Hoteli
ya Kitalii iliyopo Oysterbay jijini Dar es Salaam, yenye hadhi ya nyota tano
imeumbuka baada ya kubainika kumwaga maji ya chooni
baharini.
Madudu ya
hoteli hiyo inayotambuka kama Double Tree by Hilton, yamebainika baada ziara ya
kushtukiza iliyofanywa na Naibu Waziri, Ofisi ya Makamu wa Rais (Mazingira),
Charles Kitwanga, pamoja na maofisa waandamizi kutoka Baraza la Taifa la
Mazingira (Nemc).
Ziara hiyo
imebaini kwamba mfumo wa majitaka ya hoteli hiyo haujajengwa vizuri kuruhusu
maji hayo kusafishwa kabla hayajamwagwa au kuingizwa kwenye mfumo wa Kampuni ya
Majisafi na Majitaka Dar es Salaam (Dawasco).
Kitwanga na
maofisa hao wa Nemc walifika kwenye hoteli hiyo majira ya saa 7:00 mchana na
kuhoji mfumo wa majitaka pamoja na sababu za hoteli hiyo kujengwa hadi
baharini.
Mameneja wa
hoteli hiyo walimweleza Naibu Waziri kwamba maji hayo yanahifadhiwa vyema na
kisha kuzolewa kwa magari ambayo huenda kuyamwaga kwenye mabwawa ya
majitaka.
Hata hivyo,
Kitwanga alihoji linapopita gari la kuja kuchukua maji hayo kwa kuwa eneo zima
limezungukwa na majengo pamoja na ukuta usioruhusu gari kupita.
Baada ya
kuendelea kukagua, ndipo ilibainika kwamba uchafu wote wa hoteli hiyo na hasa
maji ya chooni yanamwagwa baharini.
"Tulichoona
hapa ni kinyesi kabisa, harufu ya maji ya chooni inatoka halafu hawa
wanatudanganya eti ni mtiririko wa maji wa kawaida, hali hii haikubaliki,"
alisema Kitwanga.
Kitwanga
alisema serikali inawahamasisha wawekezaji waje kuwekeza nchini, lakini kwa
kufuata sheria, kanuni na taratibu, vinginevyo itawachukulia hatua
stahiki.
Alimweleza
Mkurugenzi Mkuu wa hoteli hiyo, Sven Lippinghof, kwamba kumwaga kinyesi baharini
ni suala lisilovumilika na kumtaka kuzingatia sheria ya mazingira na nyinginezo
ili kulinda afya ya viumbe wa baharini na za wananchi.
Naibu Waziri
huyo aliitaka Nemc kufuatilia kwa kina usitishwaji wa kumwaga maji hayo na kumpa
mwekezaji huyo wiki moja kwamba hadi Ijumaa ijayo awe amefanya marekebisho ya
kina.
Kwa upande
wake, Mwanasheria wa Nemc, Manchere Heche, aliitaka hoteli hiyo kusitisha
kumwaga maji hayo baharini kuanzia jana na kumwandikia barua ya kusisitiza amri
hiyo.
Alisema
kuanzia leo, Nemc itafanya ukaguzi katika eneo hilo ili kuhakikisha kwamba agizo
hilo linatimizwa.
"Napenda tu
nikuhakikishie Mheshimiwa Waziri kwamba suala la afya ya wananchi ni la msingi
na muhimu, leo hii (jana) kwamba Nemc inawataka msitishe kumwaga haya maji na
nitawaandikia barua leo kusisitiza hili," alisema Heche.
Alisema: "Afya
za watu haziwezi kusubiri muda, na tutawatoza faini kwa uchafuzi huu wa
mazingira."
Kwa upande
wake, Lippinghof alisema atatekeleza maagizo hayo ya Nemc na kwamba suala la
kuzingatia sheria halina mjadala.
Alisema
atawasilisha pia maagizo hayo kwenye kikao cha bodi ya wakurugenzi wa hoteli
hiyo kwa hatua kubwa zaidi.
Awali, ziara
hiyo ilifanyika pia kwenye hoteli ya Giraffe ambayo ilibainika kuchafua bahari
na kuagizwa kufanya usafi kila siku.
Kadhalika,
Waziri Kitwanga aliiagiza Nemc kusimamisha ujenzi wa hoteli ya Blue Pearl
inayojengwa karibu na Giraffe kwa kuwa imejenga ukuta baharini na hivyo kuinyima
bahari kupumua.
Katika ziara
hiyo, kiwanda cha Coca cola Kwanza ndicho pekee kilichoonekana kuzingatia sheria
ya mazingira kwa kujenga mfumo wa kusafisha maji yenye sumu kabla
hakijayamwaga.
Maeneo mengine
ambayo yalitembelewa na Naibu Waziri huyo ni kiwanda cha dawa Sheyls
Pharmacetical, hoteli za Whitesands na Corol Beach ambazo zilipewa maelekezo
madogo baada ya kubainika kutotimiza masharti ya sheria ya
mazingira.
CHANZO:
NIPASHE
Post a Comment