Makamu wa pili wa Rais
Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi akitoa hotuba ya ufungaji wa Mkutano wa siku tano
wa Jumuiya ya Kiafrika ya Utumishi wa Umma na Uongozi AAPAM huko Zanzibar Beach
Resort nje kidgo ya mji wa Zanzibar .
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Idd amesema Viongozi wenye dhamana katika taasisi zao wanapaswa kubadilika kiutendaji na kuhakikisha kuwa utolewaji wa huduma za jamii unafanywa kwa usawa miongoni mwa raia ili kuendana na kasi ya uwajibikaji na utawala bora.
Balozi Seif ameyasema hayo leo alipokuwa akifunga Mkutano wa siku tano wa Jumuiya ya Kiafrika ya Utumishi wa Umma na Uongozi AAPAM uliokuwa ukifanyika katika Ukumbi wa Zanzibar Beach Resort nje kidgo ya mji wa Zanzibar.
Balozi Seif amesema kwa vile wengi wa Washiriki katika mkutano huo ni viongozi wanaohusiana na Taasisi za Usimamizi wa Umma na Utawala bora, ana matumaini kuwa Mkutano huo unaweza kuwa njia muafaka ya kupatikana ufanisi na uwajibikaji katika kutoa huduma za jamii kwa usawa unaokubalika.
Amesema kama Washiriki wa Mkutano huo wa AAPAM watayatekeleza ipasavyo waliyojifunza hapana shaka Bara la Afrika litapiga hatua katika suala zima la Utumishi wa Umma na Uongozi na hatimaye kupatikana kwa maendeleo.
Balozi ameongeza kuwa Mkutano huo umekuja wakati muafaka ambapo dunia kwa sasa inahitaji kuona uwajibikaji katika usimamizi wa huduma za umma na rasilimali watu jambo ambalo ni muhimu kwa maendeleo ya Afrika.
Amesema anaamini kwamba kipindi chote cha siku tano za mkutano kilitoa fursa adhimu kwa Washiriki kujifunza mambo mbalimbali sambamba na kubadilishana uzoefu hivyo wajumbe hao watakuwa wamepata mazingatio na kwenda kuyafnyia kazi katika Taasisi zao.
Aidha amefahamisha kuwa Changamoto zilizoainishwa kuwa kikwazo kwa maendeleo ya Usimamizi wa Huduma za Umma na Uongozi zinapaswa kufanyiwa kazi kwa haraka ili kutimiza malengo ya mkutano.
Katika kuhakikisha kuwa mafanikio ya mkutano huo yanafahamika Balozi amsema njia pekee ni kufanya tathmini ya mara kwa mara kuhusiana na yale ambayo wameondoka nayo katika mkutano huo.
Makamu huyo wa Pili wa Rais aliitumia fursa hiyo kuwaakaribisha Washiriki wa Mkutano huo kufanya ziara za mara kwa mara za kikazi au za kibinafsi ili kujionea vivutio mbalimbali ambavyo Visiwa vya Zanzibar vimejaaliwa.
Akitoa Salamu za shukrani Rais wa AAPAM Abdon Agaw Jok aliishukuru Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kwa maandalizi bora waliyoyafanya jambo ambalo limepelekea ufanisi mkubwa wa Mkutano huo.
Mapema akiwasilisha mada katika Mkutano huo Mwakilishi wa Mtandao wa Vijana Wasomi Afrika Esther Ng’ong’ola aliziomba Nchi wanachama wa Jumuiya hiyo kuendelea kuwaunga mkono Vijana wasomi katika harakati zao za kulikomboa Bara la Afrika kimaendeleo.
Aidha Esther aliongeza kuwa kwa sasa Bara la Afrika limepiga hatua katika suala la Usimamizi wa Huduma za Umma na Utawala bora na kuongeza kuwa viongozi wake wanapaswa wawe na dhamira za kisiasa ili kutekeleza utawala Bora.
Mkutano huo wa Siku tano ambao ulijadili njia za kuimarisha Usimamizi wa Umma na Utawala ulifanyika Zanzibar na kuhudhuriwa na zaidi ya Wajumbe 400 kutoka katika nchi mbalimbali za Afrika ambapo pia uliidhinisha Nchi ya Rwanda kuwa mwenyeji wa Mkutano ambao utafanyika Novemba mwakani mjini Kigali.
Post a Comment