WAPATANISHI wakuu
katika mgogoro wa Mali wanajaribu kukishawishi kikundi kimoja cha kiislamu
kaskazini mwa nchi hiyo kujitenga na tawi la al-Qaida.
Kuna
taarifa kwamba kikundi hicho kiko tayari kuitikia wito huo.
Waziri wa mambo
ya nchi za nje wa Burkina Faso, Djibrill Bassole ambaye anasaidia juhudi za
usuluhishi zinazofanywa na nchi yake kujaribu kuumaliza mgogoro wa Mali uliodumu
kwa miezi saba, amesema atakutana kwa mazungumzo na viongozi wa kikundi hicho,
Ansar Dine mwishoni mwa juma hili.
Ansar Dine
imetuma ujumbe nchini Burkina Faso na Algeria kuzungumzia kupatikana kwa
amani.
Rais wa Burkina
Faso Blaise Compaore ambaye ni mpatanishi mkuu wa Jumuiya ya Kiuchumi ya nchi za
Afrika Magharibi, ECOWAS, katika mgogoro wa Mali, atakutana pia na ujumbe wa
Ansar Dine, hii ikiwa ni kwa mujibu wa waziri wake wa mambo ya nchi za nje,
Djibrill Bassole.
Viongozi wa ECOWAS
wanaongoza juhudi za upatanishi nchini Mali.
Compaore
anatarajiwa kuwaeleza kinaganaga wajumbe wa Ansar Dine matakwa ya ECOWAS, ambayo
ni kulitaka kundi hilo lijitenge na mienendo ya kigaidi na kihalifu, na kurejea
kwenye mchakato wa kisiasa.
Ansar
Dine tayari kuitupa mkono al-Qaida
Kiongozi wa Ansar
Dine Algabass Ag Intalla ameliambia shirika la habari la AFP kwamba kikundi
chake kinajitegemea na kiko tayari kufanya mazungumzo ya amani.
Vile vile
ameelezea utayari wake wa kukutana ana kwa ana na waziri wa serikali ya mpito ya
Mali ambaye kwa sasa yuko mjini Ouagadougou, ikiwa mpatanishi atataka iwe
hivyo.
Afisa wa serikali
ya Mali amesema mkutano baina yao na kiongozi huyo wa Ansar Dine
unawezekana.
Blaise Compaore
anashinikiza kupatikana kwa suluhisho la amani katika mgogoro wa Mali, ingawa
maandalizi ya hatua za kijeshi pia yako mbioni.
Baraza la
Usalama la Umoja wa Mataifa mwezi uliopita lilipitisha azimio linaloutaka Umoja
wa Afrika kufanya matayarisho ya uingiliaji kati kijeshi, ambao utashirikisha
wanajeshi zaidi ya 3,000 kulikomboa eneo la kaskazini mwa Mali.
Ansar Dine ni
mojawapo ya makundi yanayoishikilia sehemu kubwa ya kaskazini mwa Mali, baada ya
kuupiku uasi wa kundi la wapiganaji wa kituareg, kufuatia mapinduzi ya kijeshi
yaliyoiangusha serikali ya Mali mapema mwanzoni mwa mwaka huu.
Kundi hilo
linaloongozwa na Iyad Ag Ghaly, limetuma ujumbe mwingine nchini Algeria, ambayo
pia inapakana na Mali.
Umuhimu wa
Algeria.
Sehemu kubwa ya kaskazini mwa Mali iko mikononi
mwa makundi ya kiislamu.
Kiongozi huyo
amekaririwa na gazeti la Algeria, El-Watan, akisema yuko tayari kuvunja uhusiano
wake na tawi la Al-Qaida kaskazini mwa Afrika, AQIM, na kujiunga na juhudi za
kimataifa kutafuta amani nchini Mali.
Algeria
inachukuliwa kama mshirika muhimu katika mapambano dhidi ya makundi yenye
misimamo mikali ya kiislamu na mwanzoni mwa Juma hili nchi hiyo ilitembelewa na
waziri wa mambo ya nchi za nje wa Marekani, Hillary Clinton, ambaye alikuja
kuunga mkono mchakato wa kutafuta suluhu kwa mgogoro wa Mali.
Vyanzo vingine
vya habari ndani ya kikundi cha Ansar Dine kimeelezea uwezekano wa ujumbe
mwingine wa kikundi hicho kuizuru Nigeria.
Post a Comment