KWA
mara nyengine tena Rais Barack Obama ametajwa kumbwaga Mitt Romney katika
mdahalo wa televisheni, ambao licha ya mada yake kuu kuwa siasa, masuala muhimu
kwa wapiga kura, yaani uchumi na ajira, yalitawala mjadala.
Safari hii,
wachambuzi wanasema kwamba mpira ulikuwa unachezwa uwanjani kwa Rais Obama -
siasa za kimataifa - na hivyo alitumia vizuri ujuzi wake kwenye eneo hilo
kuponda kile kinachoonekana kama uelewa mdogo wa Romney linapohusika suala la
siasa za nje.
"Gavana Romney,
nimefurahi kwamba unatambua kwamba al-Qaida ni tishio kwa sababu miezi michache
iliyopita ulipoulizwa ni kipi kitisho kikubwa duniani kwa Marekani, ulisema
Urusi, ilhali Vita Baridi vilimalizika tangu miaka 20 iliyopita.
Linapokuja suala
la sera za nje, unaonekana kurudisha siasa za miaka ya 1980, kama vile ambavyo
una sera za kijamii za mwaka 1950 na za kiuchumi za mwaka 1920.
Unasema
hupendelei kuigiza kilichotokea Iraq, lakini wiki chache zilizopita ulisema
unafikiria tuongeze wanajeshi zaidi nchini Iraq." Obama alimdhihaki
Romney.
Pakiwa pamebakia
wiki mbili tu kabla ya Siku ya Uchaguzi, Romney aliutumia mdahalo wa jana
kushadidia hoja yake kwamba Obama ameufuja uchumi wa Marekani.
"Ili tuweze
kuendeleza misingi hiyo ya amani, tunahitajika kuwa na nguvu, na hilo linaanza
na uchumi imara hapa kwetu, na bahati mbaya uchumi si imara kiasi
hicho.
Pale rais wa
Iraq- samahani- rais wa Iran, Ahmedinejad, anaposema kwamba deni letu
linatufanya tusiwe tena taifa kubwa, hilo ni jambo la kutisha.
Mkuu wa zamani wa
jeshi, Admirali Mullen, alisema kwamba deni letu ndicho kitisho kikubwa cha
usalama wa taifa. Tumeudhoofisha uchumi wetu." Alisema Romney.
Mchuano
mkali
Wagombea urais wa Marekani wakiwakumbatia wake
zao baada ya mdahalo wa tatu kati yao.
Wakiwa wanachuana
vikali, hakuna hata mmoja kati yao aliyeweza kumtoa mwenzake nje ya ulingo
haraka, wakati wakilumbana kuhusiana na masuala ya Israel, Iran, Urusi, na
ukubwa wa jeshi la Marekani, katika mdahalo huo uliofanyika kwenye Chuo Kikuu
cha Lynn, Boca Raton.
Matokeo ya
uchunguzi wa maoni yaliyotangazwa baada ya mdahalo huo, yamemuonesha Obama
akiongoza, ingawa asilimia 60 ya waliotuma maoni yao kwenye kituo cha CNN,
walisema Gavana Romney ana uwezo wa kuwa amiri jeshi mkuu wa majeshi, akitimiza
jukumu lililowekwa na wasaidizi wake.
CNN imempa Obama
asilimia 8 mbele ya Romney.
Kura ya maoni ya
kituo cha CBS inaonesha kuwa asilimia 53 ya watu wanaamini kuwa Obama alishinda
mdahalo wa jana, ikilinganishwa na asilimia 23 ya Romney, huku asilimia 24
wakisema wametoka suluhu.
Kwa kuwa siasa za
nje ni kipaumbele cha chini katika kampeni iliyojikita kwenye uchumi, bado si
wazi ikiwa mdahalo huu utakuwa na athari gani kwenye kinyang'anyiro hicho cha
urais.
Wachangiaji maoni
kupitia kituo cha CNN, walionekana kugawika juu ya suala ikiwa mdahalo huo
ungeliathiri kura zao hapo tarehe 6 Novemba.
Hata hivyo, picha
hii ya Boca Raton ilikuwa ni moja ya nafasi za mwisho mwisho kabisa kwa wagombea
wote wawili kuwanasihi mamilioni ya wapiga kura waliokuwa wakiifuatilia kupitia
televisheni zao, na ambapo Obama ametajwa kujidhihirisha mtundu zaidi ya
Romney.


Post a Comment