Kamishna wa Polisi Zanzibar,Mussa Ali Mussa
aliwaambia waandishi wa habari kwamba watuhumiwa hao (majina yanahifadhiwa)
walikamatwa sehemu tofauti, mmoja amekamatwa Kisiwa kidogo cha Tumbatu, wa pili
maeneo ya Mjini Unguja,mtuhumiwa wa tatu alikamatwa ofisi za Idara ya Uhamiaji
alikokwenda kushughulikia hati ya kusafiria ili aweze kutoroka hapa
nchini.
Kamishna Mussa alisema watuhumiwa wengine
watatu wamekamatwa Mkoani Tanga ambako walikimbilia kujificha baada ya kufanya
mauaji ya Afisa Polisi Koplo Said Abdulrahman.
“Watu hao walitorokea huko na tunaendelea
kuwahoji…tunawashukuru wananchi kwa ushirikiano wao mkubwa uliotuwezesha
kufanikisha ukamataji huo,tunavishukuru vikundi vya ulinzi shirikishi vilivyo
katika Shehia mbalimbali kwa kuimarisha ulinzi wa maeneo yao katika kipindi
chote cha fujo na vurugu hizo” Alisema Kamishna Mussa.
Kamishna Mussa aliwaambia waandishi wa habari
kuwa Polisi hivi sasa inaendelea kuwahoji Sheikh Farid Hadi na viongozi
wenzake wa Jumuiya ya Uamsho na Mihadhara ya Kiislam ili kufahamu wapi
alipokuwa na kuthibitisha kama kweli alitekwa ama la.
Katika hatua nyengine Polisi imeonya kuchukua
hatua kali dhidi ya wafuasi wa UAMSHO wanaodaiwa kutaka kuvamia kambi za
Polisi,kambi za Majeshi na Ofisi za Serikali ya Mapinduzi.
“Natoa onyo kali kwa wananchi wote kuwa hakuna
mtu yeyote aliye juu ya sheria,Jeshi la Polisi na Vikosi vyote vya ulinzi na
usalama tumejipanga madhubuti kukabiliana na mtu yoyote ama kikundi chochote
kitakachofanya vurugu” Alisema Kamishna Mussa.
Akizungumzia hali ya amani, Kamishna Polisi
alisema kwamba Mji wa Zanzibar ni shwari kwa sasa na wananchi wanaendelea na
shughuli zao kama kawaida.
“Jeshi la Polisi na vyombo vya ulinzi na
usalama vimeimarisha ulinzi,tunaomba wananchi wasiwe na hofu na waendelee kutii
sheria za nchi bila kushurutishwa,waendelee kudumisha amani katika maeneo yao na
pia waendelee kutupatia taarifa za mara kwa mara za hali ilivyo huko
wanakoishi”
Post a Comment