Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Bw. Ban Ki Moon amerudia tena wito wake kwa utawala nchini Syria kutotumia silaha za sumu akisema kama zitatumika itakuwa ni makosa makubwa ya uhalifu dhidi ya ubinaadamu.
Ban Ki Moon ametoa wito wa kusitishwa kwa mapigano na kufanyika kwa majadiliano ya amani baina ya serikali na waasi na amelitaka Baraza la Usalama la Umoja wa mataifa kuwa na msimamo mmoja na kuchukua hatua inayostahiki kumaliza mgogoro huo.
Wakati huo huo waasi nchini Syria wametangaza kuwa sasa uwanja wa ndege kwenye mji mkuu wa nchi hiyo Damsacus, ndio shabaha yao kuu, na wametoa onyo kwa abiria na ndege kutoutumia uwanja huo, kwamba yatakayotokea ni juu yao wenyewe.
Mapigano yamezidi kupamba moto kwenye mji huo kwa wiki nzima sasa, yakizipa hisia nchi za magharibi zinazompinga Rais Bashar al-Assad kuwa muda wa kuondoka kiongozi huyo unanukia.