
Vigogo wa Bodi ya Mikopo
********************
Serikali imesema inafikiria kuifumua na kuivunja Bodi ya Mikopo ya Elimu ya Juu (HESLB) kwa kuwa imeshindwa kukidhi matarajio ya serikali pamoja na Watanzania wengi kama ilivyotarajiwa wakati inaanzishwa.
Bodi hiyo licha ya kupewa zaidi ya Sh. trilioni moja tangu ilipoanzishwa mwaka 2005 hadi sasa, lakini imeshindwa kuweka mkazo ili kuhakikisha inawabana watu wote waliopata mikopo walipe madeni yao ili fedha hizo zitumike kuwakopesha wanafunzi wengine wanaozihitaji.
Aidha, kwa kipindi kirefu utendaji wa bodi hiyo umekuwa hauendi sawa sawa na kumekuwa na malalamiko mengi katika utoaji wa mikopo katika vyuo vikuu.
Kaimu Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Selestine Gesimba, alitoa kauli hiyo jana jijini Dar es Salaam mbele ya Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC).
“Kwa sasa idadi ya wanafunzi wanaopata mikopo hapa nchini kwa ajili ya elimu ya juu ni 300,000, lakini hali ipo hivi sasa huko tuendako idadi hiyo ikifikia 500,000 na kuendelea itakuwaje?” Alihoji Gesimba.
Aliambia kamati hiyo kuwa mpaka sasa HESLB imekusanya Sh. bilioni 20 kati ya Sh. bilioni 39 ambazo zinatakiwa kukusanywa na kwamba hayo ni mapungufu makubwa ya kiutendaji.
Gesimba alisema kwa sasa kuna vyuo 50 vya elimu ya juu ambavyo vinahudumiwa na HESLB na kwamba kila mwaka mahitaji yanazidi kuongezeka.
Hata hivyo, Gesimba alisema bajeti ya elimu ya juu inazidi kupungua ingawa idadi ya wahitaji inaongezeka kila mwaka na kwamba hiyo ni moja ya changamoto zinazoikali wizara yake.
Alisema serikali imempa kazi mshauri mwelekezi kwa ajili ya kufanya utafiti kuhusu matatizo katika utoaji wa mikopo na changamoto zake ili aweze kuishauri wizara.
Aliongeza kuwa mtalaamu aliyepewa kazi hiyo tayari amemkabidhi rasimu Waziri wa Wizara hiyo, Dk. Shukuru Kawambwa, na kwamba mpango mzima ukikamilika serikali itapata njia sahihi ya utoaji wa elimu ya juu nchini.
“Huyu mtalaamu atatuambia namna ya kupata vyanzo vya mapato vitakavyosaidia wanafunzi kusoma, namna ya kukusanya mikopo kutoka kwa wanafunzi walimaliza vyuo ambapo walipa mikopo pamoja na utendaji mzima, lakini hayo yakifanyika bodi hii haiwezi kuendelea kuwepo tena,” alisema.
Akizungumzia sekta ya elimu kwa ujumla, Gesima alisema serikali inatarajia kuongeza ada kwa wanafunzi wanaosoma ualimu ngazi ya cheti kutoka Sh. 150,000 hadi Sh. 200,000 kwa mwaka pamoja na kuanza kutoza ada kwa ajili ya usajili wa shule binafsi za msingi na sekondari.
Alisema kwa sasa hakuna gharama yoyote inayotozwa mtu ama taasisi binafsi inapotaka kusajili shule ya msingi pamoja na sekondari na kuongeza kuwa ada ya ukaguzi kwa shule hizo nayo inatarajia kupanda kutoka Sh. 500 kwa mwanafunzi mmoja hadi Sh. 1,000 kwa mwanafunzi.
Chanzo: Nipashe


Post a Comment