Uharamia na biashara ya
usafirishaji wa binadamu ni changamoto inayotafutiwa ufumbuzi na vyombo vya
Usalama vya Umoja wa Maendeleo wa Nchi za Kusini mwa Afrika
(SADC).
Akizungumza na waandishi
wa habari jijini Arusha leo Mkuu wa kitengo cha Ulinzi na Usalama cha SADC,
Kanali Gerson Sangiza alisema dunia kwa ujumla bado inaangalia namna ya
kutatua tatizo hilo.
Alisema ufumbuzi wa suala
hilo ni mgumu kutokana na ukweli kwamba maharamia na wale wanaojihusisha na
biashara ya uuzaji wa binadamu hushirikiana kwa karibu na kwa siri na wananchi
wa nchi husika. “Tatizo ni kwamba wananchi ndiyo wanaoendesha vitendo hivyo kwa
hiyo namna ya kuwakamata inakuwa ni shida” Alisema Kanali
Sangiza.
Mkuu
huyo aliongeza kuwa ili kukabiliana na tatizo hilo ushirikiano wa karibu kati ya
wananchi na taasisi zinazoshughulikia masuala hayo unahitajika. Mpaka sasa nia
na madhumuni ya biashara hiyo ya uuzaji wa binadamu bado
haijajulikana
na wale waliokamatwa
wakijihusisha na bado wanashikiliwa.
”Inasikitisha kuona
binadamu wengi wanasafirishwa kutoka Somalia kupitia Kenya, Tanzania, Malawi na
kupelekwa Afrika ya Kusini ambapo mpaka sasa Afrika kusini ina wahamiaji haramu
milioni tano”, alisema kanali Sangiza.
Mkuu huyo wa kitengo cha
Ulinzi na Usalama cha SADC alisema pamoja na tatizo la uharamia na usafirishaji
wa binadamu, nchi wanachama wa Jumuiya hiyo pia zinakabiliwa na changamoto ya
matishio ya kufanyika kwa vitendo vya kigaidi ambavyo vinahatarisha uhusiano
kati ya nchi zilizoendelea na zile zinazoendelea.
SADC kupitia chombo chake
cha Ulinzi na Usalama imeandaa mikakati maalumu kuhakikisha kwamba nchi
wanachama wa jumuiya hiyo hazisumbuliwi na matatizo ya uharamia na usafirishaji
wa binadamu. Katika hatua ya kukabiliana na changamoto hizo, wakuu wa Polisi wa
nchi zote 15 za SADC walikutana mwezi Septemba Zanzibar ili kujadili mambo
mbalimbali ya ulinzi na usalama likiwemo tatizo la uharamia na biashara ya
usafirishaji wa binadamu.
Post a Comment