HOTUBA YA MWENYEKITI WA
WiLDAF KWENYE UZINDUZI WA SIKU 16 ZA KUPINGA UKATILI WA
KIJINSIA
Ukumbi wa Diamond
Jubilee, TAREHE 26/11/2012
Ndugu Mgeni
Rasmi, Naibu Waziri wa Sheria na Katiba,Mheshimiwa,
Angelah
Kairuki,
Mheshimiwa Balozi wa
Ireland, Fionnula Gilsenan
Waheshimiwa wawakilishi
wa Balozi mbalimbali,
Mheshimiwa Mkuu wa Jeshi
la Polisi, IGP Said Mwema,
Wawakilishi wa Mashirika
wahisani,
Ndugu Viongozi Vyama na
Serikali,
Waandishi wa
habari,
Wageni
waalikwa,
Mabibi na
mabwana,
Itifaki
imezingatiwa.
Kwa niaba ya wanachama
wa WiLDAF Tanzania na kwa niaba ya Mtandao wa Kupambana na Ukatili wa Kijinsia
(MKUKI) na Kikosi kazi cha kuandaa maandalizi ya siku 16 za Kupiga Vita ukatili
wa kijinsia, ningependa kuchukua fursa hii kuwakaribisha rasmi kwenye uzinduzi
huu wa Siku 16 za Kupinga Ukatili wa Kijinsia.
Tunatoa shukrani za
pekee kwako mgeni rasmi kwa kuitikia wito wetu wa kuja kujumuika nasi katika
uzinduzi huu na hasa ukizingatia kwamba una majukumu mengi, na nyeti yanayohusu
taifa letu.
Kweli unatuthibitishia
kwamba wewe ni mwanaharakati mwenzetu.
Ndugu mgeni
Rasmi,
Aidha ningependa
kuchukua nafasi hii kipekee kabisa kulishukuru kwa namna ya pekee Shirika la
Msaada la Ireland (Irish Aid), Shirika la Msaada la Marekani USAID, UN
–Women na CONCERN kwa kutupa uwezo wa kiuchumi ili kuweza kuadhimisha siku
hii.
Tunapenda kuchukua
nafasi hii kuwashukuru washiriki wote kwa kujumuika nasi katika uzinduzi wa Siku
hizi 16 za kupinga Ukatili wa Kijinsia kwa mwaka huu 2012.
Ndugu mgeni
rasmi,
Naomba uniruhusu
nikufahamishe kwa ufupi tu kuhusu chimbuko la kampeni ya Siku 16 za Kupinga
Ukatili wa Kijinsia. Kampeni hii ilianzishwa rasmi mnamo mwaka 1991 na Taasisi
ya Kimataifa ya Wanawake katika Uongozi, huko nchini Marekani kwa nia ya
kuamsha ari ya kuzuia na kupambana na ukatili dhidi ya wanawake kwa kuzingatia
haja ya kuleta usawa wa kijinsia.
Ndugu mgeni
rasmi,
Kampeni hii ya Siku 16
za Kupinga Ukatili wa Kijinsia inaanza rasmi tarehe 25 Novemba ambayo
ilichaguliwa na Umoja wa Mataifa mwaka 1999 kuwa ni SIKU YA KIMATAIFA YA KUPINGA
UKATILI DHIDI YA WANAWAKE . Hivyo basi, Umoja wa Mataifa unashauri serikali,
mashirika ya Kimataifa na asasi zisizo za kiserikali kufanya shughuli
zinazolenga kufahamisha jamii juu ya ukatili dhidi ya wanawake.Wanawake duniani
kote wamekuwa wakikumbwa na ukatili ikiwemo kubakwa, vipigo, ukatili majumbani,
ukeketaji na aina mbalimbali za ukatili. Tarehe hii ni ya kihistoria kwani ni
kumbukumbu ya mauaji ya kinyama waliofanyiwa kina dada wa Mirabelle nchini
Dominika mwaka 1960. Wanawake hawa waliuawa kikatili kwa kuwa
walikuwa wanapinga utawala wa kidikteta wa Rais wa nchi ya Dominika (1930-1961)
Rafael Truijilo na kutetea haki katika jamii yao. Wakina dada hawa walifanyiwa
vitendo vingi vya kudhalilishwa utu wao na mwishowe Raisi Rafael Truijilo
aliamua wauawe. Aidha Kampeni hii inahitimishwa tarehe 10 Desemba ambayo ni
siku ya Kimataifa ya TAMKO LA HAKI ZA BINADAMU ikiwa ni ishara ya kuhusisha
ukatili dhidi ya wanawake na haki za binadamu na kutia msisitizo kwamba
ukatili kama huu ni uvunjwaji wa haki za binadamu.
