunzi na mazingira ya shule ambacho kipo ndani ya kitabu
hiki.
Hata hivyo, wanafunzi ambao wanamaliza shule
wanashauriwa kutohuzunishwa na hilo, badala yake wawe tayari
kujifunza maisha kutoka kwa ndugu wanaoishi nao.
MAISHA KUBADILIKA
Hali ya maisha inapoporomoka huhuzunisha, lakini
kinachotakiwa katika kukabili tatizo hili si huzuni bali kuwa tayari kutazama
kilichochangia kushuka kwa maisha hayo na kukitafutia ufumbuzi wa haraka.
Hata hivyo, watu wengi wanaelezwa kuwa
wamekuwa wahanga wa tatizo la kuporomoka kwa maisha kutokana na ubinafsi kwa
kutokuwa tayari kubadilishana mawazo na watu wengine katika kupata ufumbuzi wa
tatizo na kuhakiki mipango ya maisha yao. Utakuta mtu akipata pesa basi anaamua
mwenyewe kuanza biashara bila hata kupata ushauri kutoka kwa watu, hili ni jambo
baya.
Ifahamike kuwa kubadilika kwa hali ya maisha ni
dalili ya kuwepo kwa makosa makubwa katika mipango ya kimaisha, hivyo basi kila
mtu anayepatwa na tatizo hili anatakiwa kutafuta msaada wa mawazo kutoka kwa
wataalamu au rafiki, ili apate mbinu za haraka za kujinasua, kwani kuhuzinika
peke yake hakufai.
KURUDI KWENYE
MAKAZI YA AWALI
Mtu anapokuwa amehama nyumbani na kwenda kuanzisha
maisha yake sehemu nyingine na baadaye kushindwa na kurudi nyumbani kwa wazazi
au maskani yake ya mwanzo humfanya ahuzunike, lakini kitakachokuwa
kinamhuzunisha si kitendo hicho, bali ni hisia za kudhani kuwa atadharauliwa au
kuchekwa na watu.
Hili linaweza kuwa kweli, lakini huzuni pekee
haisaidii kuondoa tatizo, wakati mwingine mbinu za kijeshi zinaelekeza kuwa
unaposhindwa kusonga mbele na ulipo pakiwa na hatari ya kifo hatua za kurudi
nyuma hustahili kutumika.
Kurudi huku hakupewi maana ya kushindwa, bali
kujipanga katika kushambulia kwa nguvu. Kwa maana hiyo mtu anaposhindwa kuishi
peke yake na akabaini kuwa kuwepo kwake katika maisha mapya ni kifo, kurudi
nyumbani si kosa, kinachotakiwa ni nia ya kujipanga kuelekea katika ushindi
mpya.
USUMBUFU WA
BOSI KAZINI
Usumbufu wa mabosi kazini umekuwa ukiwafanya watu
wengi kufikia hatua ya kuacha kazi, kuhama vituo au kufanya kazi kwa kiwango cha
chini. Hali hii huwapata zaidi wanawake ambao wanafanya kazi na mabosi
wanaowataka kimapenzi. Usumbufu wa kutongozwa sambamba na kitisho cha kufukuzwa
kazi umekuwa ni huzuni kubwa kwa wanawake wengi makazini.
Inaelezwa na wanawake niliokutana nao wakati wa
matayarisho ya kitabu hiki kuwa, kutongozwa na bosi ni kero ambayo haikwepeki
hasa pale hisia za kimapenzi zinapokuwa hazipo kwa mtu husika. Wengi kati ya
wanawake hukiri kufanya mapenzi na mabosi wao si kwa sababu wanawapenda, lakini
kwa lengo la kulinda kazi ambayo huwa hatarini pale maelewano na bosi
yanapoyumba.
Kusema kweli uamuzi wa kuwa mtumwa wa mtu kwa sababu
ya kazi ni aibu kwa binadamu ambaye ameumbwa na uwezo utashi na nguvu za
kukabili matatizo. Njia pekee ya kukabiliana na tatizo hili, kwanza ni
kuwajibika katika majukumu kama mfanyakazi na pili ni kujiamini na kujipenda.
Unapowajibika kama ipasavyo unakuwa na ulinzi
wa kazi yako si tu kwa yule unayemfanyia kazi, bali hata kwako
mwenyewe kwa vile utakuwa na hoja za kujitetea kisheria. Lakini pia kujiamini na
kujipenda ndiyo nguzo ya kukulinda wewe na ushawishi usiokuwa na tija kwako.
