BAADHI ya
wajumbe wa Kamati ya Usajili ya Klabu ya Simba, wanatarajiwa kwenda Kampala nchini Uganda kwa ajili ya kusaka nyota
watakaowasajili kwa ajili ya kuziba mapengo ya wachezaji wake watatu wa
kimataifa waliowatema hivi karibuni kutokana na kutoridhishwa na mchango wao
dimbani.
Baada ya
mzunguko wa kwanza wa Ligi Kuu Bara kumalizika, Simba imewatema Komambil Keita
wa Mali , Danniel Akuffo wa
Ghana na Pascal Ochieng wa
Kenya .
Mjumbe
mmoja wa Kamati hiyo ambaye hakupenda kutajwa jina lake, alisema jana kwamba,
wanatarajia kuwapata wachezaji hao kupitia michuano ya Chalenji inayoendelea
nchini humo ikishirikishisha miamba 11 ya ukanda wa Afrika Mashariki na Kati,
pia Malawi
iliyoalikwa.
Alisema,
anaamini lengo lao litafanikiwa kutokana na ukweli kwamba, wachezaji wote wazuri
wanaotoka katika nchi hizo, ndiyo waliyomo kwenye vikosi vya timu zao za Taifa
zinazoshiriki michuano hiyo.
“Tumeona
baadhi yetu waende Uganda kwenye Chalenji ili kusaka
wachezaji watatu wa kimataifa watakaoziba pengo la kina Keita, Ochieng na
Akuffo, kwani huko kutakuwa na wachezaji wengi wazuri,”
alisema.
Kiongozi
huyo aliongeza kwamba, kwa upande wa wachezaji wa ndani, tayari wameishaanza
mazungumzo na baadhi ya nyota wanaotarajia kuwasajili katika dirisha dogo la
usajili linalotarajiwa kufungwa Desemba 15.
“Hatuwezi
kusema idadi kamili ya wachezaji wapya wa ndani tutakaowasajili, kwani mpaka
sasa kuna mjadala juu ya suala hilo , kuna wengine watapelekwa kwa mkopo, kuna
wengine tutabadilishana na baadhi ya timu,” aliongeza.
Kwa sasa,
Simba imebakiza wachezaji wawili tu wa kigeni, Mganda Emmanuel Okwi na Mzambia
Felix Sunzu.
Aidha,
Simba ipo katika mazungumzo na wachezaji kadhaa wakiwemo Mkenya Jerry Santo
anayekipiga Coastal Union ya Tanga, Juma Seif
‘Kijiko’ wa Yanga, huku pia ikiwa katika mpango wa kubadilishana wachezaji na
Azam Fc.
Post a Comment