Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi akitoa maamuzi makali yaliyopelekea kuteua Kamati ya kusimamia kumaliza mgogoro wa maeneo ya kilimo katika vijiji vya Dole, Ngurueni na Ndunduke Dole mara baada ya kupokea kero za Wakulima hao.
Mwenyekiti wa kufuatilia matatizo ya wakulima wa Dole na Ngurueni Bw. Daudi Sirus Mukaka akiwasilisha maazimio yao mbele ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif ambayo walikubaliana katika vikao vya awali lakini hayajatekelezwa na hatiame kuleta kero.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi akishuhudia nyaraka bandia walizopewa baadhi ya watu walio nje kabisa ya maeneo ya kilimo ambapo Mkurugenzi wa Ardhi Nd. January Fusi alizibaini baada ya kuwasilishwa kopi zake na wakulima hao. Katikati Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo na Mali Asili Zanzibar Afan Othman.
Baadhi ya Wakulima wa Dole, Ndunduke na Ngurueni Wilaya ya Magharibi wakiwa katika kikao cha kuwasilisha malalamiko yao ya kucheleweshewa kupewa umiliki wa maeneo ya kilimo mbele ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi (hayupo pichani) kilichofanyika skuli ya Wazazi Dole.
Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imezuia utolewaji wa Hati za umiliki wa maeneo ya Ardhi kwa ajili ya Kilimo kwa wakulima wa Vijiji vya Dole, Nguruweni na Ndunduke Dole kufuatia kujichomoza kwa hitilafu za umiliki wa maeneo hayo kwa baadhi ya watu na kusababisha migogoro kwa kipindi kirefu.
Uzuiaji huo umekuja baada ya malalamiko makali yaliyotolewa na Wakulima hao dhidi ya Watendaji na Maafisa wanaosimamia Ardhi na Kilimo wakiwemo pia Viongozi wa Ngazi za kati wa Serikali waliyokuwa wakiyawasilisha kwa Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi.
Malalamiko hayo ya Wakulima yaliyojaa shutuma na lawama wameyatoa katika eneo la Skuli ya Jumuiya ya Wazazi iliyopo Dole Wilaya ya Magharibi yakishuhudiwa pia na Mwakilishi wa Jimbo la Dole na Mbunge wa Jimbo la Mfenesini.
Baadhi ya wawakilishi wa Wakulima hao wa Dole, Nguruweni na Ndunduke walimlalamikia Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif kwamba tatizo hilo sugu lilikuwa likichangiwa na baadhi ya maofisa waliopewa jukumuj la kusimamia maandalizi ya utolewaji wa nyaraka kwa wakulima 28 wa awamu ya kwanza waliokubalika kupatiwa hati ya umiliki huo.
Wamesema Maafisa hao walidiriki kutumia hadaa ya kuchomekea majina ya Watu wengine ambao cha kusikitisha zaidi hawaishi wala kutambuliwa katika maeneo hayo ya wakulima.
Kwa upande wake Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo na Mali asili Zanzibar Bw. Afan Othman amesema Wizara hiyo itahakikisha inafanya utaratibu wa uhakiki wa maeneo hayo ambayo yalikuwa katika umiliki wa Wizara hiyo kabla ya kumilikishwa kwa Wakulima wa maeneo hayo.
Naye Mkurugenzi wa Ardhi Ndugu January Fusi amesema wakati umefika hivi sasa kwa kuiangalia upya sheria ya umiliki wa ardhi kwa ule utaratibu wa eka tatu tatu waliopewa wananchi kwa ajili ya kilimo mara baada ya Mapinduzi ya Zanzibar ya mwaka 1964.
Mgogoro wa maeneo ya ardhi kwa ajili ya Kilimo katika Viji vya Dole, Ngurueni pamoja na Ndunduke Dole umeibuka tokea mwanzoni mwa miaka 2000 na kuanza kushughulikiwa na Waziri Kiongozi Mstaafu Mh. Shamsi Vuai Nahodha.