JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA
WIZARA YA MALIASILI NA UTALII
Waziri Kagasheki
akizungumza na Balozi wa Urusi Alexandr Rannikh
*****************Waziri wa Maliasili na
Utalii Mhe. Balozi Khamis Kagasheki amesema kuwa Tanzania imeandaa Mkakati wa
kutangaza Utalii nchini Urusi.
Mhe. Kagasheki aliyasema
hayo alipokutana na Balozi wa Urusi Bw. Alexandr Rannikh ofisini kwake leo. Nia
kubwa ya mkutano huo ilikuwa ni kuzungumzia namna ya kukuza Utalii
nchini.
Waziri Kagasheki alisema Wizara imeandaa mkakati madhubuti wa kutangaza Utalii kwa nguvu zaidi ndani na nje ya nchi kwa lengo la kupata masoko mapya kama vile Urusi, China na Korea.
Mkakati huo ambao umeandaliwa na Bodi ya Utalii Tanzania (TTB) utazinduliwa leo katika Hoteli Serena Dar es Salaam.
Waziri Kagasheki alisema kuwa anayo hakika kuwa mkakati huo utafanikiwa kutokana na Tanzania kuwa na vivutio vya kutosha na kusisitiza kuwa ulimwenguni nchi inashika nafasi ya pili kwa kuwa na vivutio vingi na vizuri.
Waziri alisema kuwa kabla ya Kipindi cha Awamu ya Nne kumalizika atahakikisha kuwa anachukua hatua za kufanikisha Sekta ya Utalii nchini.
Alisema, baadhi ya mambo atakayohakikisha kuwa yanafanyika ni kuongeza idadi ya vitanda vya kulala watalii, pamoja na kufanya mazungumzo na Mashirika ya ndege ili yaweze kufanya safari zao Tanzania.
Mhe. Kagasheki alisisitiza kuwa kuanzia sasa wawekezaji halali ambao watakuwa wanataka kujenga Hoteli katika maeneo ya Hifadhi, maombi yao yatashughulikiwa haraka iwezekanavyo kwa usimamizi wake mwenyewe.
Naye Balozi wa Urusi nchini Mhe. Alexandr Rannikh alisema kuwa amevutiwa na Tanzania inavyokuza demokrasia yake na kuwa Urusi itaendelea kushirikiana nayo katika masuala ya kukuza uchumi.
Kuhusu Utalii, Balozi
Rannikh alisema amevipenda vivutio vya Utalii vilivyoko nchini na kusema kuwa
kinachotakiwa sasa ni kuboresha utangazaji ili Warusi wavijue vivutio
hivyo.
Kuhusu usafiri wa ndege,
Balozi huyo alisema kuwa Tanzania inatakiwa ianzishe mazungumzo na mashirika ya
ndege ya Urusi, kama vile Aeroflot, ili mashirika hayo yaandae safari ambapo
ndege zao zitatua Tanzania.
Aidha aliahidi kuisaidia Tanzania kuzungumza na wafanyabiashara wa Urusi ili waweze kuja Tanzania kuwekeza katika Sekta ya Utalii.
Balozi Rannikh alisema
pia kuwa yuko tayari kuandaa mazungumzo kati ya Mawaziri husika wa Tanzania ili
wazungumze na Mawaziri wenzao wa Urusi kuzungumzia uwekezaji.
George Matiko
MSEMAJI
WIZARA YA MALIASILI NA
UTALII
Post a Comment