Ndugu mgeni
rasmi,
Kati ya tarehe 25
Novemba na Desemba 10 kuna matukio mbali mbali ya kimataifa kama
ifuatavyo:-
- Tarehe 29 Novemba ni Siku ya
Kimataifa ya Watetezi wa Haki za Wanawake.
- Desemba 1 ni siku ya UKIMWI
duniani.
- Desemba 6 ni siku ya kukumbuka
mauaji ya kikatili ya wanawake wahandisi mjini Montreal,
Canada.
Ndugu mgeni
rasmi,
Kwa kipindi cha tangu
mwaka 1991 inakadiriwa kiasi cha nchi 156 duniani na mashirika zaidi ya 2,000
yanashiriki katika kampeni hii ya siku 16 za Kupinga Ukatili wa Kijinsia kwa
kufanya yafuatayo:-
- Kuhamasisha jamii juu ya ukatili wa
kijinsia na masuala yanayohusu haki za binadamu katika ngazi ya kitaifa, kikanda
na kimataifa.
- Kuimarisha mshikamano wa kupambana
na vitendo vyote vya ukatili dhidi ya wanawake.
- Kuanzisha ushirikiano wa dhati kati
ya wanaharakati wa ndani na nje ya nchi ili kutokomeza ukatili wa
kijinsia.
- Kuandaa jukwaa lenye kuleta fursa
ya kubadilishana mawazo, uzoefu na kuweka mikakati thabiti kwa pamoja ya
kupambana na ukatili wa kijinsia.
- Kuonesha mshikamano wa wanawake
duniani kote na kuwa na sauti ya pamoja katika kupinga ukatili dhidi ya
wanawake.
- Kuunganisha nguvu za wanawake
pamoja ili iwe nyenzo thabiti kuishawishi serikali kutekeleza ahadi walizoweka
ili kutokomeza ukatili dhidi ya wanawake.
Ndugu mgeni
rasmi,
Nchini Tanzania
katika Siku hizi 16, mashirika, taasisi na idara mbali mbali chini ya mwamvuli
wa Mtandao wa Kupambana na Ukatili wa Kijinsia (MKUKI), Kikosi Kazi cha kuratibu
maadhimisho ya Siku 16 za Kupinga Ukatili wa Kijinsia yakiratibiwa na WiLDAF
yanaungana na wapenda haki wote duniani kuwakumbuka wanawake na wasichana wote
walioathirika na vitendo vya ukatili kama vile kupigwa, kubaguliwa kijinsia,
kukeketwa, kuuawa, wajane kunyang’anywa mali, kunyimwa haki ya kumiliki ardhi na
kadhalika. Ni dhahiri kwamba, ukatili wa kijinsia ni dhana pana inayogusa
jinsi zote lakini kwa kiasi kikubwa wahanga wakubwa wa ukatili huu ni
wanawake.
Ndugu mgeni
rasmi, kampeni ya mwaka huu imekuwa na muitikio mkubwa na msisimko wa aina
yake kwani wadau wengi wamejitokeza katika kampeni hii. Mathalani, Jeshi la
Polisi limekuwa na ushiriki mkubwa na wa kipekee. Kwa kutilia mkazo na
kutekeleza nguzo ya Polisi Jamii, Jeshi la Polisi linaungana nasi kwa kufanya
shughuli mbali mbali za kuhamasisha amani na usalama katika makazi yetu na
maeneo ya barabarani. Kwa kutumia fursa ya rasilimali watu ambayo jeshi la
Polisi linayo, watatoa elimu ya athari na madhara ya ukatili, watahamasisha
jamii kukemea vitendo vyote viovu vinavyosababisha ukatili kwani ukatili wa
kijinsia ni kosa la jinai na pia unachochea uvunjwaji wa amani katika nyumba
zetu na Taifa kwa ujumla. Napenda kutumia fursa hii kulipongeza Jeshi la Polisi
kwa kuchukua hatua hizi. Pia nampongeza Mkuu wa Jeshi la Polisi Inspecta
Generali Said Mwema kwa juhudi kubwa anazofanya. Inatupa faraja kubwa sisi
wanaharakati kuona Jeshi la Polisi limevalia njuga kampeni hii. Hii inatoa
ishara nzuri kwamba kwa kushirikiana nasi basi tutaweza kuutokomeza ukatili
dhidi ya wanawake.
