RAIS wa Ivory Coast Alassane Outtara amevunja serikali yake kufuatia mzozo kuhusu sheria mpya ya ndoa itakayowapa wanawake haki sawa na waume zao.
Chama cha rais Ouattara, kiliunga mkono sheria hiyo, lakini viongozi wa upinzani waliopo serikalini waliupinga.
Chama cha PDCI, kilichomuunga mkono Bwana Ouattara, katika uchguzi wa November 2010, uliokumbwa na utata, ndicho kilichotoa upinzani mkali.
Wadadisi wanasema kuwa kutoelewana ndani ya serikali ya nchi hiyo kunaangazia hali ya wasiswasi inayozidi kutanda katika nchi hiyo inayokuza kakao kwa wingi duniani.
Hata hivyo, nchi hiyo inaendelea kuimarika taratibu baada ya miezi kadhaa ya machafuko baada ya uchaguzi huo, ambapo rais wa zamani Laurent Gbagbo alikataa kukukubali ushindi wa Bwana Ouattara.
Aliyekuwa mgombea wa chama cha PDCI, Henri Konan Bedie, alikuwa wa tatu kwenye uchaguzi huo, na alipomuunga mkono katika awamu ya pili ya ughaguzi, Bwana Ouattara alimteua waziri mkuu kutoka PDCI.
Lakini wandani wanasema kuwa Bwana Ouattara, kwa sasa anaona kwamba haungwi tena mkono kikamilifu na PDCI, chama kilichotawala Ivory Coast kwa miaka 39 tangu uhuru had mapinduzi yaliyofanywa 1999.
Kama sheria nyingi barani Afrika, sheria za nchi hiyo kwa sasa humpa mamlaka zaidi mume, akiwa kiongozi wa familia, naye hupewa jukumu la kufanya uamauzi kuhusu maswala muhimu ya familia - jambo ambalo chama cha Ouattara cha RDR kilitaka kubadlisha.
Amadou Gon Coulibaly, katibu mkuu katika ofisi ya rais, alisema hatua hiyo ya ghafla la kuvunja serikali lilifanywa baada ya PDCI kupiga kura na kupinga sheria hiyo mpya ya ndoa Jumanne jioni.
Mpambe mmoja wa rais, aliyetaka jina lake libanwe, aliliambia shirika la habari la AP kwamba: "Unaweza kusema kuwa hili lilikuwa tone la maji lililosababisha maji katika jagi yafurike."
Tangu alipochukua hatamu za uongozi mnamo Machi 2011, Bwana Ouattara amesimamia kuboreka kwa uchumi nchini Ivory Coast.
Lakini hatua hizi zinatishiwa na mashambulizi ya mara kwa mara dhidi ya vituo vya kijeshi na miundombinu nchini. Inasemekana kwamba ni washiriki wa Bwana Gbagbo kutoka nchi jirani ya Ghana wanaofanya mashambulizi haya.
Mnamo mwezi wa Septemba, mpaka kati ya nchi hizo mbili ulifungwa wiki mbili baada ya shambulizi dhidi ya kituo cha ukaguzi wa magari.
Kumekuwa na madai kwamba Bwana Ouattara hajitahidi vilivyo kujenga uwiano wa kitaifa kati ya wafuasi wake na wa Bwana Gbagbo.
BBC Swahili
Post a Comment