HASSAN Hasanoo, Mwenyekiti wa Chama cha Mpira wa Miguu Mkoa wa Pwani, jana alipandishwa kizimbani yeye na wenzake watano kwa tuhuma za kusafirisha bila kibali meno ya tembo yenye thamani ya kwenda China.
Thamani ya meno hayo ya tembo iliyotajwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu mbele ya Hakimu Mkazi, Augustino Mbando, ni ya shilingi 1,185,030,000.
Hassanoo aliyewahi kuiongoza Simba SC kwa mafanikio makubwa, pia anakabiliwa na kesi nyingine ya kusafirisha kontena la shaba bila kibali, kesi hiyo inayo naendelea kusikilizwa katika mahakama hiyo hiyo.
Mbali na Hassanoo, washtakiwa wengine ni Alli Kimwaga, Danstun Mwanga, Godfrey Mwaga, John Mlay na Khalid Fazaldin ambao kwa pamoja wote wanakabiliwa na mashitaka matatu.
Mwendesha Mashitaka wa Serikali Shadrack Kimaro
alidai washitakiwa walikula njama kati ya Septemba mosi na Novemba 20 mwaka huu jijini Dar es Salaam na Hong Kong China ya kujihusisha na biashara ya kusafirisha nyara za Serikali bila leseni.
Kimaro alidai katika kipindi hicho washitakiwa waliongoza kutenda kosa kwa kuandaa, kusimamia na kujiwezesha kifedha kusafirisha vipande 569 vya meno ya tembo vyenye uzito wa kilo 1,330 yenye thamani ya Sh 1,185.030,000 kwenda Hong Kong, China.
Hakimu Mbando alisema washitakiwa hawatakiwi kujibu lolote kwa sababu kuna taratibu bado hazijakamilika ikiwemo hati ya kutoka kwa Mkurugenzi wa Mashika nchini (DPP) hivyo atapanga tarehe ya karibu ambapo watasomewa tena na kujibu.
Kesi hiyo ya uhujumu uchumi itatajwa tena tarehe 28 mwezi huu na washitakiwa wataendelea kusota rumande.


Post a Comment