Ndugu Mgeni
Rasmi, pamoja na Jeshi la Polisi, Mashirika mengine yanayoshirikiana nasi na
yana shughuli mbalimbali katika kipindi hiki cha kampeni ya Siku 16 za kupinga
ukatili dhidi ya wanawake ni kama ifuatavyo,
- World Vision watakuwa na kampeni kuhusu afya ya mtoto sasa itakayofanyika Hoteli ya Hyatt Regency, Kilimanjaro, Kempiski
- Chama cha Wanawake Wanasheria (TAWLA) watakuwa na mjadala kuhusu ukatili wa kijinsia tarehe 29 katika ukumbi wa Diamond Jubillee
- Equality for Growth (EFG) watakuwa na uzinduzi wa kupiga vita ukatili wa kijinsia kwa kutembelea masoko mbalimbali ya wilaya ya Ilala, tarehe 5/12/2012
- Engender Health/Champion Project watakuwa na uzinduzi wa kupiga vita ukatili wa kijinsia tarehe 6/12/2012 kwa kutembelea vijiji 20 vya mkoa wa Iringa
- Children Dignity Forum (CDF) watatoa msaada wa kisheria mkoa wa Pwani. Pia wataendesha shughuli mbalimbali kupiga vita ukeketaji tarehe 8/12/2012 katika wilaya ya Tarime mkoa wa Mara.
- Pamoja na mashirika mengine Action Aid, Concern, CSOs coalition na YWCA watakuwa na shughuli mbalimbali za kupinga vita ukatili wa kijinsia.
- Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu wataadhimisha siku ya Tamko Rasmi la Haki za Binadamu na kuhitimisha maadhimisho ya siku 16 za kupinga ukatili wa Kijinsia.
Ndugu Mgeni
Rasmi, uwepo wetu leo hapa katika kuadhimisha uzinduzi wa kampeni ya Siku 16
za kupinga Ukatili wa Kijinsia unaambatana na shughuli mbalimbali zikiwemo za
kutoa msaada wa kisheria kwa waathirika wa ukatili wa kijinsia, maonesho ya
programu mbalimbali za asasi zinazolenga kutokomeza ukatili wa kijinsia, mada
mbalimbali zinazohusiana na ukatili wa kijinsia. Aidha uzinduzi huu una shughuli
mbili za kipekee. Kwanza uzinduzi wa Fomu ya Polisi namba 3 (PF 3), Fomu hii
mpya ya Polisi imefanyiwa maboresho na kuongezewa vipengele muhimu pamoja na
mambo mengine vinavyohusu ukatili wa kingono. Ni imani yetu kubwa kuwa Fomu hii
mpya ya Polisi ni nyenzo muhimu na itasaidia katika ushahidi na hivyo
kurahisisha upatikanaji wa haki kwa waathirika wa ukatili wa
kijinsia.
Ndugu Mgeni
rasmi
Shughuli nyingine ya
kipekee ni uzinduzi wa msafara wa kupinga ukatili wa kijinsia (CARAVAN). Msafara
huu umebeba Mabalozi kutoka makundi mbalimbali ya wanaume, wanawake, vijana na
walemavu. Mabalozi hawa watatoa ujumbe na kuhamasisha jamii za kitanzania
kukemea vitendo vyote vya ukatili wa kijinsia. Aidha, wataunganisha nguvu za
pamoja kwa kuhamasisha jamii zetu kuwa kila mtu mwanaume awe au mwanamke ana
wajibu wa kukemea na kuchukua hatua dhidi ya ukatili wa
kijinsia.
Msafara huu utatembea
katika kanda tatu (3) ambazo ni kanda ya Kaskazini, Mkoa wa Kilimanjaro, Kanda
ya Kati, Mkoa wa Singida, na Kanda ya Ziwa, Mkoa wa Mara-Tarime, ambapo takwimu
zinaonesha kuna kiwango kikubwa cha ukatili dhidi ya wanawake hususan ukeketaji.
