MAMLAKA ya Udhibiti wa
Ununuzi wa Umma (PPRA), imebaini kuwa taasisi 76 za Serikali zimekuwa na
matumizi mabaya ya fedha kupitia utaratibu wa ununuzi wa umma katika kipindi cha
mwaka 2011/12.
Miongoni mwa taasisi hizo,
22 zimebainika kukithiri kwa vitendo vya ubadhirifu vilivyoandamana na rushwa.
Hizo ni pamoja na Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA), Chuo cha Usafirishaji cha
Taifa (NIT), Wizara za Maji na Umwagiliaji na Mambo ya Ndani ya
Nchi.
Akisoma ripoti ya ukaguzi
wa ununuzi wa umma katika kipindi kilichoishia Juni, mwaka huu, Ofisa Mtendaji
Mkuu wa PPRA, Dk Ramadhan Mlinga alisema watawasilisha majina ya wakuu wa
taasisi hizo kwa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), kwa hatua
zaidi.
“Taasisi zote ambazo
zimepata asilimia 20 na zaidi katika viashiria vya rushwa zitapelekwa Takukuru
kwa uchunguzi na hatua zaidi,” alisema Dk Mlinga.
Kwenye orodha hiyo ya
taasisi zitakazopelekwa Takukuru, zimo pia Halmashauri za Wilaya za Kyela,
Makete, Tabora, Bukombe, Sumbawanga na Jiji la Mbeya.
Alisema baada ya
kukamilisha ripoti hiyo ya ukaguzi, bado PPRA itatumia wataalamu wake kuchunguza
kwa undani taasisi ambazo zinakabiliwa na tuhuma.
Kuhusu taasisi nyingine
ambazo pia zinakabiliwa na kashfa hiyo, alisema timu ya wataalamu wake
itaendelea kufanya uchunguzi ili kujua kama chanzo chake ni uzembe, udhaifu wa
kitaalamu au ni mbinu tu za kifisadi.
“Ukaguzi
ulifanyika katika taasisi 121 za umma na ununuzi wote uliokaguliwa ulikuwa na
thamani ya Sh2.4 trilioni... Taasisi zilizokaguliwa 41 ni wizara, idara
zinazojitegemea na Wakala wa Serikali, wakati 45 ni mamlaka na mashirika ya umma
na taasisi 35 za mamlaka ya Serikali za Mitaa.”
Dk Mlinga
alisema waligundua ubadhirifu mwingi kwenye taasisi hizo kupitia taarifa
walizopewa na watu wenye nia njema na nchi.
Pamoja na
kubainika kwa ubadhirifu huo, Dk Mlinga alisema ukaguzi wa jumla unaonyesha kuwa
taasisi za umma zimefanya vizuri zaidi ukilinganisha na miaka ya
nyuma.
Alisema tangu mwaka 2006,
taasisi hizo zimekuwa zikijirekebisha na kufanya vizuri kwenye taratibu za
ununuzi. Hata hivyo, alisema kuna uzembe ambao umekuwa ukifanywa na taasisi
kadhaa ambazo zimekuwa hazizingatii taratibu.
Kaimu Mwenyekiti wa Bodi ya
PPRA, Jaji Thomas Mihayo alitahadharisha kuwa ununuzi wa umma ni moja ya eneo
nyeti ambalo Serikali inapaswa kulichukulia kwa umakini mkubwa kwa sababu ndipo
penye matumizi makubwa ya fedha.
“Asilimia
70 ya fedha zote za Serikali hutumika katika ununuzi. Umakini usipokuwepo
tutajikuta fedha nyingi za walipakodi zinafujwa,” alisema Jaji
Mihayo.
Kwa sababu
hiyo, alisema Bodi ya PPRA inaweka mkazo katika kufumua uozo wote unaofanywa na
taasisi za umma ili kukomesha tabia za ufisadi.
Habari na Leon
Bahati
Chanzo -
Mwananchi
Post a Comment