Na Bin
Zubeiry Blog
YANGA SC
imeondoka leo alfajiri Dar es Salaam na kikosi cha wachezaji 20 kwenda Arusha
kwa ajili ya mechi yao ya Jumamosi dhidi ya wenyeji JKT Oljoro kwenye Uwanja wa
Sheikh Amri Abeid mjini Arusha.
Wachezaji
waliokwenda Arusha leo ni makipa Yaw Berko, Ally Mustafa ‘Barhez’, mabeki, Oscar
Joshua, Juma Abdul, David Luhende, Stefano Mwasyika, Nadir Haroub ‘Cannavaro’
(Nahodha), Mbuyu Twite na Kelvin Yonda.
Viungo ni
Athumani Iddi ‘Chuji’, Frank Domayo, Rashid Gumbo, Simon Msuva, Haruna
Niyonzima, Nurdin Bakari, Nizar Khalfan, Juma Seif ‘Kijiko’ na washambuliaji
Jerry Tegete, Hamisi Kiiza na Didier Kavumbangu.
Yanga
inakimbilia Arusha mapema ili kuwahia kuzoea hali ya hewa ya huko, wasije kupata
tabu katika mchezo wa Jumamosi.
Mabingwa hao
wa kihistoria wa Ligi Kuu, wanakwenda Arusha wakitoka kuendeleza wimbi la
ushindi jana katika Ligi Kuu, baada ya kuichapa Polisi Morogoro mabao 3-0 kwenye
Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Ushindi huo,
unaifanya Yanga itimize pointi 17, baada ya kucheza mechi tisa na kuendelea
kusimama katika nafasi ya tatu, nyuma ya Azam FC yenye pointi 18, baada ya sare
ya 1-1 na Ruvu Shooting Uwanja wa Chamazi, nje kidogo ya Jiji la Dar es
Salaam.
Hadi
mapumziko jana, Yanga walikuwa mbele kwa mabao 2-0 yaliyotiwa kimiani na
washambuliaji Simon Msuva na Didier Kavumbangu.
Msuva
alikuwa wa kwanza kuwainua vitini mashabiki wa Yanga dakika ya tano kabla ya
dakika moja baadaye, Mrundi Kavumbangu naye kuwapa raha mashabiki wa timu
hiyo.
Yanga
ingekwenda kupumzika ikiwa inaongoza kwa mabao 3-0 kama mkwaju wa penalti wa
Haruna Niyonzima usingegonga mwamba na kurudi uwanjani kabla ya mabeki wa Polisi
kuondosha kwenye hatari.
Refa Alex
Mahagi kutoka Mwanza alitoa penalti hiyo, baada ya Msuva kuangushwa na beki John
Bosco kwenye eneo la hatari wakati anakwenda kufunga.
Kipindi cha
pili Yanga walirudi kwa kasi tena na kuendelea kulishambulia lango la Polisi,
ingawa walipoteza nafasi nyingi na kutumia moja tu, dakika ya 58, mfungaji
Hamisi Kiiza aliyeingia kuchukua nafasi ya Jerry
Tegete.
Matokeo ya
jana yanaziweka karibu mno, Simba inayoongoza kwa pointi zake 19 baada ya
kucheza mechi tisa, Azam na Yanga pale juu, kiasi kwamba ushindani na uhondo wa
ligi hiyo unaongezeka.


Post a Comment