Ni matarajio yetu makubwa kuwa msafara huu utakuwa ni chachu kubwa katika jamii
zetu kuanza kuzungumza na kutoa taarifa ya ukatili wa kijinsia dhidi ya
wanawake. Aidha utaamsha ari kwa jamii zetu kuweza kukemea vitendo vyote vya
ukatili wa kijinsia
Ndugu mgeni
rasmi
Kampeni hii ya Siku 16
za Kupinga Ukatili wa Kijinsia itafanyika kikanda. Kanda hizo ni Kanda ya Ziwa
(Mwanza, Mara, na Shinyanga) chini ya usimamizi wa Shirika la KIVULINI na ABC
Foundation, Kanda ya Kaskazini (Manyara, Arusha, Kilimanjaro na Tanga) chini ya
usimamizi wa NAFGEM, Kanda ya Kati (Dodoma, na Singida) chini ya usimamizi
wa AFNET, Kanda ya Kusini (Mtwara, Songea, Mbeya, Iringa na Lindi)
itaadhimisha shughuli hii chini ya kituo cha wasaidizi wa kisheria Iringa na
Kanda ya Kaskazini (Tabora na Kigoma) chini ya Jeshi la Polisi wakishirikiana
na WiLDAF. Aidha kampeni hii mikoani inazinduliwa rasmi
leo 26/11/2012.
Ndugu Mgeni
Rasmi,
Tunafahamu kuwa serikali
ya Tanzania imefanya juhudi mbalimbali za kuzuia na kutokomeza vitendo vyote vya
ukatili wa kijinsia. Juhudi hizi ni pamoja na kutengeneza mpango mkakati wa
kitaifa wa kuzuia na kupambana na ukatili wa kijinsia wa mwaka 2001, kutunga
sheria na sera mbalimbali zinazolenga kuleta usawa kwa mfano:-
- Dira ya Maendeleo ya mwaka
2025.
- Sera ya Maendeleo ya Wanawake na
Jinsia ya mwaka 2000 inayolenga kuwaendeleza wanawake kijamii, kiutamaduni,
kiuchumi na kisiasa.
- Sheria ya Kanuni Za Adhabu Sura Na.
16 hususan vipengele vya makosa ya kujamiiana
- Sheria ya Ardhi Na. 4 na Sheria ya
Ardhi ya Vijiji Na. 5, zote za mwaka 1999 kama zilivyorekebishwa mwaka 2002
zinazolenga kutoa haki sawa ya umiliki wa ardhi kati ya wanaume na
wanawake.
- Mkakati wa Kitaifa wa Kupambana na
Ukatili wa Kijinsia unaolenga kuwa na jamii isiyokuwa na aina yoyote ya ukatili
ifikapo 2015.
Ndugu Mgeni
Rasmi,
Pamoja na jitihada zote
hizi nzuri zinazofanywa na serikali, vitendo vya ukatili wa kijinsia bado
vinakithiri katika jamii zetu. Hivyo basi, tuna sababu za makusudi kabisa
kuishirikisha jamii katika kuzuia ukatili wa Kijinsia kwani kwa kiasi kikubwa
jamii imekuwa ikichochea au ikikubali uwepo wa ukatili wa
kijinsia.
Mathalani katika utafiti
uliofanywa na WiLDAF mwaka 2012 katika magazeti, unaoonesha kwamba taarifa 6,001
za ukatili wa kijinsia zimeripotiwa kwenye magazeti ikilinganishwa na taarifa
3,542 za mwaka 2011.
Ndugu Mgeni
Rasmi, vitendo vya ukatili dhidi ya wanawake sio tu
kwamba vinawadhoofisha kiafya, bali pia vinaathiri uwezo wao wa kushiriki na
kuchangia katika kuleta maendeleo kiuchumi ndani ya familia zao na nchi kwa
ujumla.
Aidha, jitihada za
serikali katika kupunguza umaskini chini ya mkakati wa kuzuia na kutokomeza
umaskini (MKUKUTA) na malengo ya Maendeleo ya Millenia (MDG) hasa lengo kuu la
tatu hayataweza kufikiwa iwapo hakutakuwa na mikakati ya makusudi ya kuhakikisha
kuwa ukatili dhidi ya wanawake unatokomezwa.
