JAMHURI YA MUUNGANO WA
TANZANIA
WIZARA YA MAMBO YA NDANI YA
NCHI
JESHI LA POLISI
TANZANIA
TAARIFA KWA
VYOMBO VYA HABARI TAREHE 14/12/2012
KWA NINI
LAMBALAMBA WANAPIGWA VITA DODOMA
Kwanza ni lazima
tufahamu Lambalamba ni nini?
Hili ni kundi la watu
ambalo wameliunda kwa lengo la kujihusisha na vitendo vya kitapeli na ulaghai
kwa wananchi hususani wa vijijini, ili kujipatia mali zikiwemo fedha na mifugo
ya aina mbalimbali toka kwa wanavijiji katika mkoa wetu wa
Dodoma.
Kundi hili ni mkusanyiko
wa watu wa jamii tofauti ambao wanatoka maeneo ya Rufiji , Pwani, Tanga na
Morogoro ambao wamekuja kuivamia jamii ya watu Dodoma ambayo nayo ina mila na
desturi zake katika mambo ya jadi.
Wamekuwa wakitumia
mtindo wa kujifanya kuwa wao ni waganga wa tiba za jadi kwamba wana uwezo wa
kutoa vitu vya kichawi katika majumba ya watu, sehemu za biashara na pia
kufichua wachawi, vitu ambavyo kwa hakika hawana uwezo
navyo.
Ili mtu akubalike kuwa
ni mganga wa tiba za jadi ni lazima afahamike katika eneo analofanyia shughuli
zake hizo kuanzia uongozi wa ngazi ya chini hadi wa juu wa serikali na awe na
kibali cha kuendesha tiba hizo kisheria kitu ambacho kundi la lamba lamba
hawakidhi matakwa hayo.
Pia Mganga wa jadi kwa
asili yake hatakiwi kufanya kazi zake kwa kuita baadhi ya watu ni wachawi.
Hutakiwa kutoa tiba na kinga kwa kutumia miti shamba kulingana na uwezo wake, na
sio wanachofanya hao wanaojiita lambalamba hii ni tofauti na sheria
zinavyoelekeza.
Kwanza wanavijiji
huchangishwa na ndipo huitwa kundi hilo kuja kufanya kazi wanayodai ni ya
kufichua wachawi au washirikina, ambao wanadai wanavuta mali za watu wengine
kwao na kuwa matajiri.
Uchunguzi wetu umebaini
kwamba wanachofanya kundi la lambalamba kwa kushirikiana na washirika wao, huwa
wanapandikiza vitu kwenye nyumba, mashamba au sehemu za biashara za mlengwa
nyakati za usiku.
Baada ya kufanya hivyo
ndipo wanaondoka na kundi la watu na kwenda kutoa vitu ambavyo
walishavipandikiza kabla, kisha kinachotokea kwa anayefanyiwa hivyo ni
kudhalilika yeye na familia yake kuwa ni mchawi na kibaya zaidi hulazimishwa
kutoa kiasi cha fedha na mifugo kama adhabu na kutishiwa wasithubutu kwenda
kutoa taarifa Polisi.
Hili ni kosa la jinai na
ukiukwaji mkubwa wa haki za Binadamu, hatuwezi kuvumilia na kuwaacha wananchi
wenzetu kuendelea kupoteza fedha na mali zao kwa kuwanufaisha hao
matapeli.
Zipo taarifa kuwa
lambalamba hao wanapofika vijijini hutafutiwa wanawake wa kuwapikia na
kuwastarehesha. Huu ni unyanyasaji wa kijinsia na jambo la hatari ambalo
litachangia kuenea kwa magonjwa ukiwemo UKIMWI.
Haya yanayofanyika ni
utapeli mkubwa uliobuniwa na watu hao wa kujipatia fedha. Ni jambo
linalodhalilisha, linalojenga chuki, na uchochezi ndani ya jamii. Pia
linahatarisha usalama na amani pamoja na afya za wanawake na jamii kwa
ujumla.
Hili ni jambo la kukemea
kuanzia ngazi ya Familia, Kitongoji, Mtaa, Kata hadi Taifa. Wote kwa pamoja
tunaona athari zake tukemee kwa nguvu zote na wale wanaoendesha na kushabikia
kundi hilo watolewe taarifa ili wakamatwe.
Watu wasiogope kutoa
ushahidi dhidi ya kundi la lamba lamba na washirika wake hao wanaovuruga amani,
utulivu, usalama na kurudisha maendeleo nyuma.
Tupo kwenye karne ya
Sayansi na Teknolojia tusijiaibishe kwa kukumbatia mambo ya zama za kiza kwa
kupumbazwa akili zetu na matapeli waliobuni mradi wa kujipatia fedha na mali kwa
ujanja wa kupandikiza vitu kwenye nyumba, sehemu za biashara na mashamba, kisha
baadaye wanakuja kuvitoa na kudai wamefanya hivyo kwa uwezo wao wa kubaini
wachawi na kuifanya jamii yetu iishi kwa chuki na kukosa amani na kushindwa
kufanya shughuli za kujiletea maendeleo
Mwisho napenda
kutoa wito kwa wananchi kwa ujumla kupitia dhana ya utii wa
sheria kwa hiari kushirikiana kwa pamoja na Jeshi la Polisi kwa kutoa
taarifa za watu hao ili kuutokomeza uhalifu huu ili jamii yetu iendelee
kubaki salama na yenye amani na utulivu.
[D. A. MISIME –
ACP]
KAMANDA WA POLISI [M]
DODOMA
CONTACT:
POLISI MKOA WA
DODOMA
DAWATI LA HABARI, ELIMU NA
MAHUSIANO


Post a Comment