Serikali ya Jamhuri ya
Kidemokrasi ya Congo imetoa wito kwa Umoja wa Mataifa kuichukulia hatua Rwanda,
kwa madai ya kusaidia waasi nchini Congo badala ya kumfuatilia mtu mmoja kama
vile kanali Sultani Makenga.
Waziri wa habari wa
serikali ya Congo amesema hayo siku moja baada ya Umoja wa Mataifa na Marekani
kutangaza vikwazo dhidi ya kiongozi wa waasi wa M23, Jenerali Makenga, vikiwemo
vya usafiri na kukamata mali yake.
Serikali ya Marekani pia
imewazua Wamarekani kujihusisha kwa namna yoyote na Sultan Makenga, ambaye
alikuwa afisa wa ngazi ya cheo cha Jenerali katika jeshi la Jamhuri ya
Kidemokrasi ya Congo.
Hata hivyo haijaeleweka
iwapo hatua ya kukamata mali itakuwa na athari kwani inadhaniwa kuwa Makenga
huenda hana mali ya kiasi cha kumtisha ambayo iko nchini
Marekani.
Taarifa ya Umoja wa
Mataifa, imesema waasi wamekuwa wakipata silaha kinyume na amri ya Umoja wa
Mataifa inayozuia biashara ya silaha kuingia nchini humo.
Taarifa hiyo pia
imemtaja Jenerali Makenga kuhusika na vitendo vya mauaji, ukataji viungo vya
binadamu, ubakaji, utekaji nyara dhidi ya raia na kuwalazimisha watu kuyakimbia
makaazi yao.
Balozi wa Marekani
katika Umoja wa Mataifa, Susan Rice, amesema vikwazo vipya vinaonyesha kuwa
dunia haitavumilia vitendo vya uhalifu vilivyofanyika chini ya amri ya Jenerali
Makenga.
Uasi ulianza mwezi March
wakati wanajeshi waasi walipojitoa kutoka jeshi la Congo na kutwaa miji karibu
na Goma, mji mkuu wa jimbo la Kivu Kaskazini mashariki mwa
Congo.
Maafisa walioasi
walipinga kuhamishiwa katika maeneo mengi ya nchi wakisema wanataka kubakia
katika eneo la mashariki kwa madai ya kuwalinda wananchi wa eneo
hilo.
Pia wanasema wanataka
wakimbizi wanaoishi Rwanda, Uganda na Burundi, kupelekwa katika eneo
hilo.
Umoja wa Mataifa
umezishutumu Rwanda na Uganda kwa kuwaunga mkono waasi, shutuma ambazo nchi zote
mbili zimekana kuhusika.
Post a Comment