Mfanyakazi lazima awe na msimamo wake kuhusu kazi anayoitumikia, ili
asiyumbishwe na kitisho cha kufukuzwa kazi, kwani ajira kwa wachapa kazi zipo
nyingi katika ulimwengu.
Mwisho ni kujipenda. Yaani kuwa mwanadamu mwenye
utashi na kutokuwa tayari kuuza utu kwa sababu ya kazi. Endapo bosi atakuja na
sera za kutongozana kazini, lazima aambiwe uwazi kuwa hilo
haliwezekani na yeye auone msimamo, akitambua hilo hataweza kuleta usumbufu
ambao hatimaye utamkosesha yeye mfanyakazi na kumtia aibu katika jamii. Lakini
kufuata hatua za kisheria ni jambo linalofaa pia.
KUHAMA MAKAZI
Kuhamia katika nyumba mpya kunatajwa kuwatia hofu
pia baadhi ya watu, inaeleza kuwa asilimia 20 ya watu wanaohama makazi yao ya
awali huhuzunika. Hii inatokana na hofu ya kumudu mazingira
mapya.
Watu wengi hushindwa kulala ugenini na
kujikuta wakipoteza furaha kwa kiwango fulani. Inashauriwa kuwa mtu kabla
hajahamia katika mazingira mapya ni vema akazoea taratibu maeneo anayokwenda,
kuwatambua majirani na kusoma tabia zao, lakini zaidi ya yote ni kufuata misingi
yote ya ubinadamu na kujiamini.
KUBADILI DINI
Watu wamekuwa wakibadili dini kwa lengo la kutafuta
amani katika maisha yao kupitia njia ya kumwamini Mungu, lakini uchunguzi
unaonyesha kuwa wengi wao wamekuwa hawapati amani hiyo kutokana na mambo
mawili ambayo ni migogoro ya kifamilia na namna ya kumudu amri za
dini mpya.
Asilimia 18 ya watu wanaobadili dini huhuzunishwa na
mabadiliko hayo kiasi cha kujutia uamuzi wao, huku
idadi yao wakitajwa kurejea katika dini zao za awali au kutaka tamaa ya kiimani
na hivyo kupata madhara ya kisaikolojia.
Hata hivyo sababu za kitaalamu zinazotajwa kuchangia
ukosefu wa amani hiyo ni udhaifu katika maamuzi. Watu wanaobadili dini wengi wao
wamekuwa wakifanya hivyo kwa sababu dhaifu ambazo hutokana na shinikizo la watu
wengi wakiwemo wapenzi au tamaa ya kupata pesa na misaada ya kidini, jambo
ambalo ni hatari.
Inashauriwa kuwa mtu anayetaka kubadili dini lazima
aamue mwenyewe na awe na sababu za msingi zinazodumu si za kimapenzi wala
ushawishi wa kipesa, lakini pia awe tayari kukabiliana na matokeo hasi ya uamuzi
wake, likiwemo suala la kutengwa na ndugu ambao hawatafurahishwa na maamuzi
yake.
Vivyo hivyo, ni busara kuelewa mapema sheria na amri
za dini mpya kabla hujajiunga, hili litasaidia katika kupima uwezo wa kutumikia
kikamilifu kama muumini. Lakini ikitokea umeshindwa kupata amani uliyotaka,
hakuna ubaya kurejea ulipotoka kwa maana ya kujilinda na athari za msongo wa
mawazo utakaoletwa na kadhia za dini mpya.
FAMILIA KUBWA
Wazazi na walezi ambao wana familia kubwa wametajwa
kuwa ni watu wanaosumbuliwa sana na msongo wa mawazo kwa kiwango ha asilimia 15.
Malezi ya familia kubwa ni magumu hivyo walezi wengi hufikia kuona kero na
usumbufu mkubwa hasa nyakati ambazo mahitaji ya familia huwa makubwa kuliko
kipato. Hivyo ili mtu aweze kuepukana na tatizo hili lazima ahakikishe kuwa
anakuwa na familia ndogo ambayo atamudu kuitunza.
Lakini ikiwa ni
lazima kuwa na familia kubwa basi ni vema elimu ya kubana matumizi na uzalishaji
wa pamoja ikatolewa ili kumfanya kila mtu ndani ya familia awajibike katika
kubeba mzigo.
Haifai kuwa na familia kubwa ambayo watu wake
hawazalishi. Kama una watoto ambao wanaweza kulima, kufanya biashara, hakikisha
unawaongoza katika shughuli hizo, usiwaache walale na kula bure. Wafanye watu wa
nyumba yako kuwa msaada kwako pia katika kuendesha gurudumu la
maisha.
chanzo: UjanaTz
Post a Comment