Rais wa FIFA, Joseph 'Sep'
Blatter
TOKYO, Japan
"Tutakaa na Uefa kuzungumzia aina sahihi ya adhabu
zinazopaswa kuchukuliwa kwa makosa kama haya katika soka – na hii sio kwa Uefa
tu, bali kwa mashirikisho yote ya soka ya mabara na vyama vya kitaifa. Lazima
tuwe thabiti, wenye nguvu, tena wakali"
RAIS wa Shirikisho la Soka la Kimataifa (Fifa), Sepp
Blatter amesema anapanga kukaa mezani na Rais wa Shirikisho la Soka barani Ulaya
(Uefa), Michel Platini kujadili adhabu waliyopewa Chama cha Soka cha
Serbia.
FA ya Serbia imepigwa faini ya pauni 65,000 na Uefa, baada
ya kukutwa na hatia ya udhalilishaji na ubaguzi wa rangi uliofanywa na mashabiki
na wachezaji wa timu ya vijana, wakati wa mechi dhidi ya vijana wenzao wa U-21
wa England Oktoba mwaka huu.
"Nitakuwa na mkutano na Rais wa Uefa," alisema Blatter,
alipoongea kwenye mkutano na vyombo vya habari jijini hapa na kuongeza: "Lakini
sijui kama (Platini) ana ushawishi kwa Kamati ya Nidhamu ya Uefa kuweza
kuyatazama upya maamuzi yao."
Platini ameripotiwa kutafakari rifaa kwa Kamati ya Nidhamu
iliyo chini ya shirikisho lake juu ya ukali wa adhabu hiyo ambayo pia imefunga
milango ya Serbia kushiriki michuano ijayo ya vijana wa U-21.
Wachambuzi wa masuala ya soka wameishangaa faini iliyopigwa
Serbia, huku wakilinganisha na ile ya pauni 80,000 ya aliyolimwa Nicklas
Bendtner kwa kuonesha tu nembo ya mdhamini wake wa nguo za ndani wakati wa
fainali za Mataifa Ulaya 2012.
Katika mkutano huo, Blatter alikwepa kujibu swali
aliloulizwa na mwandishi wa BBC Sports kama haoni kuwa adhabu ya Uefa kwa Serbia
ni rafiki mno kwa wabaguzi wa rangi na wadhalimu viwanjani.
Badala yake akajikuta akijibu: "Nina uhakika kwamba tutakaa
na Uefa kuzungumzia aina sahihi ya adhabu zinazopaswa kuchukuliwa kwa makosa
kama haya katika soka – na hii sio kwa Uefa tu, bali kwa mashirikisho yote ya
soka ya mabara na vyama vya kitaifa.
"Lazima tuwe thabiti, wenye nguvu, tena wakali hasa
linapokuja suala la ubaguzi wa aina yoyote, ukiwamo huu tupigao vita kila uchao
wa rangi," alisisitiza Blatter



Post a Comment