Ndugu mgeni
rasmi mwaka huu kauli mbiu yetu ni “FUNGUKA! KEMEA UKATILI DHIDI YA
WANAWAKE. SOTE TUWAJIBIKE” Kauli mbiu hii ina maana kwamba sote tunatakiwa
kuamka katika masuala ya kuzuia Ukatili. Ni vema kutafakari kwa kina jinsi
ambavyo ukatili wa kijinsia, hususan ukatili dhidi ya wanawake unavyoathiri
maendeleo ya familia na nchi kwa ujumla. Sote tunafahamu jinsi jamii
inavyofumbia macho vitendo hivi vya ukatili wa kijinsia vinapotokea, jamii kwa
kiasi kikubwa haitoi ushirikiano kwa vyombo husika kuhakikisha tatizo hili
linapotea.. Hatuwezi kuwa na Taifa imara bila kutokomeza ukatili wa
kijinsia. Hivyo basi, kauli mbiu inaweka msisitizo kuwa ni wajibu wa kila mmoja
wetu kuzinduka na kukemea ukatili dhidi ya wanawake ili kudumisha taifa
imara.
Ndugu Mgeni
Rasmi, katika utekelezaji wa kuzuia na kupambana na Ukatili wa Kijinsia
nchini Tanzania, WiLDAF pamoja na mashirika/taasisi zingine zinazotetea haki za
binadamu zinakabiliana na changamoto zifuatazo:-
- Mgongano wa sheria mbalimbali na sheria kandamizi ambazo bado zinatumika, Aidha ukosefu wa sheria mahususi dhidi ya ukatili majumbani.
- Ushiriki mdogo wa jamii katika kujihusisha katika utetezi na kukabiliana na matatizo ya ukatili wa kijinsia, hususan ukatili dhidi ya wanawake.
- Ukosefu wa fedha za kutosha za kutoa mafunzo na kujenga uelewa wa umma katika masuala ya ukatili wa kijinsia.
- Mtazamo hasi ndani ya jamii unaopelekea kuhalalisha vitendo vya ukatili wa kijinsia uliojijenga kwenye mfumo dume.
- Ushiriki duni/hafifu wa Wizara mbali mbali na hivyo kutokutoa kipaumbele suala la ukatili wa kijinsia katika wizara zao.
- Ukosefu wa takwimu za kutosha kuhusu masuala yanayohusiana na ukatili wa kijinsia
- Ukosefu wa huduma bora za afya katika vituo vya afya kwa waathirika wa ukatili wa kijinsia mathalani sehemu za kuwahifadhi waathirika hao.
- Uelewa mdogo na kutotilia maanani suala zima la ukatili wa kijinsia kwa watoa huduma katika jamii.
- Uchelewashaji wa kesi za ukatili wa kijinsia hivyo kupelekea waathirika kukata tama na kutokuwa na ushirikiano katika kutoa ushahidi na upatikanaji wa haki.
Ndugu mgeni
rasmi
Pamoja na changamoto
hizo bado tunayo nafasi ya kurekebisha hali iliyopo. Hivyo basi sisi wadau wa
kupinga ukatili wa kijinsia tunaiomba wizara yako kuangalia mambo
yafuatayo:-.
- Kuchukua hatua za makusudi za
kutunga sera zinazolenga kuleta usawa, kubadilisha/kurekebisha Sheria ya Ndoa
na kutunga sheria mpya ya mirathi pamoja na Sheria dhidi ya ukatili
nyumbani.
- Tunaomba Wizara yako iunde kitengo
maalumu katika mahakama cha kusimamia kesi za ukatili wa kijinsia, ili kuwezesha
upatikanaji wa haki kwa haraka, kwani haki inayocheleweshwa ni sawa na haki
iliyonyimwa.
- Wizara izidi kuweka msukumo ili
serikali itenge fedha na rasilimali za kutosha kwa ajili ya kuelimisha wanajamii
juu ya haki na wajibu wao kwa mujibu wa sheria na sera zilizopo. Pia kutoa fedha
kwa mashirika yanayotetea haki za binadamu hususan haki za
wanawake.
- Serikali kuanzisha sehemu maalumu
kwa ajili ya hudma za waathirika wa ukatili wa kijinsia (one stop
centre)
- Serikali ijenge hifadhi
zitakazohudumia waathirika wa ukatili wa kijinsia
Mwisho kabisa
tunakutakia kila la kheri katika shughuli zako na Mungu
akubariki.
Mh. Naomi A.M. Kaihula
MWENYEKITI
Post a Comment